BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imewapatia mikopo wanafunzi 1000 kwa awamu ya kwanza , mwaka wa masomo 2013/2014 .
Wanafunzi hao ni wa shahada ya kwanza, ya pili na udaktari (PhD) ambao
watasoma katika vyuo vya ndani, Tanzania Bara na nje ya nchi.
Wanafunzi wa shahada ya kwanza waliopatiwa mikopo ni 800, shahada ya pili 193 na PhD wanafunzi 7.
Mwenyekiti wa bodi hiyo,Kombo Hassan Juma alisema kati ya wanafunzi hao
wanaume ni 513 na wanawake 487 wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Alisema kiwango hicho ni sawa na ongezeko la wanafunzi 113
ikilinganishwa na wanafunzi 887 waliopatiwa mikopo mwaka wa masomo
2012/2013.
Alisema mbali ya wanafunzi hao wapya, bodi inaendelea kuwahudumia
wanafunzi 1,361 wanaoendelea na masomo katika vyuo vya ndani na wengine
158 walioko nje ya Tanzania .
Mwenyekiti huyo alisema kufuatia uteuzi huo mpya bodi itakuwa na
wanafunzi 2,527 wanaohudumiwa kwa mwaka wa masomo 2013/2014, ambapo
jumla ya shilingi bilioni 8.7 zimetengwa.
Alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 4 zitatumika kwa wanafunzi
wanaoendelea na bilioni 4.7 zimetengwa kwa wanafunzi wapya.
Alisema fani zilizopewa kipaumbele ni uvuvi, usimamizi wa biashara,
hesabu, masoko, fedha, rasilimali watu, ujasiriamali, utabibu, usimamizi
wa hoteli, viwanda, madini, mazingira, mawasiliano na usafirishaji.
Kada nyengine ni kompyuta, ufundi, kilimo cha mazao ya baharini,
manunuzi na ugavi, utalii, ualimu wa sayansi na hesabu, mafuta na gesi
na ualimu wa sanaa.
Naye Mkurugenzi wa bodi hiyo,Iddi Khamis Haji aliwataka wanafunzi
waliobahatika kupata mkopo kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze
kuwanufaisha wanafunzi wengine.
Aidha alisema changamoto kubwa inayowakabili ni uwezo mdogo wa kifedha
ikilinganiswa na idadi ya mahitaji ya wanafunzi ambapo jumla ya fomu
4,310 sawa na asilimia 86 zilikataliwa.
Source - ZanziNews
0 comments :
Post a Comment