Kila mwezi tembo 850 wanauwawa
Na Albano Midelo
TEMBO waliopo nchini wanaokadiriwa kuwa sio zaidi ya 70,000 watakuwa wamefutika katika uso wa dunia nchini kwetu miaka michache ijao endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kukabiliana na majangili.
Katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania ambayo ni Hifadhi ya Taifa kubwa kuliko zote nchini yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226 ina tembo zaidi ya 30,000 ,utafiti umebaini kuwa majangili yamekuwa yanawauwa tembo hao kwa kasi hali inayotishia uwepo wa wanyama hao ndani ya hifadhi hiyo.
Mkuu wa idara ya ulinzi katika hifadhi hiyo Paulo Gwaha anasema baadhi ya majangili ambao walikamatwa katika hifadhi hiyo walikutwa wakitumia silaha za kisasa zikiwemo zile ambao zilitumika katika vita ya Idd Amini wa Uganda kati ya mwaka 1978 hadi 1979.
Kwa mujibu wa Gwaha Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 jumla ya majangili 745 walikamatwa na kwamba tangu Desemba 2011 hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2012 jumla ya majangili 480 walikamatwa ambapo idadi kubwa ya majangili walikamatwa kabla hawajasababisha madhara katika hifadhi hiyo.
Takwimu kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire za mwaka 2007 zinaonyesha kuwa mwaka huo tembo waliouwawa walikuwa 42,mwaka 2008 tembo 29 na mwaka 2009 jumla ya tembo 33 waliuwawa.
Utafiti ambao ulifanywa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 1985 ulibaini kuwa vitendo vya ujangili ambavyo vilikuwa vinafanywa na jamii inayozunguka hifadhi hiyo vilisababisha idadi ya tembo katika hifadhi hiyo kupungua kutoka tembo 2500 hadi kufikia tembo wasiozidi 500 .
Afred Kikoti mhifadhi kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) anabainisha kuwa utafiti ambao ulifanywa mwaka 2011 unaonyesha kuwa ujangili unasababisha katika Tanzania tembo zaidi ya 30 kufa kila siku sawa na tembo 850 kwa mwezi na tembo zaidi ya 10,000 wanauwawa kila mwaka hali inayohatarisha wanyama hao kufutika katika Tanzania.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika pori la akiba la Selous hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 hata hivyo idadi ya tembo katika pori hilo imeshuka kutokana na kukithiri kwa ujangili hadi kufikia tembo 43,000 mwaka 2009 ambapo hivi sasa inakadiriwa huenda idadi ya tembo katika pori hilo imeshuka na kufikia 30,000 tu.
Shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa nchini China mwaka 2012 kutoka hapa nchini ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu. Wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa huko huko HongKong katika nchi ya China.
Matukio haya mawili ya shehena za meno ya tembo ni sawa na Tembo 900 waliouwawa.Hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa ujangili umeshamiri kwa kasi ya kutisha na kuhatarisha maisha ya wanyamapori hususani tembo.
Takwimu za Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii zinaonyesha kuwa mwaka 2010 hapa nchini jumla ya Tembo 10,000 waliuwawa, takwimu hizo ni sawa na Tembo 37 waliuwawa kila siku.
Kulingana na takwimu hizo hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2012 ambapo jumla ya Tembo 23,000 waliuwawa sawa na wastani wa Tembo 63 kila siku, kutokana na kasi hii ya ujangili, ifikapo mwaka 2018 inakadiriwa Tanzania haitakuwa na Tembo hata mmoja.
Waziri wa maliasili na utalii Balozi Hamis Kagasheki anatahadharisha kuwa nchi ya Ivory Coast ambayo ilipewa jina hilo baada ya kuwa na wanyama wengi aina ya tembo katika bara la Afrika, kutokana na serikali ya nchi hiyo kushindwa kuwalinda na kuwatunza tembo, hivi sasa nchi hiyo haina mnyama hata mmoja aina ya tembo.
Takwimu za wizara ya maliasili na utalii zinaonyesha kuwa bara la Afrika mwaka 1930 lilikuwa na tembo milioni 50 na kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo waliobakia katika bara nzima la Afrika ni laki tano tu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo hapa Tanzania miaka ya 1960 kulikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000 na kwamba wanyama hao walipungua hadi kufikia 130,000 mwaka 2002 na idadi ya tembo hapa nchini imeendelea kupungua kwa kasi ambapo hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa inakadiriwa kuna tembo wasiozidi 55,000 tu.
