Viongozi wa kamati ya usalama na madili ccm.
Na muandishi wetu raiamwema
MVURUGANO mkubwa ulizuka katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya wajumbe wanaomuunga mkono Edward Lowassa, kubaini jina lake limekatwa.
Hali ilikuwa hivyo baada ya majina matano ya watangaza nia kutoka Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwasilishwa katika Kamati Kuu.
Majina hayo matano ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Balozi Amina Salum Ally.
Watetezi wa Lowassa waliongozwa na Dk. Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, Meya wa Ilala, Jerry Silaa, Mbunge wa Afrika Mashariki, Adam Kimbisa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Khamis.
Aliyeanza kuhoji viongozi wa Kamati Kuu kuhusu kufyekwa kwa majina mengine ya watangaza nia, akiwamo Lowassa alikuwa Nchimbi ambaye kama wenzake hao, alitaka kujua sababu za kuenguliwa watangaza nia wengine.
Kundi hilo lilidai kwamba hakuna sababu nzito zilizotumika kuwang’oa watangaza nia wengine na kama hoja ni tuhuma za ufisadi, hiyo ni hoja isiyokuwa na nguvu, kwa mujibu wa mtazamo wao.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu kilichoketi Ijumaa iliyopita mjini Dodoma, zinaeleza kwamba safu hiyo ya watetezi wa Lowassa ilikuwa ikipeana ‘pasi’ kujenga hoja za kushinikiza kuongezwa kwa majina mengine mbali na hayo matano ili yafanyiwe kazi na kikao hicho.
Alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi CCM, Abdallah Bulembo ndiye aliyeingilia kati na kuwataka akina Nchimbi kuheshimu viongozi wakuu waliokuwamo kwenye kikao hicho, akipinga hali iliyokuwa ikijitokeza ya kujadili suala hilo kwa njia ya kejeli.
“Watu waheshimu viongozi waliomo humu ndani. Tunao viongozi humu wametumikia Taifa kwa juhudi na umakini mkubwa, wanaheshimika nasi lazima tuwaheshimu na tuheshimu uamuzi uliofikiwa ambao umeshirikisha hawa viongozi wetu (kwenye Kamati ya Usalama na Maadili),” alisema Bulembo ambaye alikuwa akitetea majina matano bora ya watangaza nia wa CCM.
Baada ya Bulembo, alifuatia Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye alifikia hatua ya kumtaja baba yake mzazi, Moses Nnauye aliyekuwa kada mhamasishaji kindakindaki wa CCM kwa miaka mingi chini ya uenyekiti wa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Ali Hassan Mwinyi.
“Taifa hili linahitaji kuongozwa kwa umakini na watu makini. Taifa linahitaji umakini na busara ya hali ya juu. Tusikubali hata kidogo kuruhusu Kamati Kuu ya Chama hiki ibariki mchezo wa kununua uongozi. Si busara kwa Kamati Kuu kuwa chanzo cha kuruhusu watu kununua madaraka. Lazima kubadilisha mfumo. Tukiruhusu hali hii, masikini hawatakuwa na chao, hawatapata nafasi na sisi wengine tusio na fedha za kununua madaraka itabidi tuondoke humu.
“Inasikitisha watu wapo tayari humu ndani (Kamati Kuu) kutetea ununuzi wa madaraka. Mimi baba yangu (Mzee Moses Nnauye) amefanya kazi kwenye hiki chama kwa uaminifu mkubwa, kwa miaka mingi hadi anaondoka hakuwahi hata kuwa na nyumba, leo watu wananunua uongozi, wengine siku mbili tatu baada ya kupata madaraka ana nyumba nyingi,” alisema Nape.
Baada ya Nape, alizungumza Zakhia Meghji ambaye kwa ukali aliwataka wajumbe wa Kamati Kuu kuheshimu uamuzi wa Kamati ya Usalama na Maadili akisema imeongozwa na Mwenyekiti Kikwete ambaye kwa nafasi yake ya Urais, anazo taarifa za kina kuhusu watangaza nia wote.
“Kamati Kuu lazima iwe na ujasiri. Mwenyekiti anazo taarifa zote tena za kina, kwa hiyo lazima wanazo sababu za msingi za kuleta humu majina matano,” alisema Meghji kwa mujibu wa nukuu ya chanzo chetu cha habari kutoka kikaoni humo.
Rais msitaafu Benjamin Mkapa naye alizungumza kwa ukali akisema; “Tunapata wapi ujasiri wa namna hii wa kutetea maslahi binafsi? Naona hapa ni mtu kwanza chama baadaye, si chama kwanza mtu baadaye. “Hapa hakuna mwenye taarifa za kina kama Mwenyekiti. Ni nani huyo mwenye taarifa za kina kumshinda Mwenyekiti? Tuna imani na uamuzi wa Kamati ya Maadili”.
Naye Mzee Mwinyi alisema; “Ni lazima tuheshimu kiti. Lazima muwe na uwezo wa kukubaliana na mambo yanavyokwenda. Nashangaa watu wapo tayari kukitishia chama, nguvu hizi za kukitisha chama mnazitoa wapi?”
Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, yeye alitoa mfano wake mwenyewe namna Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alivyomwondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 1995.
