
KAMATI ndogo ya maadili ya CCM jana iliendelea kuhoji wanachama wake
ambao wanatajwa kuanza harakati za urais kinyume na utaratibu wa chama.
Jana ilikuwa zamu ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Januari Makamba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu,
Steven Wassira.
Hiyo ni baada ya juzi Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu
mstaafu Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
kuhojiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano
yaliyofanyika katika jengo la makao makuu ya CCM maarufu kama White
House mjini hapa, Januari ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema
hakukuwa na mashitaka bali ushauri.
Alisema ushauri huo ulihusu namna ya kupata viongozi kwa ajili ya
kuimarisha chama badala ya kukigawa hasa katika kipindi cha kuelekea
uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
“Hakukuwa na habari ya mashitaka bali kutoa ushauri na kukumbushana
misingi ya namna ya kupata uongozi na kuimarisha chama badala ya
kukigawa,” alisema.
Januari alisema binafsi amefurahi kupata nafasi ya kuitwa na kutoa
ushauri. Alisema hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwake kutoa mawazo na maoni
yake, lakini hata hivyo alishangaa kuitwa Dodoma kujieleza.
Pia alisema kuna faida kubwa ya kujulikana mapema kuliko mwishoni, kwani
watu wanapata nafasi ya kukujadili na kutoa mawazo yao kama unafaa kuwa
kiongozi au la.
“Mbaya kama unatoa fedha inakuwa unawaweka pembeni watu wenye vipaji vya uongozi,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu anapotumia fedha kupata
uongozi ni lazima sheria ichukue mkondo wake na achukuliwe hatua.
“Kuitwa ni jambo la kawaida, hakuwezi kutoa sababu ya wewe kujitafakari
na kujipima,” alisema.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika mahojiano
hayo, alisema hajawahi kutangaza nia ya kugombea urais na wala si dhambi
mtu kutamani kuwa Rais wa Nchi.
Wassira alisema hakuitiwa tuhuma ila waandishi wa habari wamefanya
mkutano uwe wa tuhuma lakini amesema wamezungumzia juu ya mustakabali wa
kuelekea uchaguzi mkuu 2015. Alisema magazeti mengi yaliripoti kuwa
wanaitwa kwa tuhuma ya kutangaza nia kabla ya wakati.
"Sijawahi kutangaza kugombea Urais, kwani ni kosa kutangaza kugombea Urais?" alihoji Wassira na kuongeza:
"Kuna barua na magazeti ambayo yanatofautiana juu ya kuitwa Dodoma,
andikeni ukweli mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu siwezi kuvuruga chama.”
Alipohojiwa kwa nini wameitwa wanachama sita tu, alisema hafahamu idadi
ya wanachama walioitwa kuhojiwa isipokuwa anachojua yeye kama Wassira
ameandikiwa barua na kuitwa Dodoma.
"Sio dhambi kutamani kuwa Rais, kwani ni nafasi moja kwa Watanzania wote
na kila mtu anayo haki ya kuomba nafasi hiyo ila utaratibu ufuatwe,"
alisema. Hata hivyo alisisitiza kuwa hajawahi kutangaza nia. Huku akiwa
na mbwembwe za aina yake hasa pale waandishi walipoanza kumpiga picha
alisema:
"Mimi sijatangaza nia na sina muda wa kutangaza leo mpaka wakati
ukifika, huku akisogea kupigwa picha na kutaka apigwe picha nyingi.
"Pigeni picha nyingi , pigeni mpaka mchoke mkimaliza ndio niondoke,"
alisema.
Kamati hiyo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Philip
Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na aliyekuwa Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha. Hatua ya
kuhojiwa kwa wanachama hao, inatokana na agizo la Mwenyekiti wa CCM,
Rais Jakaya Kikwete likitaka kamati za usalama na maadili za chama hicho
kubana wanachama wanaokiuka maadili. Baada ya kuhojiwa juzi, Lowassa
aliwaambia waandishi wa habari:
"Tumeshauriana na kukubaliana vizuri tu, ili kukisaidia chama kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015," na kuongeza:
"Sijibu lawama, kwa vile hakikuwa kikao cha lawama, kilikuwa cha mazungumzo na ndani ya kikao hakukuzungumzwa makundi."
Sumaye kwa upande wake, aliwaambia waandishi kuwa hawezi kusema lolote
kuhusu kilichojiri ndani ya kikao hicho na badala yake anasubiri wakubwa
(Kamati) wazungumze ndipo naye aseme. Mbunge Ngeleja alisema chama kina
utaratibu wake na taarifa ya kikao hicho itatolewa na msemaji wa chama.
"CCM ni chama chenye Katiba na kanuni zake na wakati wa kutangaza nia ndani ya CCM bado haujafika," alisema.
Alisema kwa mujibu wa CCM, wao wanaongozwa na kanuni, na wenye nia ya
kugombea muda haujafika na si jambo la ajabu chama kuita watu wake
kuwahoji.
"Binafsi sijatangaza nia ya kugombea urais… kama kuna ugomvi mimi siko
kwenye ugomvi huo," alisema Ngeleja. Wengine wanaosubiri kuhojiwa ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments :
Post a Comment