-->

DR EMMANUEL NCHIMBI AKATWA JINA KWENYE KUGOMBEA UBUNGE SONGEA MJINI




KAMATI ya Siasa ya chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea Mjini imetupilia mbali fomu ya mgombea UBUNGE Dr. Emmanuel Nchimbi kwa madai kuwa fomu hiyo haikuwa na vigezo na kusababisha kushindwa kuijadili baada ya mgombea kutokuwepo kwenye kikao hicho.

Akizungumza asubuhi ya leo ofisini kwake katibu wa CCM wa Wilaya hiyo Juma Mpeli alisema kuwa mpaka jana majira ya saa kumi jioni fomu za kugombea ubunge jimbo la Songea Mjini zilipokelewa tisa (9) lakini fomu moja ya Dr. Nchimbi ilikuwa imechukuliwa na mmoja wa wakazi wa Songea na ikalejeshwa siku hiyo hiyo ikiwa imejazwa.

Alisema kuwa fomu hiyo ya mgombea ilishindikana kujadiliwa kwa kuwa mgombea mwenyewe Dr. Nchimbi hakuwepo kwenye kikao ambacho wagombea wote waliitwa kujadiliwa kadri ya maelezo waliyoyatoa kwenye fomu ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo.

Alieleza zaidi kuwa fomu hiyo iliyoondolewa maelezo yaliyokuwemo imeonyesha wazi kwa ilijazwa na watu wengine na sio mgombea Dr. Nchimbi na jitihada zilifanyika za kuwasiliana naye ili kudhibitisha maelezo yaliyokuwa yameandikwa kwenye fomu hiyo alikataa kuwa yeye alishasema hagombei tena kwenye la Songea mjini licha ya kuwa alijua kuwa kuna baadhi ya wananchi walikuwa na mpango wa kumchangia fedha kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea jimbo hilo.

Kwa upande wake aliyekuwa Mbunge wa Songea mjini Dr. Emmanuel Nchimbi alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu majira ya asubuhi alieleza kuwa kwa sasa hivi yeye yupo jijini Dar es salaam na ameamua kutogombea tena Ubunge kwenye jimbo la Songea mjini licha ya kuwa anaamini kuwa bado wananchi wa Songea mjini walikuwa wanamwitaji

Dr. Nchimbi alitoa ufafanuzi kuwa kuna baadhi ya wazee walikuwa wamemuomba achukue fomu ya kuwania jimbo hilo lakini aliwaambia kuwa kwa sasa hivi hawezi tena kugombea anahitaji kupumzika.

Hata hivyo katibu wa CCM wa Wilaya hiyo Mpeli aliwataja wagombea wa Ubunge wa jimbo la Songea mjini kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama,aliyekuwa waziri wa mazingira na Mbunge wa viti maalumu kupitia vyuo vikuu Dr. Theresa Uviza, katibu wa ccm wa wilaya ya Namtumbo Azizi Mohamed Fakii, aliyekuwa afisa mawasiliano wa Bank ya biashara ya China iliyopo jijini Dar es salaam Mussa Gama, Mkuu wa wilaya ya Mahenge Francis Miti, Mhaziri wa chuo kikuu cha ufundi tawi la Mbeya Erick Mapunda,Sebastian Waryuba mwanasheria ambaye ni wakili wa kujitegemea songea mjini na Raymond Mhenga mkazi wa Jijini Dar es salaam.

Mpeli alisema kuwa wagombea wote nane wanaowania nafasi hiyo juzi jioni waliitwa kwenye kikao cha kamati ya siasa walihojiwa na baadaye walipewa ratiba ya mzunguko wa kampeni ndani ya chama ya ubunge kwenye jimbo la songea mjini ambayo imeanza leo na inatarajiwa kukoma Julai 30 mwaka huu.


Chanzo: Jamvi la Habari
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment