Polisi nchini Burundi wanasema
zaidi ya mafuvu 40 ya binadam yamepatikana katika makao ya raia mmoja wa
Italia anayefanya kazi nchini humo.
Giussepe Favaro alikamatwa mwezi uliopita baada
ya mafuvu mawili yaliyonuiwa kusafirishwa kwa ndege kunaswa katika
uwanja wa ndege nchini Burundi.Kwa mujibu wa polisi mafuvu hayo yalinuiwa kusafirishwa hadi nchini Thailand.
Polisi hata hivyo hawajatoa taarifa zaidi na mwandishi wa BBC nchini Burundi anasema watu wana shauku ya kutaka kujua mafuvu hayo yalitoka wapi na yalikua yatumike kivipi.
Kumekuwepo ripoti za sehemu za miili ya binadam kutumika katika ushirikina hasa katika nchi jirani ya Tanzania,lakini haifahamiki kwanini mafuvu yaliyopatikana hapo awali yalikua yakipelekwa Thailand.
Bw Favaro amekua akiishi nchini Burundi kwa miaka kadhaa.
CHANZO:BBCSWAHILI
0 comments :
Post a Comment