-->

KAULI INAYOTIKISA VICHWA:MAJANGILI WAUAWE

KAULI aliyotoa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kwamba majangili wauawe, inaweza kumgharimu na kupata malalamiko kama aliyopata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pale aliposema wauaji wa albino nao wauawe.
Waziri Kagasheki alisema hayo hivi karibuni jijini Arusha, baada ya kuongoza matembezi ya kupiga vita ujangili wa tembo yaliyoandaliwa na Taasisi ya David Sheldrick Wildlife Trust kupitia kampeni ya meno ya tembo.
Kagasheki alisema: “Wana usalama wakikutana na majangili huko porini wawamalize huko huko, tena katika jambo hili nawaomba wale watetezi wa haki za binadamu wafunge midomo.
“Hata hao majangili wakiwakuta watawamaliza pamoja na tembo,” alisema Kagasheki huku umati wa watu uliokusanyika ukipiga makofi.
Alisema kuwa kazi ya serikali ni kuwatetea wale wasio na uwezo wa kujitetea wenyewe kama wanyama wa porini, akiwamo tembo, na kwa kuwa kumekuwa na tatizo la kesi kuchukua muda mrefu, suluhisho ni vyombo vya ulinzi kumalizana na majangili huko huko pindi wakiwakamata.
Ingawa kauli ya Kagasgeki ina nia nzuri ya kuwatia hofu majangili wasiue tembo, lakini ninaiona ni sawa na ile iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu, Pinda, ya kutaka wauaji wa albino nao wauawe, inaweza kuwa mwiba kwa Kagasheki katika uongozi wake kama ilivyotokea kwa Waziri Mkuu, Pinda, ambapo alijikuta akimwaga machozi huku akilazimika kuomba msamaha. Lakini kama anavyofahamika Waziri Mkuu, Pinda, kwa kauli zake zilizo na utata kwani katika kikao cha Bunge alijikuta akijikwaa tena aliposema; “Watu wasiotii amri ya polisi bila shuruti, piga tu, kwa kuwa tumechoka!”
Ingawa Kagasheki ametanguliza silaha ya kuwaomba watetezi wa haki za binadamu wafunge midomo dhidi ya kauli yake juu ya majangili ombi hilo linaweza lisimsaidie na akaweza kujikuta akikumbana na tatizo.
Hata hivyo siku chache baada ya kauli hiyo Wananchi wa mkoa wa Morogoro waliohojiwa wamepinga kauli ya serikali iliyotolewa na Kagasheki.
Mmoja wa wachangiaji alisema, kauli hiyo itasababisha hata wakulima wengi wanaokwenda mashambani wakiwa na panga, wakaweza kudhaniwa kuwa ni majangili, hivyo kuuawa na kupoteza maisha. Hata hivyo inafahamika kuwa wanaochangia na kufadhili ujangili ni hao hao vigogo wa serikali, Hivyo Kagasheki alipaswa kuanza na hao na kuacha kukimbilia walalahoi? Kauli hiyo inaashiria kuwa kiongozi huyo ameshindwa kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na matendo hayo na badala yake amekuja na hoja nyepesi.
Ni rai yangu serikali itafute njia mbadala ya kuhakikisha watu wanaohisiwa kufadhili utoroshaji na ujangili wa tembo na rasilimali za nchi hii, basi wasiwe ndio wale ambao wanasimama majukwani na kuwakataza Watanzania kile ambacho wao wanafanya.
Utamaduni wa usafi na uadilifu ukianzia nyumbani, kwenye familia, majukwani, maofisini, na popote pale, ni dhahiri watu watajifunza kutofanya makosa na matokeo yake watakuwa waadilifu kama viongozi walivyo kwenye nafasi zao!
Makala hii imeandikwa na Bryceson Mathias
Source:Dullonet Tanzania
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment