Kamati ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio (revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20 kujihusisha na mpira wa miguu.
Sekretarieti
ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili
kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati ya
Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.
Uamuzi
huo wa mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya waandishi wa
habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Victoria
Makani.
Rukambura
amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama
za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu cha 73(3)(b) cha
Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu yake itamalizika Oktoba 15,
2033.
Kabla
ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa
TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya Mwanza, na fomu zake
za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha
Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Pia
imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya TFF
inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za kawaida, na
kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo (judicial organs),
Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye
Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa
Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia
ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu
Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa
kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Hivyo
Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF ya
kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Kamati
ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja anayotakiwa
kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo atafungiwa mwaka
mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a),(c) na (h) cha
Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Akilipa
faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius
Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(a)
cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa ana adhabu ya
kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa
(RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba uongozi TFF.
Hivyo,
amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya RUREFA
ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti
ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo wakati
akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa
Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha fomu yake ya kugombea.
Naye
Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na
kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya Utendaji bila kibali na
kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa Ibara ya 12(2) na
Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.
Amepigwa
faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo
akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza kuendelea na
mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile
Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya
Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.
Pia
Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga Tambwe kwa
mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwa
kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu ya kinidhamu
inayomalizika 2014.
Hivyo,
amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na ile ya
kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF, Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania
(FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa kupokea na kuidhinisha fomu zake
za kugombea uongozi wakati akitumikia adhabu ya kufungiwa.
Kamati
ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili kama
ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala na Omar Isack
Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata Katiba na Kanuni za
TFF.
Blogger Comment
Facebook Comment