KWA miaka mingi Watanzania wamekuwa wakijadili mengi, lakini
hawakupata fursa pana ya kujadili Mkataba wa Muungano ‘Articles of
Union’ uliyosainiwa na Nyerere na Karume.
Haijapita miaka mitatu tangu baadhi ya Wazanzibari walipojaribu
kuupata mkataba huu katika mamlaka zinazohusika, wakaambiwa hauonekani.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akizungumza kwa hasira katika mkutano mmoja wa hadhara mjini Zanzibar, alisema:
“Mkataba wa Muungano upo kwenye makabati ya Ikulu. Hapo hapo, akasema
wanaotaka kuuona mkataba huo wajaribu kuupata kutoka United Nations,”.
Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu mwaka jana alipowasilisha Hotuba
ya Kambi ya Upinzani bungeni, alielezea dai la Serikali ya Tanganyika,
lakini akatamka wazi kuwa:
“Hatutaki kuona picha za Nyerere na Karume wakichanganya udongo..tunataka Mkataba wa Muungano,”.
Ikumbukwe, miaka miwili nyuma, kule ‘Jamii Forums’ walitafuta kitabu
cha Julius Nyerere, kiitwacho ‘Uongozi wetu na Hatima ya Tanganyika’.
Ili kujiridhisha.
Leo tena, tunawaletea Mkataba wa Muungano ‘Articles of Union’. Wapo
wanaosema Mkataba huu ndiyo mama wa Katiba zote mbili yaani ya Muungano
na ya Zanzibar.
Wapo wanaosema yale mambo 11 ya Muungano yameongezwa kadhaa, sasa Mkataba huu hapa, tuangalie ukweli wake.
MKATABA WA MUUNGANO BAINA YA JAMHURI YA TANGANYIKA NA JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR
Kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa
Zanzibar zinafahamu uhusiano wa muda mrefu watu wake na mshikamano na
kukuza uhusiano huo na kuimarisha mshikamano na kukuza umoja wa watu wa
Afrika, zimekutana na kutafakari Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya watu wa Zanzibar.
Na kwa kuwa Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa
Zanzibar, zinapendelea ya kwamba Jamhuri hizi mbili ziungane kuwa
Jamhuri moja huru.
Moja ya masharti ya makubaliano yafuatayo:
Kwa hiyo IMEKUBALIWA baina ya Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar, kama ifuatavyo:-
I) Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa Jamhuri huru moja.
II) Katika kipindi cha kuanza kwa Muungano mpaka Baraza la Kutunga
katiba lililotajwa katika ibara ya (vii) litakapokutana na kupitisha
katiba ya Jamhuri ya Muungano (Kuanzia hapa kitaitwa kipindi cha mpito),
Jamhuri ya Muungano itaongozwa kwa masharti ya ibara ya (iii) mpaka ya
(vi).
III) Katika kipindi cha mpito katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa katiba ya Tanganyika iliyorekebishwa ili kuweka:
a) Chombo tofauti cha kutunga sheria na Serikali kwa ajili ya
Zanzibar kwa mujibu wa sheria zilizopo za Zanzibar na vitakuwa na
mamlaka ya mwisho katika Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa yale tu
yaliyo chini ya bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
b) Nafasi ya makamo wawili wa Rais mmoja kati yao akiwa ni mkaazi wa
Zanzibar atakuwa ndiye kiongozi wa Serikali iliyotajwa kwa ajili ya
Zanzibar na atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa rais wa Jamhuri ya Muungano
katika utekelezaji wa kazi za Serikali kwa upande wa Zanzibar.
c) Uwakilishi wa Zanzibar katika bunge la Jamhuri ya Muungano.
d) Mambo mengine yatayofaa au kuhitajika ili kuipa nguvu Jamhuri ya Muungano na mkataba huu.
IV) Mambo yafuatayo yatakuwa chini ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano:-
a) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
b) Mambo ya nchi za nje
c) Ulinzi
d) Polisi
e) Mamlaka yanayohusika na hali ya hatari
f) Uraia
g) Uhamiaji
h) Mikopo na biashara ya nchi za nje
i) Utumishi katika Jamhuri ya Muungano.
j) Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa
forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na kusimamiwa na
idara ya forodha
k) Bandari, mambo yanayohusu usafiri wa anga, Posta na Simu.
V) Bunge na Serikali vilivyotajwa vitakuwa na mamlaka ya mwisho juu
ya mambo yote yahusuyo Jamhuri ya Muungano na kuongezea mamlaka juu ya
mambo yote yahusuyo Tanganyika.
Sheria zote zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kutumika katika maeneo yao bila kuathiri:-
a) Masharti yoyote yatakayowekwa na chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria.
b) Masharti yatakayowekwa kwa amri ya Rais wa Zanzibar juu ya sheria
yoyote inayohusu jambo lolote lililotajwa kwenye ibara ya (iv), na
kufuta sheria yoyote inayolingana Zanzibar.
c) Mabadiliko yoyote kama yataonekana yanafaa au kuhitajika ili kufanikisha Muungano na mkataba huu.
a) Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa ni Mwalimu J. K.
Nyerere na ataongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kufuata
masharti ya mkataba huu na kwa kusaidiwa na maofisa wengine
atakaowateuwa toka Tanganyika na Zanzibar na watumishi wa Serikali zao.
b) Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
BLM kutoka Zanzibar aliyeteuliwa kwa kufuata marekebisho kama
yalivyoelezwa na ibara ya 3, atakuwa Sheikh Abeid Amani Karume.
VI) Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kukubaliana na Makamu wa Rais ambaye ni kiongozi wa serikali ya Zanzibar.
a) Atateua tume kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa ajili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
b) Ataitisha Baraza la kutunga Katiba ikiwa na wawakilishi kutoka
Tanganyika na Zanzibar katika idadi itakayoamuliwa likutane katika
kipindi cha mwaka mmoja tokea kuanza kwa muungano kwa madhumuni ya
kutafakari mapendekezo ya tume iliyotajwa juu na kupitisha Katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
VII) Mkataba huu utahitaji kuthibitishwa kwa kutungiwa sheria na
Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar kwa kushirikiana na Baraza lake la Mawaziri, na mkataba
kupitishwa na kuundwa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar
kwa kufuata masharti yaliyokubaliwa.
KWA KUSHUHUDIA HAPA: Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika na Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
wametia saini nakala mbili za mkataba huu, hapa Zanzibar siku ya tarehe
Ishirini na mbili ya mwezi Aprili, 1964
……………………………………………………………………………… …………………….
Umepitishwa na Bunge siku ya tarehe Ishirini na Tano ya Aprili, 1964
……………………………………………………………………………… …………………….
Pius Msekwa, Karani wa Bunge la Tanganyika
……………………………………………………………………………… …………………….
Adam Sapi Mkwawa, Spika wa Bunge la Tanganyika
25 Aprili 1964
ORIGINAL SOURCE:
1: {THE PATNERSHIP, ISBN: 9789987880553, pg. 156, Author: Aboud Jumbe – Rais Mstaafu wa Zanzibar}
2: {Zanzibar hadi mwaka 2000: ISBN: 9789987898015, pg. 201, Author: Ali Shaaban Juma}
SOURCE:WIPO
Home
/
habari za kitaifa
/
HUU NDIYO MKATABA WA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR (The Articles of Union)
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment