UTANGULIZI:
Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,
Hii ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua
kuwaita ili kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka
kuomba ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze
kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nasema hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini
historia yangu itainakili kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika
maisha yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama
chetu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza
wa vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya
Kikwete; wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja
kuchukua fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja
na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo
ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote
atakayepita kati ya wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa
angemuunga mkono.
Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa
dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete. Nikiwa
Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa
wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia
80 wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na
kwa nini naamini mimi ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati
huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku
muhimu kwangu.
Lakini nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema
hivyokwa sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa
Taifa letu wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania
kujenga taifa imara. Na hili pia nitalieleza kwa kina.
HALI YA NCHI NA MATARAJIO YA WATU:
Miaka 48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa
huru kiuchumi na kupiga vita maadui umaskini, ujinga na maradhi
kwakutumia silaha ya kujitegemea. Leo hii, wakati taifa likijiandaa kwa
Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna budi kutafakari tulikotoka, tulipo na
tunapotaka kwenda ili tuweze kubuni upya mikakati ya kuhitimisha azma
aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili tujenge taifa huru, lenye utulivu,
mshikamano, amani na maendeleo.
Nchi yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito
katika maeneo yote makuu ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi
na katika maisha ya kijamii.
Kisiasa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa
vyama vingi ambapo ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali
na kwa bahati mbaya kufikia sura ya kuonekana kama vile ni mapambano ya
watu binafsi badala ya mapambano ya sera na dira ya kuongoza nchi.
Tunashuhudia kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama
kimoja kimoja na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya
kingine. Kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa
kuendelea nchi yetu inaweza kujikuta mahali pabaya. Kukua kwa ushindani
ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu na tukiwa na
ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko mema kwa
wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii katika nchi yetu. Kinyume chake ushindani unaochukua sura ya
chuki binafsi au kukomoana na hata kulipizana visasi si ushindani wenye
tija na tunapaswa kuutafutia tiba. Tunahitaji uongozi imara kusimamia
kipindi cha mpito kutoka siasa muflisi za aina hii na kuelekea kwenye
siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija unaojikita katika
kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania.
Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa
mapato ya ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na
ulipaji kodi. Kwa upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na
Rais Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya
mafuta na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia
kimegunduliwa. Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia
uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja
kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania. Hata hivyo, kipindi hiki cha
mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa kimeshuhudia kuongezeka kwa
hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi kwamba hawatonufaika naukuaji huu
wa uchumi na ugunduzi wa utajiri mkubwa wa gesi asilia. Kwa upande
mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri
huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze
kukabiliana na changamoto za maisha yao. Niliwahi kusema kwamba tatizo
la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi imara ni bomu
linalosubiri kulipuka. Vijana wasio na ajira hupoteza matumaini na ni
rahisi kughilibiwa kuingiza nchi katika machafuko.Tunahitaji
uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia
suluhisho maridhawa.
Kijamii, kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko
makubwa ya tabia miongoni mwa raia katika hali ambayo haijawahi kuwa
sehemu ya utamaduni wa Watanzania. Kumekuwa na ongezeko la kutisha la
matukio ya uhalifu linalokwenda sambamba na wananchi kuonyesha
wanapoteza imani na taasisi zinazosimamia sheria na usalama na kuamua
kujichukulia sheria mikononi mwao. Kumeripotiwa matukio mengi yakiwemo
ya kuvamiwa vituo vya polisi, askari kupigwa na kuporwa silaha, matumizi
makubwa ya nguvu katika utatuzi wa migogoro mbalimbali hasa ile ya
kijamii, mathalani migogoro ya wakulima na wafugaji, mivutano ya kidini
na pia mivutano baina ya viongozi wa dini wenyewe kwa wenyewe na baina
ya viongozi wa dini na wale wa Serikali. Matokeo yakemshikamano wa taifa
nao unaingia majaribuni. Mara nyingine wananchi wanatuuliza
viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa na waasisi wetu. Tunahitaji
uongozi imara wa kukabiliana na changamoto hizi na kurudisha mshikamano
wa taifa letu na watu wake.
WATANZANIA WANATAKA MABADILIKO:
Ndugu zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote
hayo na yana mahusiano gani na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka
kuiongoza nchi yetu kupitia CCM?
Nimeyaeleza haya kwa sababu haya na matukio mengine
yanayoendelea nchini yamepelekea Watanzania kutaka mabadiliko.
Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda changamoto
hizi na kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake
anaishi akiwa na uhakika wa mahitaji yake muhimu na papo hapo
akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake
itakuwa bora zaidi kuliko leo yake. Kwa maneno mengine, Watanzania
wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara unaoweza kuwaongoza
kujenga taifaimara. Hii ndio Safari ya Matumaini.
Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi
wake, TANU na ASP, kimepata bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea
enzi za kupigania uhuru, wakati wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya
Zanzibar, na pia miaka yote tokea Uhuru, Mapinduzi na hatimaye Muungano
wetu. Watanzania hawajawahi kushuhudia chama kingine kikiongoza Serikali
zetu zaidi ya CCM. Wamekiamini na wanaendelea kukiamini. Hata katika
yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo hatukufanya vizuri katika
uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si kwamba watu wa maeneo hayo
wana matatizo na CCM kama Chama bali wana matatizo na baadhi ya viongozi
ambao walishindwa kukiwakilisha vyema Chama na kutambua matakwa ya
wananchi hao.
Mimi naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo
Watanzania wanaonekana kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba
watayapata mabadiliko hayo ndani ya CCM. Lakini kama alivyotupa wasia
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi
mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Watanzania
wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Mimi
naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko
wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli
kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya
kujenga taifa imara.
Vyama vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu.
Moja ya hulka ya binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya
mazingira anayoishi. Kwa maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa
sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’. CCM
haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa zaidi ya miongo
mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na
mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati
husika. Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa
mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili. Tanzania
imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo wetu wa siasa
kutoka ule wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya kubadili mwelekeo
wa uchumi wetu kutoka ule wa dola kumiliki njia zote kuu za uchumi kuja
katika uchumi wa soko unaozingatia ushiriki mpana wa Watanzania wa
matabaka yote; na hata karibuni kabisa katika mchakato wa kuipatia nchi
yetu Katiba mpya.Tanzania tumeweza kufanya mabadiliko ya uongozi mara
nne katika hali ya amani na maelewano, jambo ambalo nchi nyingi za
Afrika zimeshindwa. Ni imani yangu kwamba tukijikubalisha tunaweza tena
kuwapa Watanzania wanachokitaka katika zama hizi za sasa. Lakini ni
lazima tuoneshe dhamira hiyo kwa dhati ili, kama alivyotuasa Mwalimu
Nyerere, Watanzania wasiyatafute mabadiliko hayo nje ya CCM. Nasisitiza
tena kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka,
lakini pia wananchi wana hiali kuchagua mabadiliko wanayoyataka.
UONGOZI UNAOHITAJIKA KULETA MABADILIKO YANAYOTAKIWA:
Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi
chake na kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba
zake za karibuni ni kwamba yeye ametekeleza wajibu wake kwa kuweka
misingi imara ya ujenzi wa Taifa la kisasa lenye uchumi madhubuti na
unaoweza kukua kwa kasi. Amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa
nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale atakapoachia.
Kwa maoni yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
- Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;
- Uongozi thabiti na usioyumba;
- Uongozi makini na mahiri;
- Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
- Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;
- Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
- Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:
- Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);
- Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa
Tanzania na kukuza pato la Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato
kati ya aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;
- Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
- Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
- Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
- Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;
- Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
- Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara
UONGOZI IMARA, TAIFA IMARA:
Naamini kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya
Urais si kazi ya lelemama na unahitaji utashi. Kabla hata ya kutakiwa na
wenzako ni lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio
kwamba unao uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako. Na katika hilo, rekodi
yako ni lazima izungumze na kulithibitisha hilo.
Binafsi nina hazina ya uzoefu na rekodi njema ya matokeo ya
kazi nilizozifanya katika uongozi na utumishi wa umma ndani ya CCM na
ndani ya Serikali. Nilianza kazi nikiwa Katibu Msaidizi wa CCM
katika mikoa ya Shinyanga, Arusha na Moshi. Nimekuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya CCM. Niliingia Bungeni mwaka
1985 na baadae mzee wangu, Rais Ali Hassan Mwinyi, akaniamini kwa
kuniteua kuwa Waziri. Nimekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Waziri wa Ardhi, Makaazi na Maendeleo ya Miji, Waziri wa Mazingira,
Waziri wa Maji na hatimaye Waziri Mkuu.
Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na
utumishi wangu, na ambayo Watanzania wanayatambua na naamini
wanayathamini, ni pamoja na:
- Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais
Mkapa,tulithubutu kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na
makubaliano yaliyowekwa na wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi
zilizopakana na Ziwa Victoria zisiweze kufaidika ipasavyo na maji ya
Ziwa hilo. Leo hii ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanafaidika na ujasiri
wetu katika kukabiliana na suala hilo zito.
- Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi
kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu
na kuwachukulia hatua waliochafua na kuharibu mazingira.
- Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la
Rais Kikwete na kufanikisha utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa
kujenga shule nyingi za sekondari kuliko wakati mwingine wowote tokea
Uhuru.
- Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete
la kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa
wakati. Leo hii Chuo Kikuu hicho ni fahari ya Tanzania.
Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima
tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha
Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.
Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana
hizo nzito. Katika mambo ambayo najivunia na sitoyasahau katika historia
yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yangu pale ilipohitajika.
Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni askari wa
mstari wa mbele wa mapambano. Nikiwa Mbunge nilipata heshima ya kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naamini Watanzania hawatakuwa
na wasiwasi wa usalama wao nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.
Nimeeleza uzoefu wangu kwenye Chama na huo hauhitaji
maelezo zaidi. Ninakijua vyema Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kutosha
kabisa kukiongoza kama Mwenyekiti wake pale wakati utakapofika. Wana-CCM
wanajua nikikabidhiwa uongozi, Chama chetu kitakuwa chini ya nahodha
madhubuti, mzoefu na asiyeyumba.
Kutokana na rekodi yangu hii, naamini ninazo sifa za
kuwaongoza Watanzania wenzangu katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la
kisasa lenye watu wazalendo walioshikamana na lenye uchumi
imara unaomnufaisha kila Mtanzania. Naamini ninao uwezo wa kuwapa
Watanzania Uongozi imara kwa ajili ya ujenzi wa Taifa Imara.
DIRA YANGU NA MATARAJIO YA WATANZANIA:
Mfumo tuliojiwekea hapa nchini unaelekeza kila chama cha
siasa kinachosimamisha mgombea Urais na kinachowania kuongoza nchi yetu
kuja na Ilani ya Uchaguzi ambayo ndiyo inayoweka misingi ya sera
zitakazofuatwa na Serikali itakayoongozwa na chama hicho pale kinapopewa
ridhaa ya kuongoza nchi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni cha
kupigiwa mfano katika kutayarisha Ilani bora na ndiyo maana mara zote
kimepewa ridhaa ya kuongoza nchi yetu. Tumefanya hivyo tokea enzi za
mfumo wa chama kimoja na tumeendelea kufanya vizuri katika mfumo wa
kushindanisha sera kupitia vyama vingi. Najua kwamba Ilani ya CCM ya
mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za kukamilishwa na itakapopata
baraka za vikao vya Chama itakuwa ndiyo msingi wa utendaji wa Serikali
ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba mwaka huu. Hata hivyo, naamini
pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa ya Chama na ya Watanzania
kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira yake.
Mimi, baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo
na matarajio na matumaini waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi
imara unaolenga kujenga Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo
yafuatayo:
- Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia
yanayotutenganisha na kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale
yanayotuunganisha ambayo ni mengi zaidi na makubwa zaidi.
- Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na
ukabila kwa kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza
kwenye Utanzania wetu.
- Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni
shirikishi unaomnufaisha kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini.
Tunapaswa kubadili hali tuliyo nayo sasa ambapo Kilimo kinaonekana kama
kimesahauliwa na wakulima wetu wanaonekana wanakata tamaa.Wafugaji na
wavuvi nao wanahisi sekta zao hazijapewa umuhimu unaostahiki. Tunahitaji
kuondokana na hali iliyopo sasa ya kuwa Taifa linalouza malighafi na
badala yake kuwa Taifa linalosindika na kusarifu mazao na kutengeneza
wenyewe bidhaa zitokanazo na malighafi yake. Ndani ya miaka mitano ijayo
tutahakikishatunaiondolea Tanzania sifa ya kusafirisha malighafi na
badala yake kusindika mazao yanayozalishwa hapa nchini kama pamba,
kahawa, chai na korosho na kuyaongezea thamani (value addition).Mkakati
huu utazalisha ajira nyingi na kuongeza mapato ya fedha za kigeni
nchini. Tunahitaji kujielekeza kwenye kujenga viwanda na kuleta
ajira. Tuna vivutio vingi sana vya utalii lakini bado Tanzania inapitwa
na nchi kama Afrika Kusini katika kuingiza idadi kubwa ya watalii. Kwa
nini nchi kama Dubai iweze kuvutia watalii kwa mamilioni na Tanzania
tushindwe? Tunapaswa kukabiliana kikamilifu na hisia zilizopo miongoni
mwa wananchi kwamba Tanzania hainufaiki ipasavyo na utajiri wa
rasilimali zake nyingi ilizo nazo. Tutajipanga zaidi kuhakikisha
tunanufaika kama nchi na rasilimali zetu kama madini na gesi asilia. Hii
ndio Safari ya Matumaini
- Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha
ya watu wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi
tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na
kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba
wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia.
- Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa
wingi wa rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na
bahari Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na
badala yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika.We can transform our
nation from being the begging bowl to become the bread basket of Africa.
- Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza
kuwatayarisha vijana wetu waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana
katika soko la ajira. Tumepiga hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango
cha elimu bado ni hafifu. Pamoja na kuwa na shahada (degrees), bado
wahitimu wetu hawawezi kushindana kwenye soko la ajira. Wakati
tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki,hatuna
budi kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo
ya ufundi na stadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu na wenye
kujiamini katika kukabiliana na changamoto za maendeleo duniani.
- Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa
kiasi kikubwa kama si kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji
safi na salama. Ni jambo la kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na
maziwa lakini bado watu wetu hawana maji ya kunywa hata ndani ya Dar es
Salaam.
- Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na
sheria tunazozitunga na kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania
na kumjengea uwezo wa kubadili maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na
viwango vya kimataifa. Tanzania imepata sera na sheria nzuri sana
lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera
na sheria lakini wazito mno wa kuzitekeleza na kuzisimamia. Uongozi
imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa imara utahakikisha tunakuwa mfano wa
utekelezaji wa sera na sheria tulizo nazo na mpya zitakazotungwa
kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.
Mambo haya niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi
mkuu wa utendaji wa Serikali nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya
kubeba bendera ya CCM katika nafasi ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa
ya kuliongoza Taifa letu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
RAMANI YA UONGOZI IMARA NINAOUAMINI (LEADERSHIP ROADMAP):
Kama nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si
lelemama na hasa unapoongozwa na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya
nafsi unaojielekeza kubadilisha maisha ya wananchi wenzako waliokuamini
uwaongoze. Kwa vyovyote vile, hiyo haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni
kazi ya pamoja. Lakini ili muweze kufanya kazi kama timu moja
iliyojipanga kisawasawa kuleta mabadiliko yanayohitajika na ili muweze
kweli kutoa Uongozi imara unaojikita kujenga Taifa imara hapana budi
kiongozi mkuu anayeongoza timu hiyo aweke ramani anayokusudia kuifuata
katika kutoa uongoziimara anaoukusudia yaani ‘Leadership Roadmap’.
Pamoja na kuwa sehemu ya uongozi huko nyuma, kutakuwa na
maamuzi na matumaini mapya. Ramani ya uongozi imaraninayokusudia kuutoa
kwa wenzangu na ambayo nitaitumia kuiongoza timu yangu katika
kuwatumikia Watanzania wenzangu itajikita katika maeneo yafuatayo:
1. Kurejea kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na
malengo yetu ya kujenga jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu
na amani. Muhimu katika hili ni kukemea tabia mbaya zinazochochea
mfarakano katika jamii kama vile matumizi mabaya ya siasa za udini na
ukabila. Aidha moja ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano
wetu. Itakuwa dhamira yangu kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na
udugu wa damu nahistoria ya ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu,
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amri
Abeid Karume na kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
2. Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua
azma ya kujitegemea kama Taifa. Ni dhahiri kuwa pamoja na rasilimali
zetu, bado Tanzania ni taifa tegemezi. Bado tunajidanganya kuwa
wafadhili watatujengea nchi. Tukumbuke, nchi zinajengwa nawananchi wake.
Nasi pia lazima tujikomboe kifkra na tuondokane na utamaduni wa
kuwa tegemezi. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza
kujitegemea na kuijenga Tanzania sisi wenyewe.Kujiamini na
kujitegemea ndio uhuru wa kweli.
3. Kujenga uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha
uwazi katika shughuli zote za serikali na kupambana na
rushwa.Watanzania tumepoteza uzalendo kwa kiasi kikubwa. Kuna vitendo
vinavyoashiria kuwa hatuipendi tena nchi yetu. Tunashabikia wizi
na rushwa. Inabidi turejee kwenye misingi ya taifa letu misingi ya
uadilifu na uzalendo. Tukumbuke kuwa hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa
kama tutaruhusu rushwa ishamiri. Wawekezaji hawataleta mitaji yao kwa
wingi kama rushwa itaendelea kutawala katika huduma serikali na wananchi
hawawezi kupata huduma bora kama rushwa itaendelea kutawala. Ni
lazima tuipinge rushwa kwa vitendo sio maneno.
4. Kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu
inayoendeshwa kwa misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji.Maendeleo ya
watu hayawezekani bila serikali kusimamiautekelezaji sera na miradi na
kuleta ufanisi katika kutoa huduma na kusimamia maendeleo. Tumekuwa
wepesi wa kutunga sera lakini wazito wa kuzitekeleza na kuzisimamia.
5. Kuleta msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali
na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa kisasa na
unaojitegemea. Sekta binafsi ndiyo nyenzo ya uchumi
imara. Inazalisha mali, ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato
la taifa kwa kulipa kodi. Ilisekta hii itoe mchango unaotakiwa katika
maendeleo ni lazima ifanye kazi na serikali kwa karibu. Tukumbuke, bila
uchumi imarahakuna huduma bora!
6. Uwekezaji katika huduma za jamii. Elimu na afya bora,
mazingira, makazi safi na maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya
watu. Hii inawezekana tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa
kuutambua uboreshaji wa huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu
la maendeleo ya nchi. Serikali nitayoiongoza itahakikisha kuwa kila
Mtanzania anapata elimu bora na inayogharamiwa na serikali kama mimi na
wenzangu tulivyopata. Wakatitunazungumzia kuunganisha soko la ajira
katika Afrika Mashariki, hatuna budi kurekebisha mfumo wetu wa elimu na
kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na ustadi yanayowajenga wahitimu
wetu kuwa wabunifu, wenye kujiamini, wenye uwezo kushindana katika soko
la ajira na wa kujiajiri. Napenda kusisitiza kuwa elimu ndiyo muhimili
wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa kweli wa binadamu. Mimi ni mfano hai
wa ukombozi wa elimu. Elimu ndiyoimenivusha kutoka kijijini kwetu
Ngarash na kunipa upeo wa kitaifa. Mama akiwa na elimu atajua umuhimu wa
kumpeleka mwanae shule, anapata lishe bora na chanjo stahili na
kuwa anaishi katika mazingira safi. Elimu ndilo jibu la umaskini,
maradhi na ujinga.Taifa lililo elimika ni taifa lenye maendeleo.
7. Kujenga uchumi shirikishi unaolenga kuondoa
umaskini.Mkakati wa kuondoa umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye
nguzo za ushiriki wa kila Mtanzania katika uchumi wa taifa. Kwa misingi
hii, tukiweza kupunguza umaskini, tutaweza pia kupunguzatofauti za
kipato ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi cha sasa,
zinaweza kuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu.Uchumi
shirikishi ndio silaha dhidi ya umaskini.
8. Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani
mwema.Itakuwa nia yangu kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na
kudumisha umoja na amani nchini. Kadhalika, nitahakikisha kuwa usalama
wa mipaka ya Tanzania unaimarishwa kwa misingi ya ujirani mwema na
kutanzua migogoro na matatatizo yoyote na nchi jirani, kwa njia ya
diplomasia na mazungumzo.
HITIMISHO:
Hii ndiyo misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema
kuwa haitakuwa kazi rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na
maamuzi magumu, yote yanawezekana. Tumeona nchi nyingi zilizosimamiwa na
utawala thabiti wa serikali za kimaendeleo zikikabili na kupunguza
umaskini katika kizazi kimoja. Kama mataifa mengine yamefanikiwa, tena
bila raslimali kama zetu, kwa nini sisi tushindwe? Tuna kila sababu ya
kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea Watanzania matumaini mapya ya
maendeleo. Naomba nisisitize kuwa katika uongozi wangu hakutakuwa na
nafasi ya majungu, na visasi. Hatutaangalia nyuma bali tutasonga mbele
kwani ndicho Watanzania wanakitarajiakutoka kwa uongozi uliojengwa
kwenye misingi bora.
Ndugu Watanzania:-
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa matumaini na neema tele kwa wananchi.
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania kwa
umoja wetu tutajivunia kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa
kwa misingi ya utawala bora, chini ya serikali ya
kimaendeleo iliyojengwa kwenye fikra mpya za uzalendo, uadilifu,
utendaji na uwajibikaji.
Ni maono yangu kuwa Peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi
magumu na ushirikiano wa kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na wagombea
wenzangu ndani ya CCM, inawezekana kuanza safari hii ya Matumaini Mapya.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu hii fupi, kuna mambo matatu ningependa kuyaweka wazi hapa.
La kwanza, linahusu msingi wa uongozi ninaouamini na ambao
nimeusema mara kadhaa hapa. Msingi huo ni UWAJIBIKAJI.Watanzania
wananifahamu mimi si mtu wa maneno, ni mtu wa vitendo. Naamini kwa dhati
kabisa kwamba huwezi kuwa na Uongozi imara utakaoweza kusimamia ujenzi
wa Taifa imara iwapo huna ujasiri wa kuwajibika. Mimi nimeongoza kwa
mfano, na pale ilipobidi, nilikubali kuwajibika na kubeba dhamana ya
uongozinilipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.
La pili, mimi si mtu wa visasi. Siamini katika kuangalia ya
nyuma. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Na kwa nini tuangalie
nyuma wakati kama taifa tuna kazi kubwa sana mbele yetu inayohitaji
kufanywa? Mimi ni Mkristo; najifunza kutoka kwa Bwana Yesu ambaye
alipoulizwa: “Nisamehe mara ngapi?” Alijibu, “Samehe mara sabini mara
saba”. Nitaenzi na kudumisha utamaduni huu wenye sura ya utu na heshima.
La Tatu, natambua kwamba dhamana ya Urais ni shughuli nzito
hasa kwa taifa ambalo lina changamoto nyingi. Nataka niwahakikishie
Watanzania wenzangu kwamba afya yangu ni njema kuweza kuwatumikia katika
jukumu hili zito. Pamoja na vijineno vinavyosemwa pembeni, mimi
mwenyewe ndiye ninayejijua zaidi. Nawahakikishia kuwa nisingekuja hapa
leo na kueleza nia yangu hii ingekuwa sina uhakika na afya yangu.
Natoa RAI kwa Chama changu cha CCM, nadhani umefika wakati
kwamba tutende tofauti na mazoea, watu wote walionyesha nia ya kutaka
kuongoza, liundwe jopo la madaktari wa ndani na nje ya nchi tupimwe afya
zetu, kwa hili najitolea kuwa wa KWANZA KUPIMWA afya yangu
Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
0 comments :
Post a Comment