-->

MBOWE ASHTUSHWA NA KAULI YA RAISI DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE

mbatia_36bc7.jpg
Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia siku za hizi karibuni. Picha na Maktaba
Kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wanachama, wadau na makada wa CCM, kuondokana na unyonge, imepokewa kwa hisia tofauti huku ikielezwa kuwa ni ya vitisho.
Juzi, wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho tawala alisema: "Ni wakati wa kuacha unyonge na uvumilivu una kikomo chake."
Alisema CCM inaingia kwenye uchaguzi huku ikishindana na wagomvi: "...Ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wao kufanya siasa," alisema Kikwete bila kutaja jina la chama chochote cha siasa.
Alisema amechoshwa na vitendo vya ugomvi huku akitolea mfano wa tukio la Kahama mkoani Shinyanga ambako kijana mmoja alitolewa macho kwa bisibisi na mwingine kumwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga, mkoani Tabora.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza kushangazwa kwake na kauli ya Rais Kikwete akisema: "Nimeipokea kwa mshtuko na ninawataka wafuasi wa chama changu kuwa watulivu na kuchukua tahadhari kubwa."
"Nilichokifanya ni kuwaagiza wafuasi wa Chadema kufanya kampeni za kistaarabu kwa kutolipiza kisasi ili kuhakikisha kwamba hakuna damu ya Mtanzania itakayomwagika Kalenga," alisema.
Hatua ya Rais Kikwete, imekuja baada ya CCM kumtangaza, Godfrey Mgimwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga. Mgimwa ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha, hayati Dk William Mgimwa aliyefariki mwezi uliopita nchini Afrika Kusini.
Mgombea huyo atachuana na mgombea wa Chadema, Grace Tengega.
Jana, Mbowe alisema ingawa Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM, alitakiwa kufahamu kwamba ni kiongozi wa nchi na ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye vikosi vya Ulinzi na Usalama vipo chini yake.
"Anapotoa kauli nzito kama hiyo, inatakiwa afahamu kwamba yeye si Mwenyekiti wa CCM tu, bali ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, hakustahili kutoa kauli kama hiyo inayoweza kuamsha hisia," alisema Mbowe.
Alisema kauli zake za kiitikadi za kupendelea chama chake wakati akifahamu kuwa yeye ni kiongozi wa Watanzania wote, zinawafanya wananchi wagawanyike kwa misingi ya vyama.
"Rais Kikwete anadai kwamba mtu wao alimwagiwa tindikali na mwingine kutolewa macho kwa bisibisi, lakini hazungumzii viongozi na wanachama wa Chadema waliouawa kwa kupigwa risasi na wengine kwa mabomu. Anasema hayo huku akifahamu fika kwamba kuna vyombo vya dola na Mahakama ambavyo vinashughulikia matukio hayo."
CHANZO:MJENGWA
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment