-->

JULIUS MTATIRO:TUANZE KWANZA KUFUTA “GREEN GUARD!”


Kichwa cha habari cha makala hii kinaweza kuwashtua watu wengi. Nimekiandika hivi kuakisi hali halisi ya hoja nayotaka kuijenga hapa chini.
Wengi wetu tumekuwa tukisikia majina ya vikundi maarufu sana vya kiulinzi vinavyosimamiwa na vyama vikubwa vya siasa hapa Tanzania. Chama Cha Mapinduzi CCM kina kikundi chake kinachoitwa “Green Guard”, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kina kikundi chake kiitwacho “Red Guard”, na Chama cha Wananchi CUF kikundi chake kinaitwa “Blue Guard”.
Vikundi hivi vya vyama huwa vinapewa majina yanayoendana na nembo au rangi za bendera za vyama vyao na sote tunafahamu kuwa rangi za bendera mahali kote duniani huongelea au humaanisha jambo fulani hivi ambalo lazima lina maana kubwa tu kwa chama hicho, hata hivyo mjadala wa rangi hizo siyo lengo la andiko langu.
Najadili hoja hii kwa sababu hivi karibuni, viongozi wa Jeshi la Polisi wamesisitiza kuwa watapiga marufuku vikundi vya ulinzi katika vyama, hata Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ameliongea jambo hili mara kadhaa akiungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi na wadau wengine wengi.
Mchambuzi mmoja na mwanahabari wa siku nyingi ambaye nimekuwa nikifuatilia sana uandishi wake mzuri, Maggid Mjengwa, naye amekuwa akilikomalia sana suala hili la vikundi vya ulinzi katika vyama. Hoja wanazozijenga ni nzuri lakini kwa mtizamo wangu hazitekelezeki kirahisi!
Lazima tukubaliane kuwa dhana ya ufutaji wa vikundi vya ulinzi katika vyama inawezekana kabisa, ni kiasi tu cha serikali kuamua kuwa kuanzia sasa vikundi hivi havitaruhusiwa kuwepo na mimi ntakubaliana sana na uamuzi huu wa serikali, ikiwa kwanza kikundi cha kwanza kufutwa ni “Green Guard” cha CCM.
Wakati serikali inalalamikia vikundi vya ulinzi katika vyama inasahau kuwa wakati vyama vinasajiliwa hapakuwepo na vikundi hivi. Serikali inasahau kuwa manyanyaso na hujuma zisizofuata taratibu za kisheria pamoja na matendo ya ajabu ambayo serikali imewahi kuwafanyia viongozi wa vyama vya upinzani ndiyo yalipelekea kukawa na mawazo ya kuanzisha vikundi vya ulinzi vyenye vijana wakakamavu wasiotumia silaha na ambao watawalinda viongozi wa chama husika dhidi ya hujuma zozote ambazo wanaweza kutendewa na mahasimu wao.
Lakini hata wakati vyama vya upinzani vinaanzisha vikundi vya ulinzi kwa ajili ya kujilinda, tayari CCM ilikuwa na vikundi vya vijana ambao huwatumia kwa ajili ya ulinzi. Mimi zamani nikiwa shule ya Msingi na Sekondari nilikuwa mshiriki mzuri wa “SCOUT”.
SCOUT ilichukuliwa kama jukwaa muhimu la kuwapa vijana wadogo uimara wa fikra na mwili, tulipelekwa kwenye mapori mbalimbali na kufundishwa ukakamavu, lakini nakumbuka nikiwa Shule ya Sekondari Musoma Kutwa, tulipomaliza mafunzo ya tatu ya U-Scout, alikuja Mshauri wa Mgambo pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ili kushawishi vijana wachukue kadi za CCM, mimi nilikataa.
Tulishawishiwa kwamba kujiunga CCM huku tukiwa na vyeti vya SCOUT kutatufanya tuhesabiwe kama walinzi wa chama hicho wa viongozi na mali za chama, rafiki zangu wengi walijiunga. Lakini pia CCM imekuwa na vikundi vingi vya Chipukizi za watoto ambazo baadaye pia hubadilishwa na kuwa “Green Guard”. CCM haiwezi kuachana na mfumo huu kwa sababu vijana wa Green Guarad wanatoa msaada mkubwa sana kwa chama hicho na misaada mingine siyo hata mizuri kuitaja kimaadili.
Na kama CCM haiwezi kuachana na “Green Guard” sielewi serikali hii hii ya CCM inapata wapi ujasiri wa kuonya uwepo wa vikundi vya ulinzi katika vyama. Uongozi ni kuongoza huku umetangulia siyo umekaa nyuma. Kama kweli IGP na wengine wote wanaojenga hoja za kutaka vikundi vya ulinzi katika vyama viondolewe, lazima CCM ioneshe mfano, ioneshe kuwa watanzania wanaweza kabisa kuendesha siasa bila kutumia vikundi vya ulinzi vya ndani ya vyama.
CCM ikishavunja ‘Green Guard” yake, serikali itakuwa na jukumu la kuwezesha jeshi la polisi lifike kwenye matukio kwa haraka sana na ama liwepo katika matukio yote ya kisiasa ili kuwalinda viongozi wa vyama vya siasa na mali za vyama hivyo.
Ikiwa Serikali na CCM vitatekeleza mambo hayo mawili, mimi binafsi ntaungana na gwiji wa habari, Maggid Mjengwa ili tupigane vikundi vyote katika vyama vifutwe mara moja, maana vitakuwa vimeishiwa kazi ya kufanya. Lakini ikiwa IGP na viongozi wengine wanalalamikia vikundi hivi kwa maneno, huku CCM ikiendeleza kusaka vijana wapya wa ‘Green Guard’, inakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Kwa sababu vikundi hivi havina silaha, na uwepo wao hauvunji katiba wala sheria na tena uwepo wa vikundi hivi haujaathiri wala kusumbua dhana ya “majeshi ya ulinzi” katika nchi, sioni sababu yoyote ya kuvipiga vita. Na kama ni lazima kuvipiga vita, hebu IGP na viongozi wengine wa majeshi waanze kupiga vita “Green Guard” hadi ifutike.
Hivi karibuni wakati Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA anakagua vikundi vyake vya Ulinzi katika Mkutano wa Halima Mdee (Mbunge) uliofanyika kwenye viwanja wa Tanganyika Packers, Kawe – mdau mmoja alinipigia simu akishangazwa sana na tukio lile, akaliita ni kama “kupindua nchi”, nikacheka sana lakini nikamjibu kwa kumtumia kipande cha video kikionesha Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, pia akikagua Gwaride la Heshima la vijana wa Green Guard. Yule ndugu yangu hakujibu ujumbe wangu tena na nilipompigia aliniambia amenielewa sana.
Dawa ya maji ni moto na dawa ya kufuta vikundi vya ulinzi katika vyama ni kuanza na CCM.
(Julius Mtatiro +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment