Mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge kupitia viti maalum katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) unadaiwa kutawaliwa na hongo.
Habari kutoka vyanzo vyetu mbalimbali ndani ya CCM na Jumuiya zake
zinaeleza kuwa kuna baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge wanaoshikilia
nafasi hizo ambao wanamwaga kiasi kikubwa cha fedha kuwahonga wajumbe wa
vikao mbalimbali kuanzia kata, wilaya na mikoa watakaopiga kura.
Mbali na kumwaga kiasi kikubwa cha fedha kwa wajumbe, pia wanadaiwa
kuwahonga watendaji ambao wanawatumia kuwaandalia mikutano isiyo rasmi
kwa ajili ya kukutana na wapigakura.
Malalamiko mengi ya kumwagwa hongo kwa ajili ya kupata viti maalum
yanauhusu Mkoa wa Dar es Salaam ambao vigogo kadhaa wamejitosa kwa ajili
ya kusaka nafasi hizo.
Vigogo watatu (majina tunayahifadhi) wanaowania nafasi hizo ndio wanaolalamikiwa zaidi kwa kufuru ya hongo.
Chanzo kimoja kimeeleza kuwa kuna kigogo mmoja mwenye ukwasi mkubwa
ambaye anakata dau kubwa kuwashawishi wapigakura na kwamba kwa sasa
anatoa hadi Sh. 200,000 kwa kila mjumbe.
“Yaani nakwambia sasa hivi napiga raundi ya tatu mkoani. Kuna wajumbe
kama 300 hivi, kila mmoja mara ya kwanza aliwatoa Sh. 150,000, lakini
juzi hapa baada ya Bunge kuvunjwa ameibuka na anatembeza Sh. 200,000,”
alilalamika mwanachama wa UWT
Mwanachama huyo aliyeomba kutokutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama,
alisema kuwa kwa mwelekeo wa sasa ndani ya CCM ni miujiza kama mtu hana
fedha za hongo, kuchaguliwa.
“Yaani ukifika kwenye ofisa za kata kama hujatoa fedha, hakuna
anayekusikiliza. Akija aliyetoa fedha utashangaa anavyoshangiliwa.
Jamani CCM imefika hapa kweli,” alilalamika.
Mwanchama mwingine alisema kuwa hali hiyo kama haitadhibitiwa wananchi wasahau kupata viongozi wanawakilisha shida zao.
“Kama mtu ananunua wajumbe unafikiri akipata huo ubunge atawakumbuka
waliomuuzia kura. Hii ni biashara ya kura. Inauma kweli,” alilalamika
mwanamama huyo anayetoka Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Licha ya kuwapo madai hayo, viongozi wa chama hicho wanasema hawana taarifa kuhusu vitendo vya hongo miongoni mwa wagombea.
Katibu Msaidizi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama hicho Mkoa
wa Dar es Salaam, Kibure Dilawa, alipoulizwa jana, alisema kwa ufupi
kuwa hawana taarifa.
Alisema kinachoendelea ni kuwa wanaendelea kupokea majina ya wagombea
ubunge wa Viti Maalum kutoka kwa makatibu wa wilaya na kwamba idadi ya
wagombea waliyonayo ni 35.
“Tunasubiri kufanya kikao cha pamoja leo (jana) mchana ili kupanga ratiba ya kampeni, lakini tutaanza Julai 26,” alisema.
SOURCE:UKWELI MTUPU
0 comments :
Post a Comment