TV: Adui wa maadili, maendeleo ya Elimu ya Watoto!
Na Ahmed Lukinga, MSJ
“Kadiri unavyokuwa huru ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kuminya uhuru wa mtu mwingine,” ni msemo wenye maana pana inayogusa kila njanja ya maendeleo kwa namna na kiasi chake.
Ukomo wa uhuru wa mwanadamu hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine kulingana na mipaka inayoelekeza namna na kiasi cha uhuru anachostahiki mtu, kundi au jamii.
Uhuru wa Tanganyika kutawaliwa na viongozi wa kiafrika ulirejeshwa kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961, baada ya msululu wa mapambano ambao kilele chake hakikutugharimu umwagaji wa damu ukilinganisha na Zimbabwe na Afrika ya Kusini.
Mataifa mengine ya Afrika yaliyotangualia kupata uhuru baada ya vita ya pili ya dunia na wakaunda umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) lengo kuu likiwa kusaidia nchi za bara hilo kuondoa ukoloni na kulinda uhuru wao ambao awali uliminywa.
Uhuru wa baadhi ya viongozi wa serikali huru za Kiafrika umetumiwa kuminya uhuru wa wananchi kwa manufaa yao kwa mifano michache machafuko Tunisia, Libya na Misri kwa kutumia silaha kutoka katika mataifa yaliyowahi kututawala.
Tofauti na zama za ukoloni wa kimabavu, hivi sasa ulimwengu ni kijiji cha mawasiliano ya mtandao unaowasogeza watu walio mbali kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu kupitia uvumbuzi wa vifaa vya kidigiti Luninga ikiwa moja wapo.
Wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikizuia kuingizwa kompyuta na luninga nchini mwaka 1974, miaka miwili kabla Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishazindua kituo cha luninga iliyorusha matangazo ya picha za rangi.
Mapinduzi ya uhuru wa kupata habari kwa upande wa Tanzania bara yalianza mwaka 1994 kituo cha kwanza cha luninga (ITV) kilipozinduliwa japo nacho kilirusha matangazo katika mfumo wa analogia.
Watanzania wa zama hizi za matumizi ya ving’amuzi wanaweza kutazama vilivyowapita miongo kadhaa iliyopita, wanaweza kutazama kwa ukaribu zaidi katika nyumba zao ukilinganisha na zama za vibanda vya Luninga na magari ya abiria yaliyokuwa na Luninga ndani yake.
Kwa wale wanaoishi kwa mazoea sio rahisi kukubaliana na utafiti wangu kuhusu madhara ya Luninga kwa watoto ikiwa chombo hicho humbembeleza au kumuepusha mtoto kujumuika na wenzake wenye tabia zisizokubalika kwa hofu ya kufeli masomo, wizi na utukutu.
Binafsi naafiki hoja ya kuminya uhuru wa mtoto kwa kumuepusha na makundi mabaya isipokuwa sikubaliani na uamuzi wa kumruhusu mtoto kutazama vipindi vya Luninga vinavyomshawishi kuwa na tabia mbaya zaidi ya zile zinazozaniwa kuwa ni tatizo pekee katika ukuaji wa mtoto.
Watafiti wa madhara ya luninga, Bandura na Walters (1963) walithibitisha kwamba matumizi ya nguvu katika program mbalimbali za luninga yanaweza kuunda tabia za matumizi ya nguvu miongoni mwa watoto wanaovutiwa na waigizaji wa programu hizo.
Programu za luninga zinazochochea tabia ya ukorofi kwa watoto ni pamoja na filamu na tamthilia zinazohusu makosa ya jinai, katuni na michezo ya watoto (play stations) ambayo ilibuniwa na mataifa yaliyoendelea kama Marekani.
Mzazi wa zama za kidigiti haoni tabu kumruhusu mtoto wake kutazama nyimbo, kuangalia tamthilia za Kifilipino na vipindi vinavyoonesha maisha “halisi” ya wanasanaa kupitia Luninga ya familia kwa lengo la kumfurahisha au kumtuliza mtoto wake nyumbani.
Kana kwamba haitoshi mzazi ananunua santuri za filamu za Kitanzania maarufu kama ‘Bongo movie’ pasipo kujari madhara yake kwa mtoto kulingana na lugha inayotumika, mavazi yasiyoendana na maadili na vitendo vinavyochochea matamanio ya kufanya mambo yasiyoendana na umri wa watoto.
Aidha, mtoto mwenye mazoea ya kutazama Luninga mara kwa mara na kwa muda mrefu hupoteza umakini wa kujifunza shuleni na kuna uwezekano ufaulu wake kitaaluma ukashuka.
Ushawishi wa adui huyu tunayemuhifadhi katika nyumba zetu ambapo ni mahali salama unaminya uhuru wa mwanafunzi kujikumbusha alichofundishwa shuleni au kufanya kazi za ziada za kitaaluma akiwa nyumbani.
Mwanafunzi akitumia muda anaopaswa kulala kuangalia filamu za kutisha huaribu afya yake kwani maendeleo ya mtoto kiakili na kimwili, pamoja na mambo mengine, anapaswa kulala kwa muda usiopungua masaa nane kati ya 24 kila siku.
Luninga inapogeuka kuwa rafiki kipenzi wa mtoto kuna hatari ya kupunguza ukaribu na wazazi wake na jamii inayomzunguuka kwa kudhani kuwa aliyoyaona kwenye Luninga ndiyo maisha halisi.
Aidha, kupitia matangazo ya vyakula vya viwandani watoto wanashawishika kutumia kiasi kikubwa cha vinywaji baridi vyenye kiwango kikubwa cha sukari, chokoleti na peremende ambazo ni sehemu ya mlo wa kila siku.
Vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta vinavyoandaliwa haraka kama chipsi vinatumiwa na wanafunzi wa shule za msingi manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ya Tanzania hususani mjini.
Rejea ya utafiti wa buijzen na Valkenburg (2003) unaodhihirisha kwamba maombi ya watoto wanaotazama matangazo ya vyakula vya viwandani ni mengi zaidi ukilinganisha na wale ambao uhuru wao kutazama Luninga umeminywa na wazazi, mazingira au kipato.
Kisaikolojia, tabia ya mwanadamu hutokana na urithi kutoka kwa wazazi, na mazingira yanayomzunguuka. Lakini kwa kiasi kukubwa tabia huundwa mazingira ambayo yanajumuisha familia, dini, shule, makundi rika na vyombo vya habari.
Waswahili husema “samaki mkunje angali mbichi.” Hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha usalama wa mtoto kwa kuwasimamia na kuwapangia aina ya vipindi, eneo na muda wa kutazama Luninga.
Vilevile, kuna haja ya kuboresha uhusiano kati ya taasisi za elimu na wazazi kwasababu kuna uwezekano mkubwa mwanya uliopo ukatumiwa vibaya na wanafunzi kuiga tabia zisizofaa kutoka kwa marafiki wabaya.
Ili kuboresha mahusiano hayo kwa lengo la kuwalea vyema wanafunzi, shule za msingi na sekondari zinapaswa kusimamia miongozo inayoonesha majukumu ya wazazi katika maendeleo ya mwanafunzi.
Nichangamoto kwetu kama taifa kuhakikisha kuwa teknolojia ya leo inakuwa na manufaa zaidi kwa vizazi vyetu kuliko madhara. TV zina mengi ya kunufaisha ambayo kila kituo kinayaenzi huku kila kimoja kikidhibiti yale yasiyofaa. Mamlaka ya Mawasiliano nayo isilale wala kusinzia katika usimamizi wa maadili ndani ya vituo vya luninga.
Maoni 0655 229 266 BOFYA HAPA CHINI UWEZE KUI-DOWNLOAD MAKALA HII
******************************MAKALA*************************************
0 comments :
Post a Comment