Nimesoma uchambuzi wa The Citizen asubuhi hii kuhusu gharama za maisha Dodoma. Kwamba kwa utafiti wao, ( The Citizen) laki mbili zinatosha mpaka kumlipa dereva na kiasi kingine unaweza kuweka akiba.
Na hakika, huhitaji utafiti kuelewa ukweli huu. Mimi nimefika Dodoma zaidi ya mara kumi. Sijawahi kutumia zaidi ya elfu 50 kulala kwenye nyumba ya wageni ya hadhi kabisa, na asubuhi unaikuta mezani chai na sahani ya mayai ya kukaangwa, achilia mbali matunda.
Sasa Dodoma waliyokwenda wabunge hawa ni Dodoma ya nchi gani?
Kwa mtazamo wangu, hiyo laki mbili kwa siku ingepunguzwa na iwe laki na nusu tu. inatosha kabisa. Na kwa nini wanaunda kamati kujadili posho? Tuliandika, kuwa tutaviona vioja...
Na je, hivi hawa wajumbe wa Baraza la Katiba huko walikotoka si wana kazi zao. Ina maana na mishahara yao imesimamishwa kwa siku 70? Kama wanaendelea kupokea mishahara yao kwa kweli waione kazi yao hii ya Dodoma ni kama kujitolea kwa nchi yao.
Ni heshima kubwa waliyopewa. Laki moja na nusu ingetosha kabisa na hata wangejitolea pia baadhi ya siku wafanye kazi bila posho. Wafanye hivyo ili kuonyesha kwa dhati uzalendo wao kwa nchi waliyozaliwa.
Ee Mola, uwajaze mioyo ya uzalendo wajumbe wetu wa Baraza la Katiba..
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0 comments :
Post a Comment