TAARIFA KWA UMMA
TAARIFA YA BAADHI YA WAJUMBE WA BARAZA KUU NA MKUTANO MKUU CHADEMA MIKOA YA DSM, PWANI NA TANGA KUPINGA UHUNI WA KISIASA UNAOITWA UKAWA.
UTANGULIZI.
Ndugu
wanaHabari, Tunapenda mtusaidie kufikisha ujumbe wetu huu kwa umma
unaotokana na malalamiko na manung’uniko ya wanachama wenzetu wa CHADEMA
kuhusu udhaifu mkubwa wa kiuongozi unaoendelea kwa sasa chini ya
mwavuli wa UKAWA.Kwa wiki kadhaa sasa, kumeibuka msamiati mpya wa
kisiasa wa UKAWA uliopelekea mpaka kuundwa kwa BARAZA KIVULI LA UKAWA
pale Bungeni bila kufuata Utaratibu.
Sisi
viongozi ambao miongoni mwetu ni Wajumbe wa vikao halali vya chama,
ambavyo ni Baraza Kuu na Mkutano mkuu wa chama kutoka mikoa ya Tanga,
Pwani na DSM kwa masikitiko makubwa tunasema kuwa hatupendezeshwi na
mwenendo huu wa chama unaofanywa na viongozi wetu wakuu.
KUSUSIA BUNGE LA KATIBA.
Ndugu wanaHabari,
Kwa
namna ambavyo tumepambana kwa miaka mingi kudai na kuishinikiza
serikali kuridhia uandikaji wa katiba mpya, ni mpumbavu pekee anayeweza
kususia fursa ya uandishi huo tena kupitia chombo huru (BUNGE LA KATIBA)
kwa sababu tu ya mgongano wa kimaslahi.
Tunasikitika
sana kuwaona viongozi wetu na wabunge wa chama chetu cha CHADEMA
wamesahau kazi tuliyowatuma ya kwenda kuandika katiba mpya yenye
kuzingatia maslahi ya wananchi badala yake wamekwenda kupigania vyeo.
Tumefedheheshwa
sana na namna ambavyo wawakilishi hawa wamekubali kutanguliza mbele
maslahi yao na kuyaacha maslahi ya wananchi ambao ndio waliuowatuma,
kwenye Rasimu yenye sura zaidi ya 18 ni uzezeta kususia sura 2 tu za
mwanzo kisa tu maslahi yao ya kugawana vyeo wanaona hayawezi
kutekelezeka.
Tunaomba
ifahamike kwamba, hakujawahi kukaliwa kikao chochote halali cha chama
chetu kilichoazimia na kuwaagiza wajumbe wanaotokana na chama chetu
wasimamie katiba yenye SERIKALI TATU, na ikionekana haiwezekaniki WASUSE
NA KUTOKA NJE YA BUNGE.
Huu
ni udhaifu unaotawaliwa na uroho wa madaraka, sisi kama viongozi halali
wa kikatiba wa chama hatujawahi kuwaza wala kuamua kuhusu ujinga huu,
siku zote tumekuwa tukiwasisitiza wajumbe wetu kwenye fursa yoyote
watakayoipata kwenda kusimamia mawazo na misimamo ya wananchi ambao ni
wanyonge.
Tunawatuma
wajumbe wetu kuhakikisha tunapata katiba itakayosimamia na kuzitunza
Rasilimali zetu, na wala si kweli kuwa Idadi ya Serikali kama ni 3 au 2
au 5 au zozote inaweza kuwa muarobaini wa changamoto zetu.
Daima
dumu tumekuwa tukiamini kwenye mapambano ya Hoja ambayo ndio msingi
mkuu wa demokrasia ya kweli Tunayoisimamia kama CHADEMA.
Hivyo
Basi tunasema, si sahihi hata kidogo kwa wajumbe wetu wa Bunge la
katiba kususia vikao vile na ndio maana hata baadi ya wabunge wengi wa
chama chetu wamekuwa wakilalamika chini chini kwetu sisi wajumbe wa
baraza kuu kwamba wamechoka sasa kuburuzwa na viongozi wakuu wa chama na
kwamba wao nao wana mawazo na misimamo yao, sasa kwa niaba yao pia
tumeona kama viongozi wa chama ulikemehe hili.
Nipo
tayari kuyataja majina ya wabunge hawa wanaolalamika kuburuzwa ambao ni
zaidi ya wabunge 31 wa kuchaguliwa na wa viti maalum.
Muungano
wetu huu wa UKAWA ni muungano wa kinafiki usiokuwa hata na hadidu za
rejea, hakunaga muungano duniani kote ambao waunganaji wake wanaungana
kiujanja ujanja tu kama walivyofanya viongozi wetu hawa. Hatuungi mkono
na tunawataka wasiendelee na upuuzi wao huu, warudi bungeni kama
hawataki wajitoe tuchague wabunge wengine watakaowawakilisha wananchi
wanaotuamini.
Ni
sawa na ndoa ya mkeka, hakuna maridhiano, hakuna vikao, asubuhi wapenzi
jioni wana ndoa, ndoa ya namna hii kamwe haiwezi ikadumu hata kidogo.
BARAZA KIVULI LA UKAWA.
Tunasikitika
sana na kitendo cha mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe,
kutufanya sisi wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu hatuna maana kwenye
kufanya maamuzi ya chama.
Walituaminisha
kwamba CUF wamefunga ndoa na CCM na kwamba wao ni sehemu ya serikali
hivyo hawawezi kushirikiana na chama ambacho ni sehemu ya serikali, kwa
msingi huu tukaazimia kwenye vikao vya chama ambavyo ni halali kwamba
chama chetu hakitashirikiana na chama kingine chochote cha siasa kwa
kuwa ni washirika wa CCM na kwamba wao ni CCM-B
Tumemkashigu
na kumtuhumu James Mbatia na NCCR nzima kuwa ni Tawi la CCM na ndio
maana hata Mbatia ameteuliwa kuwa Mbunge, inakuwaje leo tunashirikiana
na watu hawa ambao wanatumiwa na CCM?
Ni lini Muungano wa CCM na CUF umevunjika rasmi? Ni lini ushirikiano wa NCCR ya MBATIA na CCM umekufa rasmi?
Je
mazingira yaliyofanya tuwahesabu wenzetu hawa kuwa ni CCM B leo
yamebadilika?, na kama yamebadirika yamebadilika lini na yamebadilikaje?
Je sio kweli kwamba tuliwatenga wenzetu na kuwakashifu kwa sababu tu ya uchu wa madaraka?
Yaani
sio kweli kwamba tuliwafedhehesha wenzetu hawa kwa sababu ya UWAZIRI
KIVULI? Na leo tunawasafisha wenzetu hawa kwa UWAZIRI KIVULI HUO HUO.
Kwa nini viongozi wetu wanakuwa na UCHU na UROHO wa MADARAKA kiasi hiki?.
Kama
tunaweza tukawaita wenzetu MASHETANI asubuhi na jioni tukawaita MALAIKA
kwa sababu ya UWAZIRI KIVULI, je tukipewa nchi na kushika dola, si
Tutawaita wenzetu majina mabaya zaidi?
Si tutakuwa na serikali mbovu na ya ajabu zaidi ya hivi sasa tulivyo kwenye siasa za upinzani tu tulio nao?
Kwa
misingi huu, Tunaamini kuwa UKAWA ni UNAFIKI WA KISIASA, na umebuniwa
kwa sababu moja tu nayo ni kugawana vyeo, hakuna sababu yoyote yenye
mantiki iliyopo kwenye uundwaji wa UMOJA huu na ndio maana hauna hadidu
za rejea wala hauna hati za makubaliano miongoni mwetu.
Napenda
kuwaambia watanzania kuwa sisi baadhi yab wajumbe wa Baraza kuu na
mkutano mkuu wa mikoa ya Pwani, Dsm na Tanga hatuungi mkono upuuzi
wowote wenye lengo la kusimamia ugawanaji wa vyeo na madaraka, watu wa
namna hii tunawaita WALAFI wa MADARAKA.
Tunaunga mkono watanzania wote wanaoitakia heri Tanzania yetu.
Mungu ibariki Tanzania
Imeandaliwa na Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Mikao ya Pwani, Dar es Salaam na TANGA na imesomwa nami
……………………………………………………
JOSEPH YONA PATRICK
+255713802226
Mwenyekiti wa CHADEMA WILAYA YA TEMEKE
Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa TEMEKE
MJUMBE WA BARAZA KUU CHADEMA TAIFA
MJUMBE WA MKUTANO MKUU CHADEMA TAIFA
MJUMBE WA KAMATI YA UTENZAJI BAVICHA TAIFA
0 comments :
Post a Comment