WANANCHI
wa Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kwenda katika hospitali za Serikali
wanapohisi dalili za ugonjwa wa denge, kwa kuwa matibabu hutolewa bure
wakati Serikali ikijiandaa kusambaza vifaa vya kupimia ugonjwa katika
wilaya zote nchini.
Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal akifungua Kongamano la Pili la Kisayansi
lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
(Muhas), alisema Serikali haina mzaha katika kukabiliana na mlipuko wa
ugonjwa wa denge.
Alisema
Serikali imeamua kusambaza vipimo hivyo, baada ya kuonekana kuwa ni
tishio kwa maisha ya binadamu hivyo serikali imejipanga kuhakikisha
ugonjwa huo unatokomezwa.
“Kutokana
na ukubwa wa tatizo hili, tayari Serikali imejipanga kipambana na
ugonjwa huu, ndio maana sasa tumeandaa mkakati wa kusambaza vifaa vya
vipimo vya ugonjwa huu kwa kupitia wilaya zote nchini,” alisema Dk
Bilal.
Akizungumzia
masuala ya utafiti nchini, Bilal alisema wanaweka mikakati kuongeza
rasilimali watu hasa vijana katika masuala ya utafiti ikiwemo katika
masuala ya afya, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi tafiti hizo.
Muhas
Awali
Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya, alisema chuo hicho kimeandaa
kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu ugonjwa huo,
ambacho kitashirikiana na watafiti wengine.
Profesa
Kaaya alisema lengo la kongamano hilo ni kutafakari na kuangalia malengo
waliyojiweka chuoni hapo hasa katika masuala ya utafiti kama
yamefanikiwa katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu na nini
kifanyike katika kukamilisha yale yalisalia.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Profesa John Mkoma,
alisema kwa sasa Mamlaka yake kupitia Muhas na Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, wameanza kutumia simu za mkononi kwa ajili ya kufikisha
taarifa mbalimbali kwa wananchi kwa njia ya ujumbe mfupi.
Alisema
lengo la kutumia simu za mkononi, ni kutoa taarifa kwa haraka kwa
wananchi juu ya masuala mbalimbali ya afya yanayotokea, ikiwemo magonjwa
ya milipuko kwa nia ya kupunguza maambukizi kwa haraka.
Dar es Salaam
Naye Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema matibabu ya denge
yanatolewa bure na kuwataka wananchi wakijisikia dalili, kwenda katika
hospitali za Serikali.
“Tunaomba
wananchi wanapohisi dalili za ugonjwa huo kwenda katika hospitali za
Serikali, ambazo ni Amana, Mwananyamala na Temeke kwa kuwa matibabu
yanatolewa bila malipo,” alisema Sadiki alipokuwa akizungumzia gharama
za matibabu ya homa hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwa sasa wanajenga uwezo ili kila wilaya iwe na vituo vitano kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa huo.
Dawa
Sadick
aliongeza kuwa Serikali itanyunyuzia dawa ya (Lavacide) sehemu za
mikusanyiko kama vile mashuleni na kwenye madimbwi, lakini maeneo ya
hotelini na mabaa watapaswa kunyunyuzia dawa kwa gharama zao.
“Kwa
upande wa wizara, idara na taasisi za Serikali wanapaswa kunyunyuzia
dawa kwa gharama zao, (yaani matumizi mengineyo),” alisisitiza huku
akisema hata kwenye ofisi yake wamefanya hivyo kwa gharama zao.
Sadiki
aliwataka viongozi wa mitaa na watendaji wengine kuwahimiza wananchi
kuhusu usafi wa mazingira ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema
wananchi wanapaswa kuhakikisha vifuu vya nazi na visoda kwani maji
kidogo yanayokaa katika vitu husababisha mbu wanaosababisha ugonjwa huo
kuzaliana. Alisisitiza hatua ya kwanza kuzuia ugonjwa huo ni usafi wa
mazingira na dawa ni hatua ya mwisho.
Ushauri
Katika
hatua nyingine, Serikali imeshauriwa kuwapa semina waganga wa tiba
mbadala kuhusu hali halisi ya ugonjwa huo, ili kuepuka kuibuka kwa
wataalamu watakaodai wanatibu na kuwafanyia majaribio wagonjwa.
Ushauri
huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mandai Herbal Clinic,
Dk Abdallah Mandai, wakati akizungumzia ugonjwa wa denge na kuongeza
kuwa umekuwa ni tatizo la kitaifa linalohitaji hatua stahiki za
kukabiliana nalo.
*Dalili
Hivi
karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles
Pallangyo, alisema dalili za ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya
viungo na uchovu na dalili hizo huanza kujitokeza kuanzia siku 3 hadi 14
tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge.
“Kwa
wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na dalili za
malaria, hivyo basi tunawaomba wananchi wakipata homa kuhakikisha
wanapima kama wana malaria au la, ili hatua stahiki zichukuliwe,”
alisema Pallangyo.
Aidha
aliongeza kuwa kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo katika namna
unavyojitokeza, iwapo mtu aking’atwa na mbu mwenye virusi hivyo.
Aina ya
kwanza ndio homa ya denge yenyewe, ambayo huambatana na dalili kuu tatu
za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.
Kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza
wakiwa na dalili hizo.
Aina ya
pili ni denge ya damu, ambayo huambatana na dalili za magonjwa kutokwa
na damu kwenye fizi au puani na kutokwa na damu chini ya ngozi. Iwapo
mgonjwa huyo ataumia sehemu yoyote, ni rahisi kupoteza damu nyingi
kupitia kwenye michubuko.
Aina ya
tatu ni denge ya kupoteza fahamu, ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza
damu nyingi ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu.
Mpaka sasa dalili hizo zimeonekana kwa mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa 400 waliokwishwathibitika kuwa na ugonjwa hapa nchini.
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwako, Lucy Lyatuu(HABARILEO) na Magreth Kinabo (MAELEZO).(FS)
0 comments :
Post a Comment