Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya akizungumza, Dar es Salaam jana kuhusu vikao vya Baraza Kuu la uongozi wa chama hicho kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kumsimamisha mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Kulia ni Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya. Picha na Venance Nestory
Na Hussein Issa
Posted Alhamisi, Julai 16, 2015 (9:24am)
Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), limeutaka uongozi wa chama hicho kusitisha uamuzi wa kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyama vinavyounda Ukawa hadi suala hilo litakapojadiliwa kikatiba ndani ya chama hicho Julai 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye uamuzi wa kutoa tamko la kuendelea kuwamo ndani ya Ukawa au kujitoa.
Taarifa hizo za CUF zinakwenda tofauti na taarifa iliyotolewa juzi na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia kwamba wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye atatangazwa kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo, alisema hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Hata hivyo, jana Sakaya alisema: ”Hili la kujiunga na Ukawa linatakiwa kujadiliwa kwa kina na Baraza Kuu na hata ikiwezekana kuwashirikisha na wanachama ndipo mwafaka wa kujiunga au la utolewe.”
Alisema hata baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza mbele ya viongozi wa Ukawa kwamba juzi wangemtangaza mgombea wa urais lilikuwa ni kosa kwani liliwashtua wajumbe wa Baraza Kuu kwa kuwa hawakushirikishwa.
Alisema kutokana na katiba ya chama hicho, hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kutangaza jambo kama hilo hadharani bila ya kushirikisha Baraza Kuu ili litoe baraka zake.
Alisema jambo jingine ambalo liliwashtua wajumbe wa baraza hilo na wanachama wao ni baada ya kusikia taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba tayari mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Ukawa ameshapatikana.
“Ni jambo la kushangaza kwani mpaka idadi ya kura ambazo mgombea huyo kupitia chama fulani alizozipata zimewekwa hadharani kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, suala hili lilitushtua sisi viongozi na hata wajumbe wa baraza Kuu hivyo tumeona tulijadili kwanza,” alisema.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge wa CUF, Shaweji Mketo alisema ni muhimu Watanzania wakatambua kwamba CUF haijajitoa Ukawa, bali ni mchakato tu unaoendelea kwa mujibu wa sheria ya chama hicho.
Alisema nchi inapitia kipindi kigumu na pia ongezeko la majimbo 26 ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa kampeni, ni changamoto kubwa kwa Ukawa.
Alisema CUF ina imani kwamba kwa maridhiano ya pamoja, Ukawa itajengwa imara na hatimaye kuwa na mgombea mmoja wa urais, wabunge na madiwani.
Mbowe atoa ufafanuzi
Akizungumzia msimamo huo wa CUF, Freeman Mbowe alisema wamewaelewa vizuri wenzao na kwamba masuala ya chama yanasimamiwa na viongozi, hivyo ni lazima wayamalize kwa mchakato wao ndani ya chama ndipo wajihakikishie ushiriki wao.
“Kuhusu hoja ya CUF kusikiliza Baraza lao Kuu kwanza ni suala la msingi sana na wameshatwambia na tumewaelewa kwa sababu hata sisi tulipata baraka zote ndani ya baraza ndiyo maana tukaamua kushiriki kikamilifu,’’ alisema.
Alisema ana imani kwamba CUF, itashiriki kikamilifu kwenye Ukawa kuhakikisha wanampata mgombea mmoja kama walivyowaahidi wananchi.
“Wananchi wanatuamini sasa lazima haya mambo tuyafanye kwa umakini sana ili tusije tukajiharibia sifa na kuambulia aibu kutoka kwa wananchi ambao wana imani na sisi,’’ alisema.
Mwananchi: CUF yaiweka Ukawa pagumu
0 comments :
Post a Comment