Dodoma. Wizara ya Fedha imepigilia msumari
maombi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kutaka waongezewe posho
na kusema anayeona ameacha kazi inayomlipa zaidi kwenda bungeni
afungashe virago na kuondoka.
Msimamo huo umekuja siku moja tu baada ya gazeti
hili kudokeza kuwa madai ya wajumbe wa bunge hilo kutaka waongezewe
posho kutoka Sh300,000 za sasa kwa siku, yamegonga mwamba baada ya
kamati iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wake kusema kiwango hicho
kinatosha.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Kificho
alisema jana bila kutaja viwango, kuwa ripoti ya kamati hiyo
imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi.
Madai ya wajumbe kutaka waongezewe posho,
yamechafua hali ya hewa ndani na nje ya Bunge, huku baadhi ya wananchi
wakipaza sauti zao na kumsihi Rais Kikwete alivunje bunge hilo iwapo
wajumbe watashikilia msimamo wa kutaka nyongeza ya posho.
Jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema wanaoshiriki kutunga Katiba ni Watanzania na siyo wataalamu
washauri waliokodiwa kutoka nje.
Alisema kwa msingi huo, Serikali ilitarajia kuwaona watu hao wakitanguliza uzalendo zaidi badala ya kudai malipo manono.
“Katika kutengeneza Katiba hii, hatujakodi
consultants (wataalamu washauri) kutoka Uingereza, Marekani, Kenya,
Uganda wala nchi nyingine yoyote… Hawa ni Watanzania na kazi
wanayoifanya ni yao,” alisema.
“Wangekuwa wataalamu wa kukodi wangeweza kudai
malipo hayo, lakini hapa ni tofauti... wanafanya kazi yao na kila mtu
anafanya kazi yake na anapaswa kujivunia kushiriki katika tendo hili la
kihistoria kwa kutanguliza uzalendo,” alisema.
Nchemba alisema anazielewa hoja za baadhi ya
wajumbe walioibua suala la posho, lakini kwa mtazamo wake, hoja hiyo
hata kama ingekuwa na mashiko kiasi gani, imewasilishwa wakati usiokuwa
mwafaka. Alisema wapo makandarasi na wazabuni waliotoa huduma kwenye
taasisi mbalimbali za umma lakini hawajalipwa.
Alisema kwa kawaida, Februari ni mwezi mbaya kwa
kuwa baadhi ya wilaya zina historia ya kukumbwa na uhaba wa chakula
hivyo kuhitaji fedha nyingi za Serikali ili kuokoa maisha ya watu katika
maeneo hayo.
Pia alisema si wakati mwafaka wa kudai nyongeza
hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna walimu wapya 30,000 nchini kote ambao
hawajapangiwa vituo kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa stahiki
zao.
Nchemba alisema mbali na walimu hao wapya
kutokupangiwa vituo, walimu wengine wanadai malimbikizo ya fedha zao na
kwamba hawajalipwa kutokana na ufinyu wa bajeti serikalini
0 comments :
Post a Comment