Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu
OIC imelaani na kukosoa vikali uamuzi wa serikali ya Angola wa kuipiga
marufuku dini ya Kiislamu nchini humo. OIC imetoa taarifa na kusema
imesikitishwa na kushangazwa na uamuzi wa serikali ya Angola wa kuipiga
marufuku dini ya Kiislamu na kuzitaka jumuiya na taasisi zote duniani
kulaani vikali hatua hiyo. Taarifa ya OIC pia imeutaka Umoja wa Mataifa,
Umoja wa Afrika, nchi zinazozungumza lugha ya Kireno na Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kuchukua msimamo madhubuti wa
kukabiliana na uamuzi huo wa serikali ya Angola. Jumuiya ya Ushirikiano
wa Kiislamu imesema uamuzi wa Angola wa kuipiga marufuku dini ya
Kiislamu unakiuka sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu na uhuru
wa kuabudu. Wizara ya Utamaduni ya Angola imetangaza kuwa dini ya
Kiislamu ni marufuku nchini humo na kwamba sasa serikali hiyo imeamua
kuibomoa misikiti yote nchini humo. Serikali ya Angola imedai kuwa
Uislamu si dini bali ni tapo tu la imani.
Wakati huohuo mtandao wa habari wa Al
Misril Yaum umemnukuu Mkuu wa masuala ya habari wa chama tawala nchini
Angola MPLA akisema kuwa hakuna msikiti wowote utakaofungwa nchini humo.
Ramadhan Shiblolo amesema Uislamu ni moja ya dini muhimu zaidi duniani
na kwamba habari za kufungwa misikiti nchini Angola hazina ukweli. Huku
akiashiria kuwepo misikiti mia moja nchini humo amesema Angola katu
haitoupiga marufuku Uislamu. Katika upande mwengine Sheikh Othman bin
Zaid, Imamu wa msikiti wa Nurul Islam ulioko katika mji mkuu wa Angola
Luanda amesema serikali haijachukua uamuzi wa kufunga misikiti na kwamba
mkuu wa masuala ya kiutamaduni na kidini wa serikali amekanusha habari
za kuchukuliwa uamuzi kama huo. Sheikh Zaid amesema kuna misikiti miwili
iliyobomolewa kutokana na kujengwa katika eneo ambalo halikuwa
limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa misikiti.
CHANZO:IRANI SWAHILI
Blogger Comment
Facebook Comment