Namna ya ‘kumteka’ mteja
SIKU zote ni rahisi kumpata mteja ila ni
vigumu kumfanya abakie kuwa wako.
Hili ni tatizo kubwa linalowakumba
wafanyabiashara wengi, wateja wanakuja kwenye biashara zao mara moja au mbili
kisha hawaonekani tena, jambo ambalo limekuwa likiibua hisia tofauti kwa
wafanyabiashara.
Wafanyabiashara wengine wanasema wana gundu,
wamerogwa au bidhaa ni mbaya. Unakuta mfanyabiashara ana bidhaa nzuri, huduma
inaridhisha lakini anashindwa kumfanya mteja anayekuja kwenye biashara yake
aendelee kuwa mteja wake wa kudumu.
Hili linatokana na huduma mbaya kwa wateja
inayosababishwa na mazingira machafu ya biashara yasiyovutia, vifaa chakavu,
lugha mbaya na mteja kutohudumiwa kwa wakati.
Kwa upande mwingine tatizo hili
linasababishwa na kutokuwa na utashi wa kujua aina za wateja
maalumu na namna maalumu ya kuwahudumia kwa maana ya tabia zao na namna ya
kuwahudumia.
Wafanyabiashara wengi wamekosa utashi wa kujua
aina za wateja, tabia zao na namna ya kuwahudumia, suala linalosababisha kuona
kuwa wateja ni watu wa kutanga tanga, hawashikiki au hawana sehemu maalumu ya
kununua bidhaa au huduma, jambo ambalo si kweli.
Kutanga tanga kwa wateja kuna sababishwa na
wafanyabiashara wenyewe kushindwa kuwafanya waendelee kubaki kuwa wao na
wasiende kwingine.
Hapa huna haja ya kwenda kwa mganga ili kumfanya
mteja abakie kuwa wako, bali ni kwa kutumia kanuni za kibiashara ambazo ni
kuuza bidhaa zenye ubora, kutumia lugha nzuri, kuwa mbunifu, kumpa mteja zaidi
ya kile alichokitarajia.
Kwa mfano, wenzetu wanaouza dawa za meno
wanaweka zawadi ya mswaki au dawa ndogo ya kuwavutia wateja.
Kwa kina mama wanaotoa huduma ya chakula
ukiagiza chakula wanakuletea na matunda kidogo; ndizi au kipande cha
parachichi, ambapo haukilipii, ni bure, chakula tu ndicho unalipia.
Kutokana na ubunifu huo wateja wanakuwa wengi kwasababu
wanavutiwa na wanahisi kuwa wanapata zaidi ya kile wanachokilipia, wanaridhika
na kuifurahia huduma hiyo na wengine wanashindwa kuvumilia kuridhika huko na
kufurahishwa, matokeo yake wanawaambia wenzao na wenzao wanawaambia wenzao!
Matokeo yake habari nzuri zinasambaa kuhusu huduma yako au
bidhaa, wateja wanazidi kumiminika, unajikuta umejenga mtandao mkubwa wa wateja
na kushinda ushindani ulioko kwenye biashara husika.
Mara nyingi wafanyabiashara wanajisahau katika
hili la kumpa mteja zaidi ya kile anachokitarajia, wanafanya hivyo wakati
wanaanzisha biashara zao mpya, wakiona biashara imezoeleka kidogo wanasitisha
na wateja nao wanakata miguu.
Hapa sizungumzii promosheni bali nazungumzia
jambo endelevu litakalomfanya mteja aendelee kuwa wako na asiende kwa mtu
mwingine.
Kumpa mteja kitu cha ziada zaidi ya kile
alichokuwa anakitarajia kutoka kwako, namaanisha kile kitu ambacho ukimpa
hakiwezi kuathiri biashara yako na hapa
ni suala la ubunifu zaidi ndio unahitajika.
Kwa haraka haraka ukiangalia unaweza kuona
unapata hasara lakini ukifanya uchunguzi wa kina utagundua kuwa
sehemu hizo zinapata faida kubwa ukilinganisha na idadi kubwa ya wateja
wanaokuja katika biashara hiyo na ‘kuwaungisha’.
Sehemu nyingine nimeona wafanyabiashara
wanaouza biashara nzuri ila wanakabiliwa na ukosefu wa wateja wa kutosha na
kuamua kutumia mbinu ambazo hazizai matunda.
Mfano
unakuta nje ya biashara kuna bango limeandikwa: “Ukimleta mteja akanunua
bidhaa tunakulipa.”
