Wazee wa
kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai (Malaigwanan) kutoka Wilaya ya
Monduli wamemuomba waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kubaki na
kuendelea kuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ndicho
kilichomlea na anakijua.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Monduli kwa niaba ya Malaigwanan, Mzee
Joseph Mesopiro kutoka Kata ya Sepeko wilayani humo alisema viongozi wa
mila wanakusudia kutuma ujumbe maalumu kwa Lowassa kumshauri asihame CCM
kama baadhi ya watu aliowaita wapambe wanavyomshauri.
“Sote
Monduli tumesononeka kwa jinsi vikao vya chama vilivyomtendea mbunge
wetu. Bado tunampenda kama ambavyo tunakipenda chama chetu. Tunaamini
ataendelea kubaki CCM na kupigania ushindi wa chama katika uchaguzi
ujao,” alisema Mzee Mesopiro
Alizungumza
hayo wakati wa hafla ya kuchukua fomu na kuomba kuteuliwa na CCM
kugombea ubunge Jimbo la Monduli, mwanasiasa wa siku nyingi Loata
Sanare.
Kwa
upande wake Laigwanan Julius Laizer kutoka Kata ya Moita, alisema licha
ya mizengwe iliyotawala vikao vya uteuzi vya CCM vilivyomalizika mjini
Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha ufa miongoni mwa
viongozi na wanachama, bado anaamini chama hicho kitaendelea kubaki
imara hata kama baadhi ya watu watakihama. “Kama viongozi tuliolelewa
na kukuzwa na CCM, tunaamini chama hiki kitaendelea kuwa imara na hatuko
tayari kukubali ushawishi wowote wa kututaka tuhamie upinzani,” alisema
Laizer.
Mwenyekiti
wa CCM, Kata ya Lepurko wilayani Monduli, Njoput Alami alibeza taarifa
za kushawishi watu kuhama CCM kwa kisingizio Lowassa kukatwa akiziita ni
kelele za wapambe wanaohofia kukosa fursa walizozitarajia iwapo Lowassa
angeteuliwa kuwa mgombea wa CCM.
Akizungumzia
taarifa za wanaCCM wilayani Monduli kughadhabika na kutishia kukihama
chama hicho kutokana na Lowassa kukatwa, Katibu wa CCM Wilaya ya
Monduli, Elisante Kimaro alikiri baadhi ya wanachama kuchana kadi na
kuchoma bendera za chama hicho, lakini akasema ni idadi ndogo
ikilinganishwa na wanachama waliopo wilayani humo.
“Kuna
taarifa za kadi na bendera za CCM kuchomwa moto katika baadhi ya maeneo
kama Migungani, Mto wa Mbu, Makuyuni na Nalaarani. Tunaendelea kukusanya
taarifa sahihi na kufanya tathmini ya matukio hayo,” alisema Kimaro
0 comments :
Post a Comment