POLISI Kaunti ya Kericho, Jumatatu
walikumbana na kazi ngumu ya kutegua kitendawili kuhusu mzazi halisi wa
mtoto msichana mwenye umri wa miezi minne anayepiganiwa na wanawake
wawili.
Kila mmoja wa
wanawake hao anadai kwamba ndiye mzazi halisi wa mtoto huyo na polisi wameamua kufanya uchunguzi wa chembechembe za jenetiki (DNA), ili
kubaini ukweli.
Kabla ya
matokeo ya uchunguzi huo, itabidi mtoto huyo abaki na majina mawili -
Cynthia Achieng, anavyodai Bi Mercy Amenya, mkazi wa Eldoret, au Naomi
Chepkoech kama anavyodai Bi Joyce Chepkemoi.
Hapo Jumatatu
wanawake hao walirushiana maneno makali katika kituo cha polisi cha
Kericho kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kudaganya ndiye mama wa mtoto
huyo.
Bi Amenya
anadai kwamba Joyce aliiba mtoto huyo, madai ambayo Joyce amekanusha
vikali. Bi Amenya anadai alimuajiri Joyce kuwa yaya nyumbani kwake kabla
ya kumwibia mtoto.
Lakini Joyce anadai Bi Amenya anataka kumnyang’anya mtoto.
Bi Amenya
anadai kwamba alijifungua mtoto huyo mnamo Juni 14 mwaka huu katika
hospitali ya wilaya ya Narok, ilhali Joyce anadai alijifungua Mei 14,
katika hospitali ya wilaya ya Siongiroi, Kaunti ya Bomet.
Bi Amenya aliambia Taifa Leo
kwamba alimuajiri Joyce ingawa hakuwa na stakabadhi za kujitambulisha
na hakufichua alikozaliwa akidai alitoka Chebunyo, Kaunti ya Bomet na
wakati mwingine kudai alizaliwa Nandi.
“Nilimchukua
msichana huyo nilipompata Narok akionekana mdhaifu na nikamhurumia.
Baadaye nilimwajiri yaya nyumbani kwangu na sikujua anaweza kuiba mtoto
wangu,” akasema akitokwa na machozi.
Bi Amenya
anadai kuwa siku ambayo mtoto aliibwa alimuacha na Joyce akaenda kazini
Kericho na aliporudi nyumbani kupeleka nguo alizonunua akapata ametoweka
na mtoto.
“Nilipata
nyumba imevurugwa. Kifungua mimba wangu Kibet aliniambia yaya aliondoka
na mtoto na kubeba nguo. Niliwauliza majirani na wakaniambia walimuona
akitoka na akawaambia atarudi,” akasema.
Kukagua nyumba
Bi Amenya
alisema alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Baharini na akaagizwa
akague nyumba kujua kama kuna mali nyingine iliyoibwa na akagundua
vyeti vya matibabu vya mtoto na Sh1,000 zilikuwa zimetoweka.
“Baadaye
Joyce alimpigia simu mumewe na kumtaka amtumie pesa ili arudishe mtoto.
Polisi walifuata mawasiliano ya simu hiyo na kumkamata na ninashangaa
akisema mtoto ni wake,” akasema.
Lakini Joyce
alikanusha alikuwa yaya wa Bi Amenya akisema hakumuona mtoto mwingine
kwake alipokuwa mgeni wake. Anakiri kwamba alikutana na Bi Amenya eneo
la Chebown, Kericho, alipokuwa hana mbele wala nyuma baada ya kujifungua
mtoto msichana.
Aliambia Taifa Leo
kwamba hana vyeti vya kuzaliwa vya mtoto huyo. “Chepkoech ni mtoto
wangu na ana umri wa miezi minne. Nilipokuwa katika nyumba ya Mercy
hakuwa na mtoto isipokuwa mvulana aliyeitwa Kibet,” akasema.
Kamanda wa
polisi wa Kericho, Bi Rose Muchuma, alisema kesi ya utekaji nyara mtoto
iliripotiwa Eldoret na mshukiwa akakamatwa eneo la Chebown, Kaunti ya
Kericho, baada ya polisi kufuatilia mawasiliano ya simu.
CHANZO:SWAHILIHUB
Blogger Comment
Facebook Comment