TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO
kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni
umemalizika Ikulu, Dar Es Salaam, muda mfupi uliopita leo, Jumanne,
Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo mbili kukubaliana kama ifuatavyo:
Moja ,
kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo
ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili ifatutwe namna ya
kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.
Pili,
kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa
Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano
na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo
kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa. Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Viongozi wa
vyama vyama vya siasa waliokutana na Mheshimiwa Rais Kikwete ni
Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na Mheshimiwa James Mbatia ambaye
ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wengine ni
Makamu Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Philip Mangula, Mheshimiwa Isaack
Cheyo ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha UDP Mheshimiwa John
Cheyo na Mheshimiwa Nancy Mrikaria ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa
TLP Mheshimiwa Augustine Mrema. Waheshimiwa John Cheyo na Mrema wako nje
ya nchi.
Wengine
ambao wameambatana na wenyeviti wao ni Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana
Julius Mtatiro wa CUF, Waheshimiwa Tundu Lissu na John Mnyika wa CHADEMA
na Bwana Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Blogger Comment
Facebook Comment