Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia
utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa
sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba,
2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba.
Lakini, baada ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na
nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni
radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka
hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya
uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na
wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi
kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjiniKampala.
Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa
Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa
mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia
kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama
ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi
wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi
kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na
Tanzania na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika
hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya
majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu
zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa
hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe
ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29
Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni
maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226walikamatwa wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe
ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na
vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711walikuwepo
kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote
aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale
watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni
ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa
wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri
jambo hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi
nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku
zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni
kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa
uraia. Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au
walikotoka wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao
walilazimika kuachia nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia.
Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao
wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali
mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu
waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi
wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala
kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu.
Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti, taarifa itolewe kwa Wakuu
wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua zipasazo
zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT,
Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa
Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia,
nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa
Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya
Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba, 2013 na
kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si
mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa
bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada na
Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo
nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu
tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea
kupata licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na
uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara
zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri
wa Wizara hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila
kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini
Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa
Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa
Bunge la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano
baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa
mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa
ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi
yetu ya kupatiwa vitabumilioni 2.4 vya sayansi na hisabati
yamekubaliwa na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo
utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya
umeme na barabara za vijijini za kugharamiwa na Serikali ya Marekani
kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia yamepokelewa vizuri.
Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani
cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo
lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na
“International Congressional Conservation Foundation” kwa kutambua
juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori na
mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana
nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada
tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi
wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa
moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo
zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa
Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili
na biashara ya meno ya tembo duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha
kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa
Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada
kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya
mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development Agenda: Setting the Stage.
Kama mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka
2015.
Katika
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike
baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa kufanya
tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000
umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na
kwa dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na
jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika kila nchi. Yapo
malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa na yapo
ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile vile
yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
(1) Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2) Lengo
la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi
na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko
wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika
elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo
kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa
kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo
katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
(3) Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
(4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
(5) Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia
shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa
maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama
tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu.
Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira
mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo
ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha
hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la
Milenia namba 1kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya
nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi
katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza
mapato ya wakulima. Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango
cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa
kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash Transfer ili
tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa kuutekeleza
mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini ya
lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama
wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama
wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya
uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo
mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia
ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo
vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana
mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia
kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu
tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya
lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo
la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao
kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati
mbaya sana mataifa
tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile
wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza
ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti
kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo
ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna
nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote
kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa
yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya
Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina budi
kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo
ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale
paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya
mwaka 2015.
Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati
nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la
kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko Nairobi, Kenya.
Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa.
Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta
na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika
wakati huu wa majonzi.
Nafahamu
kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu
kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998
Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa
inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi
katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku
hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na
ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo
zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada
ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha
mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema
kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna
kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni
kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu
vifanikiwe zaidi.
Hali
kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi
kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za
ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka
vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua watu wanaweza
kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya
kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba
muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa
makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama
wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama
wake, wa kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi
na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za
tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi
kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka,
Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria
hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi
zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na
imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni
kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya
na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi
sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba
itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge
Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi
kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya hatua
hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote
vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala. Majadiliano
yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la
asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa
awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo
yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama
ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika
mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya
kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na
kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo
mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais
wa Zanzibar. Pili walishauri kwambakama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada
kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya
Katiba, Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao
na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na
mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo
Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia
Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni
zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina
zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu
mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa
kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati
mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani
yalisaidia kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na
upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache
ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao
wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na
Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye
Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni
yake.
Ndugu Zangu;
Baada
ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza
kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka
malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka
Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa
kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa
upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho
kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao
walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Pia
wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati
ya Bunge zima.
Wabunge
waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo
ya kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia
kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na
mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa
mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na
lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa
maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi
yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki
mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. Bahati mbaya
hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya
kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo
lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na
kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua
hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman
Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii.
Naamini na wao wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna
msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”. Naomba hekima ziwaongoze
viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia
utaratibu tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande
zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na
kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua
zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya
kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa
kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania
wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu.
Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya
kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine
iliyojificha?
Kama
dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na
Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya
ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na
kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa
kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya
taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda
pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani.
Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za
uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya
TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo
tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali
pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa
sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa
kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi
mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya
kutaka Rais asiteue waleWajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda
ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na
maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo
kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa
ngumu zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza,
kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi
za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.
Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili
kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa
nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu,
wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara,
wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa
vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa
wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa
tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na
kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya
dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa
kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT
hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada
ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine.
Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya
moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila
taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo
nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata
uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya
kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi mbalimbali
nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum.
Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama
kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani,
labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi
na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri
tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya
Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166?
Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli
wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu
linaloingia akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini
nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea
maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi
Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama
vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima
tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima
tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba
na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika
lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya
wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati
nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya
kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo
huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa
ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa
Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi
mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao
au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa
pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza
kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa
maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi napata tabu
kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa
msingi wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia
kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya
wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo
hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili
lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi
muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo
basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia
vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa
pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na
utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote (consensus)
na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za
pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi
kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo
hakuna uamuzi.
Hivyo
basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani
unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke
yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar.
Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo
ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini,
hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo
kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa
sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi
kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna
mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa.
Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna
kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa
ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa
sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa
Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge
Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya
Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu
na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si
haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge
Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo
uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza
kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba
nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi
kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana
na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama
iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata
safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila
maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua,
naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo
na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu.
Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
About Omari Makoo
Blogger Comment
Facebook Comment