MAMA na mtoto, wote wa kazi wa Kijiji cha
Iseche, Kata ya Mwambani, Tarafa ya Kwimba, Wilaya ya Chunya, mkoani
Mbeya, wanatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua
Silvester Chikondo (55).
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa
Polisi mkoani humo, Diwani Athuman, alisema marehemu alishambuliwa kwa
marungu na mama huyo ambaye ni mkewe na mtoto wake.
Alisema tukio hilo limetokea Novemba 12 mwaka huu, saa mbili usiku katika Kijiji cha Iseche, wilayani humo.
Aliongeza
kuwa, marehemu alikutwa na mauti wakati akitoka kilabuni kwenye pombe
za kienyeji ndipo mama huyo akiwa na mwanaye wa kiume, walianza
kumshambulia.
Hata hivyo, Kamanda Athumani alisema marehemu alipigwa
marungu kichwani na kuongeza kuwa, mama huyo anaitwa Husulina Kornel
(42) na mwanaye Kondo Chikondo (19).
Akizungumzia mazingira ya tukio
hilo, alisema marehemu alishambuliwa baada ya kufika nje ya nyumba yake
ambapo chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa kimapenzi.
"Marehemu
alionekana akizungumza na mwanamke kilabuni ndipo mke wake alipoingiwa
na wivu, ugomvi huo ulianzia kilabuni, mke na mwanaye wamekimbia,"
alisema.
Alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kubainika ubongo kuchanganyika na damu hivyo kusababisha kifo chake. Hata
hivyo, Kamanda Athumani ametoa wito kwa jamii hasa wanandoa, kutatua
matatizo yao kwa njia ya mazungumzo si kujichukulia sheria mkononi
kinyume cha sheria.
Alitoa wito kwa watu wenye taarifa za
watuhumiwa, wazitoe ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Pia
amewataka watuhumiwa hao, wajisalimishe wenyewe. MAJIRA
0 comments :
Post a Comment