-->

UPASUAJI WA WATOTO MAPACHA WALIUNGANA WAKAMILIKA KWA USALAMA MUHIMBILI




WATOTO WALIOUNGANA
Madaktari wakiendelea na upasuaji wa watoto walioungana  katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha watoto.
 
UPASUAJI wa kuwaokoa pacha pengine unadhaniwa kuwa ni jambo linalowezekana nchi za nje pekee. Lakini hata hapa nchini, inawezekana. 

Agosti 30, 2013 ulifanyika upasuaji wa kihistoria kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo mtoto aliyezaliwa ameungana na mwenzake kwa sehemu ya chini ya uti wa mgongo alitenganishwa na mwenzake ambaye hata hivyo hakuwa amekamilika viungo vyake.  
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Watoto, MNH Dk Zaitun Bokhary anaeleza mengi kuhusu tukio hilo na masuala mengine yanayohusu umahiri wa MNH katika kukabiliana na aina hiyo ya tatizo katika jamii pamoja na pia kutoa ushauri.
Anasema tukio hilo  limeandika historia nyingine kwenye  tasnia ya kitabibu nchini na kuonyesha kuwa Watanzania wanaweza.
Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wakishirikiana na wenzao ( MNH) walifanikisha upasuaji huo wa mtoto aliyezaliwa akiwa ameungana na mwenzake sehemu ya chini ya uti wa mgongo.
Licha ya kuwa na uhai, kiwiliwili cha mtoto huyo mwingine  hakikuwa na viungo muhimu kama kichwa na macho.  Pia, hakikuwa pia na moyo, figo, tumbo na maini, ila kilikuwa na uti wa mgongo.
Mtoto  huyo ambaye amepewa jina la Kudra alifikishwa MNH akitokea Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alikozaliwa na  mama yake, Pili Hija (24), Agosti 18, 2013.
Kwa kuona uwezo wao, madaktari wa Mnazi Mmoja waliamua kumhamishia MNH mtoto na mama yake kwa  upasuaji mkubwa zaidi ili kumwokoa.
Ushuhuda wa Dk Bokhary 
Upasuaji kama huo wa kutenganisha  watoto pacha walioungana si wa kwanza kufanyika katika hospitali hiyo na hapa nchini.
Anasema mwaka 1994, Profesa Joseph Shija, gwiji wa kwanza Mtanzania mtaalamu wa upasuaji wa watoto aliwahi kufanya upasuaji kama huo.  

Hata hivyo, tofauti na Kudra, watoto wale waliofanyiwa upasuaji na Prof Shija walikuwa wamekamilika, waliungana tumboni (omphalopagus), kila mmoja akiwa mtu kamili.  Mmoja wao alipona, mwingine  alikufa.
Upasuaji mwingine wa kutenganisha  pacha ni ule uliofanywa na bingwa  mwingine, Dk Petronila Ngiloi mwaka 2009 kwa pacha waliokuwa wameungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo (ischiopagus). MWANANCHI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment