Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakinyoosha mikono ili wapatiwe Rasimu ya Kanuni zitakazoendesha bunge hilo
Madai ya
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya
Bunge hilo yamegonga mwamba, Mwananchi limebaini.
Habari
kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la
Katiba, Pandu Ameir Kificho ili kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa
baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe wa kamati hiyo hawakuona sababu ya
kupendekeza posho hizo kupandishwa.
Taarifa
hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia uamuzi huo baada ya kupitia
viwango vya posho vinavyolipwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.
Pia
kamati hiyo ilichambua viwango vya posho walivyolipwa wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na viwango vya posho ya kujikimu vya Sh80, 000 kwa
siku wanavyolipwa watumishi wa Serikali.
"Hili
jambo linahitaji busara sana na kutazama mazingira ya nchi pia, kwa hiyo
wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango vya posho vya taasisi
mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha," alisema mmoja wa wajumbe ambaye
hakutaka jina lake kutajwa.
Mjumbe
mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa, alisema kuwa watakaa leo
kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya kuikabidhi kwa Mwenyekiti
Kificho.
Alisema
pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge, lakini isingekuwa rahisi kuongeza
posho katika mazingira ya sasa, ambapo wananchi wanalia hali ngumu ya
maisha.
Wajumbe
hao walioteuliwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir
Kificho ni William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul
Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Awali,
taarifa kutoka ndani ya Bunge zilidokeza kuwa wajumbe hao walikuwa
wakutane jana saa 9:00 alasiri ili kuandaa ripoti itakayopelekwa kwa
Kificho ikiwa imebeba ushauri kuwa kiwango cha sasa cha posho kinatosha.
Sh300,000
wanazolipwa wajumbe wa Bunge Maalamu la Katiba zinajumuisha Sh80,000
kwa siku ambayo ni posho ya kujikimu na Sh220,000 kwa siku kama posho
maalumu ya kuhudhuria kikao.
Posho
maalumu ya Sh220,000 inajumuisha posho ya dereva inayopaswa iwe kati ya
Sh40,000 na Sh45,000 kwa siku, usafiri wa ndani (mafuta ama teksi),
mawasiliano na matumizi mengine binafsi.
Ofisi ya Bunge Maalumu
CHANZO:MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment