Tanzania
ina wanachama hai zaidi ya 600 wa kundi la watu wenye imani ya siri ya
Freemasons wakiwa wanatokana na watu wa kada mbalimbali wakiwemo
maarufu, huku ikielezwa kwamba miongoni mwao hakuna viongozi wakuu wa
serikali.
Hayo
yalibainishwa na Kiongozi wa kundi la Freemasons katika eneo la Afrika
Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama Sir Andy Chande.
Kiongozi
huyo Mtanzania mkazi wa Dar es Salaam mwenye asili ya Kiasia, alisema
licha ya Tanzania kuwa na wanachama hao, kwa sasa idadi ya wanachama
duniani inapungua tofauti na inavyoonekana sasa kuwa wanaongezeka
kutokana na kuibuka maneno mengi kuhusu kundi hilo.
Alisisitiza
kuwa si rahisi kumjua mwanachama wa kundi hilo, bali wenyewe ndio
wanaofahamiana, akisema ni siri na kwamba wenyewe wanakutana katika
vikao mbalimbali mara moja kwa mwezi au zaidi.
Alisema
nchini kuna wanachama zaidi ya 600 wakiwemo wafanyabiashara, watumishi
serikalini, walimu pamoja na wanataaluma mbalimbali wanaoheshimika sana
na kusisitiza kuwa kuna maneno mengi yanayosemwa kuhusu kundi hilo,
ambayo siyo ya kweli.
Alisema
idadi ya wanachama wake duniani inazidi kupungua kutoka milioni nane
hadi sasa wako milioni sita, tofauti na wengi wanaodhani kuwa idadi hiyo
inaongezeka.
Chande
alizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Shule ya Sekondari ya
Shaaban Robert ambako yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule alipozungumzia
maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Alisema
duniani kuna watu wazito wengi ambao ni wanachama wa kundi hilo kama
majaji wakubwa na hata Binamu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza ni
kiongozi mkubwa wa kundi hilo.
Akizungumzia
masharti ya kujiunga na kundi hilo, Chande alisema ni lazima mwanachama
huyo awe anaamini katika Mungu bila kubagua iwapo ni Mkristo au
Muislamu.
Alisema
pia ni lazima anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21 na walio
chini ya umri huo hawaruhusiwi kujiunga na lazima familia ya anayetaka
kujiunga na wanandugu wafahamu kuwa umejiunga na kundi hilo.
“Unajua
katika imani hii kuna michango mbalimbali ambayo unatakiwa kutoa ambayo
ni zaidi ya dola milioni sita (karibu Sh bilioni 10), hivyo ni lazima
ndugu wafahamu ili kuepuka matatizo utakapotakiwa kutoa,” alisisitiza.
Alisema
si kweli kuwa wenye fedha wengi ni wanachama wa kundi hilo huku
akikanusha wanachama wanajiunga kwa ajili ya kupata fedha, bali ni dini
kama imani nyingine.
Alisisitiza
kuwa hakuna ukweli kwamba wanaopata mafanikio katika maisha wakiwa
ndani ya imani ya Freemasons kuwa wanatoa kafara watu wao wa karibu kwa
lengo la kupata utajiri.
Chande
pia alisema hairuhusiwi kutumia jina la kundi hilo kwa nia ya kujipatia
nafasi sehemu mbalimbali au kuongeza nafasi katika chuo au shule.CHANZO:THE CHOICE
0 comments :
Post a Comment