Yala ni
shule ya msingi iliyopo katika Kijiji cha Yala Kata ya Luhanga Wilaya ya
Mbarali mkoani Mbeya na ipo umbali wa kilomita 40 kutoka Barabara Kuu
ya Mbeya-Iringa, ili kufika shuleni hapo inakulazimu kutembea kwa mguu
kutokana na magari na pikipiki kushindwa kufika.
Shule
hiyo ina muda wa zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, imezungukwa
na mito minne ambayo imekuwa ikijaa maji kipindi cha masika na
kusababisha kukatika kwa mawasiliano na ukosefu wa huduma mbalimbali
ikiwa ni pamoja na elimu.
Kutokana
na tatizo hilo la mito kujaa maji shule hiyo imekuwa ikigeuka kuwa
kisiwa na kusababisha wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni kwani
mito hiyo haina madaraja ya kuwawezesha kupita na kufika shuleni hapo.
Wanafunzi
wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa wakitoka katika Vitongoji vya
Mwashikamile, Ruaha, Waninyika, Mtakuja, Yala na Lusaka na wote
hushindwa kuvuka mito hiyo na kufika shuleni huku walimu pia wakikumbwa
na adha hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na nyumba za kuishi Walimu.
Jairos
Mpale ni Mwenyekiti wa serikali ndogo ya maendeleo ya Mwashikamile
katika Kijiji cha Yala anasema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi kwa
mwaka huu ukilinganisha na miaka mingine.Hii ni kutokana na mvua
zinanyesha kwa wingi na wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu bila
kwenda shule.
"Watoto
wetu wameshindwa kwenda shuleni hapo tangu shule zote zilipofunguliwa
Januari, kutokana na mito kujaa maji na kuna mamba wengi na viboko hivyo
ni vigumu kuvuka kwenda katika Shule ya Yala na watoto wetu wamekosa
masomo na hatujui ni lini wataanza masomo," anasema.
Naye
Mtendaji wa kijiji cha Yala shule ilipo, Isaac Ngera anasema kuwa tatizo
hilo huwa linajitokeza mara kwa mara katika msimu wa mvua na mito hiyo
imekuwa ikijaa na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma
mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja elimu, afya na majisafi na salama.
Aliitaja
mito iliyojaa maji kuwa ni Itambo na lwashimala na vitongoji vilivyopo
ng'ambo ya mito hiyo ni Ruaha na Woninyika kwa upande wa Kusini kuna
vitongoji vya Mtakuja na Lusaka ambavyo vipo ng'ambo ya Mto Itambo na
yote imejaa maji hakuna mawasiliano na upande wa pili.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo Stephano Mlewa anasema kuwa kwa sasa hali ni mbaya
katika shule hiyo kwani hakuna mwanafunzi anayefika shuleni hapo.
"Siyo kwa
wanafunzi pekee hata kwa Walimu ni tatizo kubwa kwani wanaishi katika
kitongoji ambacho kipo mbali na shule hiyo na inawalazimu wavuke mito
miwili ambayo kwa sasa imejaa maji hivyo hakuna masomo," anasema.
Anasema
kuwa shule hiyo pia ina changamoto ya madarasa kwani ina jumla ya vyumba
vya madarasa vinne pekee na wanafunzi wapo kuanzia darasa la kwanza
hadi la saba hivyo husoma kwa kupokezana.
Ofisa
Elimu Wilaya ya Mbarali, Henerico Batinoluho anasema kuwa shule ina
wanafunzi zaidi ya 400 na kwamba mwaka huu shule ilifunguliwa Januari 6,
lakini wamefanikiwa kuingia darasani katika kipindi cha wiki moja
pekee.
CHANZO: MWANANCHI
(J M)
0 comments :
Post a Comment