-->

VURUGU ZAZUKA BAADA YA SHEKH BASALEH KUZIMIWA KIPAZA SAUTI


Jana katika msikiti wa Idrisa uliopo kariakoo Dar es salaam zimezuka vurugu kubwa, baada ya muumini mmoja kumzimia kipaza sauti Sheikh Maalim Ally Basaleh na kupinga nafasi aliyopewa ya kuongea na kuwaombea dua waislamu waliohudhuria msikitini hapo.

Akizungumza na Blogu ya ahbaabur rasuul muumini aliyeshuhudia tukio hilo bwana Ramadhani Issa alisema, Sheikh basaleh alipewa nafasi hiyo baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa na Imamu msaidizi wa msikiti huo.

Sheikh Basaleh aliombwa kuwasalimia Waislamu na kuwaombea dua baada ya kurudi toka Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hijja.

Anasema Ramadhani aliposimama Sheikh Basaleh na kuanza kuzungumza ndipo muumini mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, akasimama na kwenda kuzima kipaza sauti ili Sheikh Basaleh asizungumze.

Baada ya tukio hilo zikazuka vurugu kubwa na sintofahamu msikitini hapo ambapo ilibidi waitwe polisi kutuliza vurugu hizo ambao walimchukua mtu huyo na kuondoka nae. Haijafahamika kama mtu huyo amefunguliwa mashtaka ama la.

Kutokana na vurugu hizo Sheikh basaleh hakuweza kuzungumza wala kuwaombea dua waislamu waliokuwepo msikitini hapo. Hakuna mtu yeyote alijeruhiwa katika vurugu hizo.

Msikiti wa Idrisa katika siku za hivi karibuni umekumbwa na vurugu za hapa na pale baada ya watu wanaodaiwa ni waumini wa msikiti huo kufanya mapinduzi ya kiuongozi kwa madai kuwa uongozi uliokuwepo madarakani umeshindwa kuendesha msikiti na kupelekea uduni wa huduma za msikiti huo kwa waumini wanaosali msikitini hapo.

Jitihada za kumtafuta Sheikh Basaleh na upande unaopinga uongozi kupata maelezo yao zinaendelea kufanywa.

 
HABARI KUTOKA AHBAABUR
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment