Dar es Salaam. Wiki mbili zilizopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliadhimisha sherehe za kutimiza miaka 37 tangua kuanzishwa, huku kikiwa na mambo matano yanayokikaba koo.
Pamoja na CCM kuendelea kuongoza nchi, ni dhahiri
chama hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi zinazoweza kusababisha
kusambaratika au kung’olewa madarakani katika uchaguzi ujao wa 2015.
Dalili za kusambaratika zinatokana na mgawanyiko
wa makundi, yakiwemo yale yanayonyoosheana vidole kwa ufisadi, harakati
za urais 2015, hali inayoendelea ya kuumbuana hadharani huku kashfa na
tuhuma za rushwa na ufisadi ndani ya chama na katika Serikali yake
ziliendelea kutamalaki, mambo ambayo yanaipa picha mbaya CCM mbele ya
Watanzania.
Jambo jingine ni suala la kutetea Serikali mbili
ndani ya Katiba Mpya. Iwapo CCM itashindwa kutetea mfumo wa sasa wa
Serikali mbili, huenda ikawa ni mwanzo wa kuonekana kuwa imeshindwa
kudumisha yale yaliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili; Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati, Abeid Karume.
Waasisi hao walipounganisha Zanzibar na Tanganyika
na kuzaa Tanzania, waliona Serikali mbili ndizo zinazofaa kujenga
mshikamano wa taifa moja, wakiamini kuwa Serikali tatu zingepanua wigo
ule wa umoja.
Hata hivyo, Pius Msekwa ni mmoja wa viongozi
wazoefu wastaafu ambao wametumikia chama hicho tangu mwaka 1960,
anapingana na mambo hayo, akiamini kwamna CCM bado ni imara na inaendela
kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.
Kuumbuana ndani ya CCM
Pamoja na athari za wazi zinazoonekana, Msekwa
anasema kauli za kuumbuana na kupakana matope zinazoendelea kujitokeza
ndani ya chama hicho kuhusu urais 2015 hazina athari zozote kwa chama
wala Serikali.
“Si jukumu la chama kuwanyamazisha watu, ila
wasikilizaji wa kauli hizo watachambua mchele na pumba,” anasema Msekwa
na kuongeza kuwa vitendo vya viongozi ndani ya CCM kunyoosheana vidole,
kushutumiana na hata kudharauliana hadharani vinaashiria uhuru wa
demokrasia ya maoni ndani ya chama.
Hivi karibuni Mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana
wa CCM (UVCCM), Paul Makonda alitoa msimamo ukimtuhumu Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa kuanza kampeni za urais 2015 na kumwelezea kuwa
hafai na wala hana sifa za kuwa rais.
Kauli za Makonda ziliungwa mkono na Makamu
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, John Malecela ambaye pia alimshutumu Lowassa
akidai tayari ameanza kampeni za urais kwa kusambaza fulana
zinazohamasisha mtandao wa marafiki zake.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kpamoja na
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nnape Nnauye, katika miezi ya karibuni
waliibua suala la mawaziri saba mizigo na kuwatangaza hadharani
wakimtaka Rais Jakaya Kikwete awachukulie hatua.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment