Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mjema akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu habari za upotoshaji
zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya
kijamii kuhusu chuo hicho, leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Mkuu
wa chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam Prof.
Emanuel Mjema amesema kuwa habari zilizoandikwa na kuchapishwa na gazeti
moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya kijamii hapa nchini
zililenga kukidhalilisha chuo na kuipotosha jamii kufuatia chuo hicho
kuendelea kufanya vizuri katika kulinda maadili na viwango vya taaluma
hapa nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mkuu wa chuo hicho
amesema kuwa habari zilizochapishwa kuhusu kuwekwa kwa mfumo wa kamera
za kisasa madarasani na taarifa ya kufukuzwa kwa mwalimu mmoja wa chuo
hicho akihusishwa na vitendo vya ngono na wanafunzi zimepotoshwa na
vyombo hivyo kwa kukosa weledi wa kushindwa kupata uhalisia na usahihi
wa habari husika kutoka mamlaka za chuo hicho.
Prof.
Mjema amesema kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara ni Chuo cha Serikali
ambacho kimekua kikitoa Elimu ya Biashara kwa miaka 49 na kuongeza kuwa
chuo hicho kinaajiri wakufunzi wake kupitia utaratibu wa serikali wa
kutangaza nafasi za kazi kupitia Tume ya Ajira iliyopo chini ya Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma.
Ameongeza
kuwa chuo hicho kina wakufunzi na wataalam wanaoheshimu maadili ya
utumishi wa umma na taaluma zao na kuongeza kuwa chuo hicho kina
wakufunzi wenye sifa ambao hawahitaji kufuatiliwa na mtu katika kazi
zao.
“Nachopenda
kusema ni kwamba chuo chetu sasa kinao wataalam na wakufunzi wenye sifa
na walioajiriwa kwa kuzingatia kanuni na vigezo vilivyowekwa,taarifa
zilizotolewa hazina ukweli wowote na zimelenga kukidhalilisha chuo na
kuipotosha jamii”
Amesema
kuwa kamera za kisasa ziilizofungwa katika vyumba vya madarasa vya chuo
hicho zimewekwa kwa lengo la kudhibiti udanganyifu katika mitihani na
kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za chuo na kuongeza kuwa juhudi
zinafanyika katika mwaka ujao wa fedha kuongeza vifaa hivyo hasa katika
maeneo ya kuingilia nay ale yanayotumiwa na watu wengi chuoni hapo.
“Napenda
kuwafahamisha kuwa kamera za CCTV tulizonazo zimefungwa katika vyumba
vya madarasa kulingana na teknolojia iliyopo sasa na ni jambo la kawaida
na zimefungwa kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa lengo la kutoa
wataalam waliobobea na si kama ilivyoandikwa kwa kupotoshwa na gazeti
hilo na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa zinalenga kudhibiti vitendo
vya ngono darasani” amesema Prof. Mjema.
Aidha
kuhusu hali ya ulinzi na usalama chuoni hapo amesema kuwa chuo hicho
kimekuwa na utaratibu wa kuweka walinzi getini kwa miaka 49 na kuongeza
kuwa hakuna walinzi wapya walioajiriwa kwa ajili ya kukagua mavazi ya
wanafunzi hao huku akibainisha kuwa utaratibu uliopo sasa wa kukagua
vitambulisho kwa wanafunzi wanaoingia chuoni hapo na wageni wengine
wanaoingiia ni wa kawaida kwa ajili ya usalama wa chuo.
Katika
hatua nyingine Mkuu wa chuo hicho amesema kuwa chuo hicho kitaanza
kutoa masomo ya juu kwa ngazi ya shahada za uzamili kuanzia mwaka ujao
wa kitaaluma na kutoa wito kwa wananchi kuichangamkia fursa hiyo.
Pia
amesema kuwa chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha “Eastern
Finland” kitaanza kutoa shahada za umahiri na kufafanua kuwa wataalam wa
kuifanya kazi hiyo hapa nchini wapo.
“Tutaanza
kutoa mafunzo kwa ngazi ya shahada za uzamili katika mwaka ujao wa
kitaaluma, wahadhiri wanaofundisha sasa hapa chuoni wana elimu za juu
hivyo kuwezesha mchakato huo kuanza”
Katika
kuboresha kiwango cha elimu chuoni hapo Prof. Mjema ameeleza kuwa Chuo
chake tayari kimeingia mkataba na chuo Kikuu cha masuala ya Teknolojia
cha Shenyang , kilichopo nchini china ambapo wanafunzi wa vyuo vya CBE
nchini wataweza kwenda China kumalizia masomo yao kwa mfumo wa
kubadilishana.
“ Ni
hatua nzuri katika maboresho ya elimu katika chuo chetu kwa kushirikiana
na vyuo vya nje hasa Finland na China na sasa baadhi ya wanafunzi
wameshaanza kunufaika” ameeleza Prof. Mjema.
MATUKIO MICHUZI
0 comments :
Post a Comment