Gor
Mahia imekuwa timu ya kwanza kutinga kwenye hatua ya robo fainali
kwenye michuano ya Kagame Cup baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo
yake miwili kwenye Kundi A, kundi pekee lenye timu tano kwenye michuano
ya Kagame. Gor Mahia waliibuka na ushindi wa goli 2-1 kwenye mchezo wao
wa ufunguzi kwa kuifunga Yanga na leo wameitwanga KMKM goli 3-1 na
kuongoza Kundi A kwa kuwa na pointi sita huku wakiwa wamefunga magoli
matano wakati wao wamefungwa magoli mawili.
Mshambuliaji
wa Kenya Michael Olunga amezidi kung’ara kwenye michuano ya Kagame Cup
baada ya kufunga magoli mawili kwenye mchezo wa leo uliopigwa kwenye
uwanja wa Taifa kati ya KMKM ya Zanzibar dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Gor
Mahia ndio walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa Kagere Medie
dakika ya tatu kipindi cha kwanza lakini goli hilo lilisawazishwa na
Mateo Antony Saimon dakika ya 11 na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko
zikiwa sare kwa kufungana goli 1-1.
Kipindi
cha pili KMKM ilishindwa kuhimili kasi ya Gor Mahia kwani dakika ya 69
Michael Olunga aliifungia Gor Mahia goli la pili, wakati KMKM wakiwa
katika harakati za kuhakikisha wanasawazisha goli hilo Olunga tena
akarejea kambani na kuiandikia Gor Mahia goli la tatu na la ushindi kwa
upande wa Gor Mahia.
KMKM ilijitahidi kucheza vizuri
kipindi chote cha kwanza lakini makosa madogomadogo yaliwakosesha
ushindi. Walijitahidi kutengeneza nafasi za kufunga lakini walishindwa
kuzitumia nafasi hizo kupata mabao. Licha ya kupiga mpira mwingi leo,
Juma Mbwana Faki alikosa goli akiwa amebaki yeye na kipa, Mateo Saimon
na yeye pia alipoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Mbali na kukubali kichapo hicho
cha magoli matu, KMKM ilionesha mpira mzuri hasa kipindi cha kwanza na
kuwapa matumaini wadau wengi wa soka la Tanzania huenda wakaweza
kuutafuna mfupa uliomshinda Yanga lakini kipindi cha pili mambo
yalibadilika na kujikuta wakiruhusu magoli mawili.
Olunga mpaka sasa ameshafunga
magoli matatu baada ya kucheza mechi mbili. Mchezo wa kwanza alifunga
goli moja wakati timu yake ikicheza dhidi ya Yanga na leo ametupia
kambani goli mbili na kuipeleka timu yake kwenye hatua ya robo fainali
ya michuano hiyo.
Mchezo uliotangulia (saa 8:00
mchana), Khartoum ya Sudan iliibuka na ushindi wa kishindo kwa
kuicharaza Telecom ya Djibouti kwa goli 5-0.
0 comments :
Post a Comment