Igunga. Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe amesema sababu ya kutaja mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.
Zitto alitoa kauli hiyo jana mjini Igunga, wakati
akitangaza mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa
mujibu wa Zitto, kwa mwaka kiongozi huyo wa nchi analipwa Sh384 milioni
ambazo ni wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi.
Hatua ya Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), kutaja mshahara
wa rais inakuja wiki moja baada ya kutaja mshahara wa Waziri mkuu kuwa
ni Sh26 milioni kwa mwezi pasipo kukatwa kodi
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi
wanancholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi bali ni usiri
unaofanywa juu ya kiwango hicho. Alisemaha ni jambo la kusikitisha kuona
mwalimu anayelipwa mshahara wa Sh200,000 kwa mwezi ukikatwa kodi huku
viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo
kukatwa kodi.
Alisema katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza
kuwa rais atalipwa mshahara na malipo mengine huku ibara hiyo hiyo
kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupu rupu kupunguzwa, hali
aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa
manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk Slaa akiwa Rais na
akataka kupunguza mshahara wake kwa katiba hii hawezi na hili jambo si
sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka
Serikalini,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa kitendo cha Serikali kuyafungia
magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, hakikuzingatiwa kulingana na uwazi
uliowekwa kwa kuandika uwazi wa viwango vya mishahara.
Alisema kuwa waziri aliyehusika kufunguia magazeti
hayo hakufikiria kwa makini kutokana na kuwa na uelewa mdogo na
kuongeza kuwa hakuna kosa lolote linalopelekea kufungiwa magazeti hayo
kutokana na ukweli ulioandikwa.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
Blogger Comment
Facebook Comment