JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
IDARA YA UHAMIAJI
Idara
ya Uhamiaji ni moja ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyenye jukumu la
kuhakikisha kwamba Ulinzi na Usalama wa nchi unaimarishwa. Katika
kusimamia jukumu hilo kikamilifu, Idara ya Uhamiaji inatekeleza majukumu
makuu ya Msingi yafuatayo:
i. Kuwezesha na kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu nchini
ii. Kutoa huduma ya pasipoti au hati nyingine za safari kwa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
iii. Kutoa huduma ya Vibali vya kuishi nchini pamoja na Pasi mbalimbali kwa wageni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.
iv. Kufanya misako, doria, kubaini na kuwakamata wahamiaji haramu nchini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
v. Kuratibu mchakato wa maombi ya wageni wanaoomba uraia wa Tanzania na kumshauri ipasavyo Mhe. Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi kwa hatua ya uamuzi.
Majukumu
hayo ndiyo yanaipatia Idara ya uhamiaji wajibu wa kulinda na kuimarisha
ulinzi na usalama wa nchi, sambamba na Vyombo vingine vya Ulinzi na
Usalama.
Uwezeshaji na Udhibiti wa wahamiaji nchini
Tanzania ni nchi inayofahamika sana
duniani kwa ukarimu wa watu wake, ardhi yenye rutuba, rasilimali
mbalimbali na vivutio vingi vya aina yake kwa watalii. Tanzania pia
kutokana na historia yake ya amani na utulivu pamoja na imani ya
viongozi wake kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja, Tanzania
imekuwa ni kimbilio salama la wakimbizi wengi na wapigania uhuru kutoka
mataifa mbalimbali Barani Africa.
Tanzania
pia inazidi kuwa kivutio kwa wageni wengi kutokana na kuwa na fursa
nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji,
madini, utalii n.k. Hata hivyo, si wageni wote wanaoingia nchini
wanafuata taratibu za kiuhamiaji katika kipindi chote cha kuwepo hapa
nchini. Hivyo, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa
na changamoto ya kuwepo wahamiaji haramu.
Wahamiaji haramu hao wanatokana na makundi makuu yafuatayo:
Wahamiaji haramu walioingia nchini kabla ya uhuru pamoja na vizazi vyao.
Wengi walikuja kama manamba katika
mashamba ya wakoloni. Ingawa wengi wao wamefariki, lakini vizazi vyao
bado vipo. Wahamiaji haramu wa aina hii wengi wanapatikana katika mikoa
mingi ya mpakani, Tanga, Pwani na Morogoro. Hawa kwa mujibu wa historia
yao ni miongoni mwa wahamiaji “walowezi” hapa nchini. Kazi kubwa
inayofanywa na Idara ya Uhamiaji ni kuwatambua, kuwaandikisha na baadae
kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu hatua za kuchukua.
Wahamiaji haramu wanaotokana na kuwepo kwa makambi ya wakimbizi na wapigania uhuru nchini.
Baada
ya nchi nyingi kupata uhuru, wapigania uhuru wengi waliondoka, lakini
baadhi vizazi vyao bado vipo hapa nchini na baadhi ya vizazi hivyo
vinaishi isivyo halali nchini.
Aidha,
wengine ni wale walioishi nchini kama wakimbizi na baadae kutorejea
nchini kwao pamoja na vizazi vyao. Wengi wa wahamiaji haramu hao wapo
katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mtwara Ruvuma, Morogoro.
Katika
kuwashughulikia Wahamiaji haramu wa aina hii, Idara imeweka utaratibu
wa kuwatambua kwa kuwaandikisha katika madaftari maalum ili kuwa na
kumbu kumbu zao sahihi na baadae kuishauri Serikali kuhusu hatua za
kuchukua. Madaftari haya yameisaidia Serikali kuwatambua Wahamiaji
haramu katika Mikoa ya Kagera na Kigoma wakati wa Operesheni “Kimbunga”
inayoendelea hadi sasa.
Wahamiaji wanaozidisha muda wa ruhusa ya kuwepo nchini.
Hawa ni Wahamiaji wanaoingia nchini
kihalali na kupewa muda maalum wa kuwepo nchini. Baadhi yao muda huo
unapokwisha hawaondoki, wanaendelea kuishi kwa kujificha na kuukimbia
mkono wa sheria. Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa
kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na
kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa nchini.
Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Hawa ni wale ambao wanaingia nchini bila
kufuata taratibu zozote za Uhamiaji. Wengi wao wanatumia njia
zisizohalali wakati wa kuingia nchini. Kundi hili linahusisha Wahamiaji
haramu wengi waliopo katika maeneo ya mipaka yetu na nchi jirani pamoja
na makundi ya Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kutoka nchi za Pembe ya
Afrika (Somalia na Ethiopia).