Binafsi niliona kuwa mbinu hii haina ushawishi
mkubwa na inaonekana kuwa inashurutisha zaidi na ni ya kizamani,
wafanyabiashara hao wamekosa utashi wa kibiashara, mbinu za kijasiriamali
ambazo wakati mwingine hazihitaji matumizi makubwa ya nguvu ya pesa au mwili,
bali ni kufuata mbinu na kanuni za kijasiriamali, kisha utashangaa wateja
wanakuja, huna haja ya kutafuta watu wakupigie debe biashara yako.
Mbinu hizo nilizozitaja hapo juu na
juhudi za kuwavutia wateja katika
biashara yako zinatakiwa ziambatane na utashi wa kujua aina za wateja, tabia
zao na namna ya kuwahudumia ili uweze
kupata mbinu zaidi zitakazokupa nguvu na uwezo wa kumfanya mteja abakie kuwa
wako.
Ukizijua aina hizi zitakusaidia kuwavutia
wateja na kuliteka soko la biashara kwasababu biashara ni wateja.
Kuna aina sita za wateja maalumu pamoja na
tabia zao na jinsi ya kuwahudumia, ambao ni kama wafuatao:
Mteja mkimya ni mteja anayelalamika kimoyo
moyo, ukimhudumia mteja huyu vibaya anakuambia hakuna shida lakini ndani ya
nafsi yake kuna shida, na hataonekana tena kwenye biashara yako.
Mteja mgomvi ni muwazi na mlalamikaji,
unatakiwa umsikilize kwa makini, akikutuma kitu fulani muulize kama atahitaji
kingine na kama atakuambia una makosa ukubali.
Wafanyabiashara wengine wanaambiwa kuwa wana
makosa wanakataa, wanawaambia wateja: “Nyie hamna hela.”
Wengine huhoji
mbona kulikuwa na hivi miaka mingi lakini sasa havipo, inawezekana
ulipata wateja wengi ambao ni wakimya
hawakukuambia ukweli kuhusu huduma za bidhaa yako.
Mteja mgomvi atakusaidia ujue matatizo
yaliyoko kwenye biashara yako na kuyatatua.
Mteja mstaarabu hutegemea bidhaa nzuri,
hulalamika si kama mkimya, anaweza kukuita na kukueleza, hana maneno mengi,
anategemewa asikilizwe, asemi kwa watu wengi
bali anakwenda kuitafuta bidhaa hiyo sehemu nyingine.
Huyu hapendi visingizio, anapenda maelezo
yaliyonyooka. Kuna wahudumu au wafanyabiashara wanawaeleza wateja uongo mwingi
na hilo tu linatosha kumfukuzisha mteja kwenye biashara yako na unaweza
usimuone tena.
Mteja tapeli ni aina nyingine ya mteja ambaye
lengo lake ni kujipatia vitu ambavyo hastahili na unaweza kuwajua kwa kuangalia
tabia zao, ikiwamo kuuliza bei hata kama anaiona, hupenda kugusa gusa bidhaa,
ananung`unika sana, anakuuliza maswali ambayo huwezi kumjibu.
Namna ya kumhudumia ni pamoja na kuzingatia
misingi ya taaluma au biashara husika, kutomwacha awe mbali muda mrefu na wewe
kwa sababu anaweza kukuta vitu vinavyobebeka akaondoka navyo.
Kitu kingine, usimwonyeshe bidhaa moja kabla
hajakupa nyingine, usimwonyeshe bidhaa zaidi ya mbili hiyo inaweza ikawa fursa
ya kukuchanganya kwa wingi wa bidhaa ulizompa na kushindwa kujua ni ipi
amechukua kwa muda huo anapokurudishia na kukuambia kuwa atakuja siku nyingine
au anaweza akawa amenunua ila amezidisha kipimo cha bidhaa zaidi ya pesa
aliyoitoa.
Fikiria namna ya kumfanya aendelee kuwa mteja
wako, anaweza kuwa mwizi na ni mteja vilevile.
Mteja aliyekubuhu kwa kulalamika ni aina ya
mwisho ya mteja anayeweza akawa anakuja njiani huku analalamika kabla hata
hajafika dukani, mteja wa aina hii haridhiki kwa lolote hata ukimpa nyongeza
anaona ni kidogo.
Usifike mahali ukashindwa kumfanya mteja
aendelee kuwa wako kwa sababu ya tabia yake, kwa kuwa tayari una ufahamu na
maarifa ya namna ya kumhudumia, hivyo itakusaidia katika kukuza biashara na
kufanikiwa zaidi kwa kuwa na wateja wengi ambao hawatakuwa tayari kwenda kwa
mfanyabiashara
Source:tanzania daima
Blogger Comment
Facebook Comment