Dar es Salaam. Daktari
wa Hospitali ya Mwananyamala, Saleh Kijangwa amejitokeza na kueleza
jinsi alivyougua homa ya dengue ambayo imeukumba Mkoa wa Dar es Salaam.
“Niliumwa
sana, nikadhani ni malaria na nikahisi imekuwa kali kiasi hicho kwa
sababu sikuwahi kuugua malaria maishani mwangu. Nilipima magonjwa mengi
lakini hakuna kilichoonekana,” alisema.
Dalili alizoona
Dk
Kijangwa alisema alianza kuhisi maumivu makali ya kichwa usiku wa Ijumaa
Kuu yaliyoambatana na maumivu ya misuli na viungo vya mwili na joto la
mwili kuwa kali isivyo kawaida.
“Niliumwa
sana kichwa, misuli, mgongo, kiuno na shingo. Maumivu yalikuwa makali
kiasi nilishindwa kupata usingizi, wakati huo joto lilikuwa kali sana.”
Daktari
huyo alisema kosa alilofanya ni kuamua kujitibu kwa kunywa dawa ya
maumivu aina ya diclofenac ambayo kwa kawaida haipatani na maradhi hayo.
“Diclofenac
ina tabia ya kuingiliana na utendaji kazi wa chembe hai hizo, hivyo mtu
mwenye dengue akizinywa huathirika zaidi. Kujitibu ni kosa
tunalolifanya mara nyingi. Ndiyo maana tunatakiwa tupime kwanza kabla ya
kumeza dawa ya aina yoyote,” alisema.
Dk
Kijangwa alisema alibainika kuwa na homa hiyo siku tano baada ya kuanza
kuona dalili na kwa kuwa dengue haina tiba, alitibiwa kwa paracetamol na
kutakiwa kunywa maji kwa wingi.
Kilichosababisha maambukizi
Dk
Kijangwa alisema anahisi kilichosababisha yeye pamoja na wakazi wengi wa
Wilaya ya Kinondoni kupatwa na ugonjwa huo ni uwepo wa bwawa la maji
maeneo ya Kambangwa ambalo huenda ndicho chanzo cha mazalia ya mbu
anayeambukiza maradhi hayo, Aedes Egyptiae.
Mpapai wadaiwa kutibu dengue
Baadhi ya
ripoti zimeonyesha kuwa majani ya mpapai yana uwezo wa kutibu homa ya
dengue. Ingawa haijathibitishwa lakini historia inaonyesha kuwa majani
ya mpapai yanatibu ugonjwa huo baada ya kulipuka mara kwa mara nchini
India.
Majani ya mpapai hayana madhara na wala si sumu pale yanaponywewa na yamekuwa pia yakitumiwa kwa chakula nchini.
Tafiti
zilizowahi kuchapishwa na Jarida la Archieve la India limeeleza kuwa
juisi ya majani ya mpapai ilisaidia wagonjwa watano waliopata homa ya
dengue kuongeza chembechembe zinazohusika na kuganda kwa damu ndani ya
saa 24.
Tafiti
nyingine zilizofanywa na madaktari na watafiti kutoka Marekani na Japan
na kuchapishwa katika Jarida la Ethnopharmacology zilieleza kuwa juisi
ya majani hayo ilionyesha kuwasaidia wagonjwa wa homa ya dengue na
ilionyesha kuwa na uwezo wa kutibu malaria na saratani.
Daktari
kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Vinitah Saini alisema baadhi
ya maeneo wanatumia juisi ya majani ya mpapai kutibu ugonjwa huo lakini
akasema hakuna ushahidi wa kisayansi kuwa yanatibu. (CHANZO: MWANANCHI)(FS)
0 comments :
Post a Comment