Sera ya Taifa ya wanyamapori ya mwaka 1998 inaelekeza kuwa aina zote za viumbe hai zihifadhiwe,wanyamapori wasitumiwe kiasi cha kuifanya idadi yao ipungue na kuwa katika hatari ya kutoweka,kuinua mchango unaotolewa na wanyamapori katika pato la Taifa,kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kumiliki wanyamapori na kusimamia kwa niaba ya wananchi.
Hata hivyo Kasi ya ujangili inayoendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka inaelezwa kuwa imechangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo kukua kwa uchumi wa nchi ya China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia.
Waziri Kagasheki amethibitisha kuwa miaka ya karibuni makonteina matatu yaliyosheheni meno ya tembo yalikamatwa katika nchi za Hong Kong,Vietnam na Philipines ambapo imebainika kuwa mwanzo wa safari ya makonteina hayo ilikuwa ni bandari ya Dar es salaam nchini Tanzania.
Ujangili dhidi ya tembo umeziathiri nchi zote za Afrika zenye Tembo kutokana na kushamiri kwa Biashara ya Pembe za Ndovu.Hata hivyo utafiti unaonyesha kuwa nchi za Tanzania, Kongo-DRC na Msumbiji zipo kwenye hatari zaidi ya Tembo wake wote kutoweka kama ilivyo katika nchi ya Ivory Coast kutokana na nguvu kubwa waliyonayo wafanyabiashara haramu wa Pembe za Ndovu.
Hata hivyo waziri Kagasheki amezitaja baadhi ya sababu zilizosababisha kushamiri kwa biashara haramu ya meno ya tembo hapa nchini kuwa ni umaskini wa watu,rushwa, mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa umma, mahakama na jeshi la polisi.
“Upo mtandao mkubwa wa watu wenye fedha,viongozi wa ngazi za juu serikalini,kuna maofisa usalama wa Taifa,TRA,mtandao unaojihusisha na biashara hii ni mkubwa ndani na nje ya nchi,unaotumia silaha na teknolojia ya kisasa,kasi ya kuuwawa kwa tembo hivi sasa inatisha kwa kuwa wanauwawa kwa maelfu’’,alisisitiza.
Waziri Kagasheki ameutaja mkakati wa wizara yake kuwa ni kuitisha mkutano mkubwa wa kimataifa wa wadau wa utalii utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili ya kutafuta njia sahihi ya kudumu katika kutokomeza ujangili wa wanyama hasa tembo katika hifadhi hapa nchini .
Naibu waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu anadai kuwa miongoni mwa wanaokwamisha vita dhidi ya ujangili ni wabunge kutokana na baadhi yao kudaiwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu.
“Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya tembo waliouwawa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Agosti 2013 ni 378 hali ni mbaya serikali tunawataka majangili wote wajisalimishe polisi vinginevyo hawatapona katika vita hii tutawasaka kila mahali’’,alisisiza Nyarandu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alisema idadi ya tembo imepungua sana katika mbuga za wanyama nchini, hali ambayo imefanya idadi sahihi ya tembo waliobaki kutojulikana hivyo inatakiwa kufanyika utafiti ili kupata takwimu sahihi za wanyama hao waliopo katika hatari ya kutoweka.
Mwandishi wa habari Julian Rademeyer raia wa Afrika Kusini,amechunguza mtandao mzima wa biashara haramu ya meno ya tembo. Mwandishi huyo anasema katika nchi za Kusini Mashariki mwa Asia kama Vietnam, meno ya tembo yana bei kubwa kuliko dhahabu na dawa za kulevya.
Anabainisha zaidi kuwa biashara hii imejaa tamaa za mali na rushwa ya kiwango cha kutisha na kwamba kuna ushahidi wa namna biashara haramu ya pembe za tembo ilivyotumika kuendeleza vita Msumbiji na Angola kwa nguvu ya Serikali ya Makaburu wa Afrika ya kusini.
Katika kitabu hicho Mwandishi anathibitisha kuwa Meno ya tembo huko Asia hutumika kama mapambo kwa kutengeneza mapambo ya thamani na kwamba meno haya hutumika kama dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume na hivyo kusababisha bei yake kuongezeka.
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika kuhakikisha kuwa tembo waliobakia wananusurika wamependekeza maazimio mbalimbali ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ sasa kutumika kulinda hifadhi,serikali kutangaza rasmi kuwa mauaji ya tembo ni janga la kitaifa pia serikali izuie katika kipindi maalum utalii wa uwindaji.
HABARI KUTOKA:KWANZA JAMII
0 comments :
Post a Comment