Wahamiaji
haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa kuwasaka, kuwakamata na
kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha
mahakamani na kuwaondoa nchini.
Udhibiti wa Wahamiaji haramu katika maeneo yaliyopo nje ya Mikoa ya “Operesheni Kimbunga”
Wakati wa utekelezaji wa agizo la Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la
kuwataka majambazi, majangili na wamiliki wa silaha kinyume cha sheria
kujisalimsha na Wahamiaji haramu walipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma
na Geita kurudi nchini kwao kwa hiari, Idara ya Uhamiaji iliendelea na
shughuli za udhibiti wa wageni katika kipindi hicho kwenye Mikoa iliyopo
nje ya eneo la operesheni. Katika shughuli hizo za udhibiti wa wageni,
Jumla ya wahamiaji haramu 6,653 kutoka
mataifa mbalimbali wamekamatwa na kuchukuliwa hatua mbali kwa mujibu wa
sheria. Mataifa ya Wahamiaji hao haramu na idadi yao kwenye mabano ni
kama ifuatavyo:- Malawi (3,778), Burundi (696), Congo DRC (1,739), Kenya
(147), Uganda (20), Pakistan (12), Somalia (31), Nigeria (23) na
Msumbiji (20). Wengine ni India (16), China (09), Rwanda (40), Ethiopia
(97), Komoro (10), Uturuki (03), Afrika Kusini (02), Bukina Faso (01),
Liberia (02), Italia (01), Singapore (01), Libya (01), Bulgaria (01),
Ghana (02) na Syria (01).
Wengi
wa Wahamiaji haramu hao wameondolewa nchini, wengine wamefikishwa
mahakamani wakati wengine uchunguzi dhidi yao bado unaendelea. Aidha,
wapo walio halalisha ukaazi wao nchini wakati wengine wameorodheshwa kwa
ajili ya hatua zaidi.
Watanzania Wahamiaji haramu katika nchi nyingine.
Wakati Tanzania ikiendelea na udhibiti
wa Wahamiaji haramu nchini, takwimu zilizopo zonaonesha kwamba wapo
watanzania ambao nao wanakiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi
mbalimbali wanazokwenda, ikiwemo kuingia na kuishi katika nchi hizo
wakiwa Wahamiaji haramu.
Katika
kipindi cha mwaka 2012, Jumla ya watanzania 1,263 walirejeshwa nchini
kutoka mataifa mbalimbali. Aidha, katika kipindi cha Januari-August,
2013 jumla ya watanzania 715 wamerejeshwa nchini kwa makosa ya kukiuka
taratibu za Uhamiaji katika nchi walizokwenda, hususan Afrika Kusini.
Kwa
kuwa sasa tunaishi katika ulimwengu ambao watu wanasafiri kutoka nchi
moja hadi nyingine kuliko kipindi chochote kile katika historia ya
binadamu, tunapenda watanzania nao wasafiri nje ya nchi kwa ajili ya
kunufaika na fursa mbalimbali na tumekuwa tukiwawezesha kufanya hivyo.
Pamoja na nia hiyo njema ya Serikali, tunatoa wito kwa watanzania
wenzetu kuheshimu Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika nchi wanazo
kwenda, kama ambavyo tunapenda wageni nao waheshimu Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo hapa nchini. Kufanya hivyo sio tu kwamba kutatujengea
uaminifu na uadhilifu katika jamii ya watu tunaoishi nao ugenini, bali
pia kutajenga jina zuri na heshma kwa nchi yetu miongoni mwa mataifa
mengine.
Sote
tufahamu kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuvumilia Wahamiaji
haramu, bila kujali wanatoka taifa gani. Kila nchi inajitahidi
kukabiliana na changamoto hii ya Wahamiaji haramu. Tofauti ni mbinu
zinazotumika kulingana na mazingira na uwezo wa nchi husika. Ndio maana
kwa mazingira ya jiografia ya nchi yetu, mapambano dhidi ya Wahamiaji
haramu ni endelevu bila kujali kama kuna operesheni maalum au ni katika
hali ya utendaji kazi wa kawaida.
Hitimisho:
Suala
la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni la kila mwananchi. Vyombo vya
Ulinzi na Usalama peke yake haviwezi kutekeleza jukumu hili bila
ushirikiano wa karibu na wananchi. Wahamiaji haramu hawana kisiwa chao
wenyewe, bali wanaishi ndani ya jamii. Tunawashukuru wote waliotupatia
ushirikiano katika kutekeleza majukumu yetu na tunaomba tuendelee
kushirikiana kuanzia mwananchi mmoja mmoja, viongozi wa ngazi
mbalimbali, wanahabari pamoja na vikundi mbalimbali vya kijamii.
Blogger Comment
Facebook Comment