-->

PASTOR AFARIKI DUNIA KATIKA NYUMBA YA MWANAMKE

Hali ya taharuki ilikumba mtaa wa Buruburu, Nairobi baada ya mwili wa kasisi kupatikana katika chumba cha kulala cha mwanamke aliyesemekana kuwa muumini wa kanisa la pasta huyo.

Estate Za Buruburu Nairobi
Kasisi huyo mwenye umri wa miaka 70 alisemekana kutembelea mwanamke huyo katika mtaa wa Buruburu Phase 1 mwendo wa saa tano asubuhi na kukaa ndani ya chumba hicho siku nzima.

Maafisa wa polisi walisema mwili wa kasisi Geoffrey Maingi ulipatikana bila majeraha yoyote.
Mkuu wa Polisi wa Buruburu Richard Kerich alisema kasisi huyo anayehudumu katika kanisa la Redeemed Gospel Buruburu aliliegesha gari lake katika duka la Tuskys mtaani humo kabla ya kuelekea kwa mwanamke huyo.

Mwanamke mwenye chumba hicho alisema kasisi huyo alikuwa ameenda kumuombea na kuongeza kuwa hakujua iwapo alikuwa mgonjwa.

“Si mara ya kwanza kwake kuja tushiriki maombi pamoja. Amekuwa akinitembelea mara kwa mara,” alisema mwanamke huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 40 aliwaambia polisi kuwa kasisi huyo alianguka ghafla na kufariki.
“Kando na kuwa pasta wangu yeye pia ni rafiki na ndio maana huwa tunashiriki maombi pamoja,” akasema

Jirani wa mwanamke huyo alithibitisha kuwa kasisi huyo amekuwa na ziara kadhaa chumbani humo.

Tukio hilo lilivutia umati mkubwa huku baadhi ya wakazi wa mtaa huo wakidokeza kuwa huenda kifo cha pasta huyo kilitokana na matumizi ya dawa za kuongeza hamu/ashiki za mapenzi.

“Hii ilikuwa adhabu ya Mungu kwa kasisi huyo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo. Mungu alikuwa anataka kuleta vitendo vyake vya gizani hadharani,” jirani mmoja alinukuliwa.

Majirani walisema mwanamke mshukiwa alikosana na mumuwe mwaka uliyopita kufuatia mzozo wa kifamilia.

Waendesha teksi walisema kuwa mwanamke huyo aliwaomba msaada ampeleke hospitalini lakini tayari alikuwa amekufa.

Kuachiliwa:
“Alikuja hapa akitaka tumpeleke marehemu hospitalini lakini baada ya kufika kwake tulipata mwili wake ukiwa baridi kumaanisha alikuwa ashakufa,” alisema mhudumu wa teksi ambaye alisema baadaye waliwajulisha maafisa wa polisi.

Polisi walimzuilia mwanamke huyo kwa saa kadhaa ili kutoa habari kuhusu kisa hicho lakini wakamwachilia baadaye.
“Tutabaini chanzo cha kifo cha kasisi baada ya mwili wake kufanyiwa upasuaji, kwa sasa hauwezi kutoa taarifa yoyote,” alisema Bw Kerich .

Bw Kerich alisema kuwa polisi wamekusanya bidhaa katika chumba hicho ambazo zitatumiwa katika uchunguzi.

Mwili wa marehemu ambao polisi walisema haukuwa na majeraha yoyote ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City kufanyiwa upasuaji.

Waumini wa kanisa la Redeemed Gospel Buruburu walifika katika eneo hilo na kuondoa gari la pasta huyo ili kuzuia wanahabari kulipiga picha.
CHANZO:WACHIMBA RIZIKI

Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment