Miaka mitatu sasa, Simba haijafuzu kushiriki michuano ya kimataifa
inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hiyo haimsumbui
straika mpya aliyerejea kikosini, Mussa Mgosi ambaye amewataka mashabiki
kutulia kwani hali hiyo itarejea ndani ya msimu huu.
Mgosi aliyejiunga na Simba siku chache zilizopita baada ya kumaliza
mkataba na Mtibwa Sugar, amesema: “Heshima iliyopotea Simba, sasa
itarudi.”
Alisema kwa kushirikiana na wenzake, atahakikisha msimu ujao
watafanya kila liwezekanalo ili Simba kama siyo kutwaa ubingwa basi
ishike nafasi ya pili na kukata tiketi ya kucheza michuano ya Caf.
“Nimetoa kauli hiyo kwa kuzingatia usajili uliofanywa kwa maana wale
tunaojiunga na timu tukishirikiana na wenzetu tuliowakuta hapo tutakuwa
na timu bora,” alisema Mgosi.
“Sasa ndiyo muda wa Simba kurudisha heshima yake kama zamani kwani
imedharaulika kwa muda mrefu lakini napenda kusema msimu uliopita ndiyo
ulikuwa mwisho wa dharau hizo.”
Mbali na Mgosi, wachezaji wengine waliosajiliwa na Simba hadi sasa ni
kiungo Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City, Mohammed Fakhi (KMKM), Samih
Ali Nuhu (Azam FC), Laudit Mavugo na Nimubona Emiry (Vital’O) na kiungo
Emmanuel Ntinde kutoka Burkina Faso ya Morogoro.
0 comments :
Post a Comment