“Lazima tuheshimu mamlaka, Mwenyekiti anazo taarifa nyingi. Mimi mwaka 1995 Mwalimu Nyerere alining’oa na akasema kama nitapewa nafasi CCM yeye ataondoka, anakwenda kuanzisha chama. Mimi nikanyoosha mikono na kujitoa, Mwalimu akanifuata na kunikumbatia,” alisema Malecela ambaye alikuwa akisisitiza wajumbe wenzake wakubaliane na hali halisi.
Mzee Malecela ambaye alikuwa nje ya nchi kwa matibabu, alilazimika kutopumzika ili kuungana na wazee wenzake kuokoa jahazi lililoelekea kuzamishwa na nguvu ya fedha.
Rais msitaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kama ilivyokuwa kwa wenzake, naye aliweka bayana kuunga mkono uamuzi wa Kamati ya Usalama na Maadili akisema ni uamuzi uliopaswa kuungwa mkono.
Baada ya jina lake kutofikishwa Kamati Kuu na baadaye kushindwa kuilazimisha jina lake lirudishwe NEC, wapambe wa Lowassa wanadaiwa kuandaa mpango wa kutaka kumsaidia Balozi Amina aweze kupitishwa kuwa mgombea wa urais wa CCM, ili naye baadaye amtangaze Lowassa kuwa Mgombea Mwenza na hatimaye aweze kuwa Makamu wa Rais.
Mkakati huo ulitiwa nguvu na Balozi Amina mwenyewe wakati akijieleza kuomba kura ambaye mara mbili alisema kwamba alikuwa tayari kufanya kazi na Lowassa.
Hata hivyo, habari zinasema mpango huo ulikuja kuvuja kutokana na papara za baadhi ya wapenzi wa Lowassa kuanza kampeni za wazi kwa ajili hiyo katika Mkutano Mkuu ili Balozi Amina ashinde kwa kura nyingi.
Baadhi ya wafuasi wa Lowassa waliozungumza na Raia Mwema mjini Dodoma walidai kura za Balozi Amina zilichakachuliwa kumbeba Magufuli, kutokana na wao kuamini kuwa na nguvu kubwa ndani ya mkutano.
Alipokosea Lowassa, kilichomponza Membe
SITAKI kudai kuwa najua kwa uhakika sababu za Kamati ya Usalama na Maadili kukata jina la Edward Ngoyai Lowassa kutoka katika orodha ya wagombea wa urais ambao majina yao yaliwasilishwa katika Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa kwa ajili ya mchujo.
Lakini si vigumu sana kudodosa kwa nini kampeni ya Lowassa iliangukia pua. Lowassa alifanya makosa kadhaa ya kimkakati.
Ili kuelewa kilichomfanya Lowassa kufanya makosa hayo ya kimkakati, ni muhimu kupitia muktadha wa historia ya Lowassa kisiasa. Kuna mambo mawili ya msingi katika muktadha huu.
Kwanza, Mwalimu Nyerere alihoji usafi wa Lowassa na inadaiwa alimkataa wakati wa uhai wake asigombee urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na utajiri mkubwa usioelezeka.
Pili, Lowassa alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 baada kashfa ya Richmond iliyohusiana na mkakati wa Serikali wa kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hicho ndio cheo chake cha mwisho kikubwa cha kisiasa. Ndoto za Lowassa, ambaye aliamini angedumu katika wadhifa huo kwa miaka 10 yote ya Kikwete na hatimaye kumrithi nafasi ya urais, zilizimika ghafla.
Watu wawili wanatajwa kuwa ni nyota wa sinema ile ya kisiasa, ya Richmond, iliyomdondosha Lowassa. Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe na Spika wa Bunge wa wakati ule, Samuel Sitta. Si ajabu basi kuwa wawili hawa wamebakia kuwa ni maadui wa kisiasa wa Lowassa.
Baada ya kustaaafu, kumekuwa na tetesi kuwa uhusiano wa Lowassa na rafiki yake wa karibu wa siku nyingi, Jakaya Kikwete umekuwa ukiyumba huenda labda kwa sababu Lowassa anaamini hakutetewa. Wapo hata wanaoamini kuwa Kikwete alikuwa nyuma ya mkakati wa kumuondoa kutokana na ‘spidi’ kali ya utendaji ya Lowassa iliyotishia kumfunika.
Katika muktadha huo, urais kwa Lowassa ungekuwa na maana mbili kubwa. Kwanza, ingekuwa ni nafasi ya kusafisha jina lake kwa sababu kwa kawaida ni matendo yetu ya mwisho ndiyo yanayojenga urithi wa namna tutakavyokumbukwa. Nafasi ya juu ya Lowassa serikalini ilikuwa ni uwaziri mkuu ambao aliuacha kwa kashfa akituhumiwa kufisidi.
Pili, kwa Lowassa hii ingekuwa nafasi ya kulipa kisasi kwa wabaya wake. Wapambe walidai hana visasi, lakini je angemteua Mwakyembe, Sitta au Paul Makonda kushika nafasi yoyote Serikalini.
Nina hakika, utawala wa Lowassa ungehitimisha au kufifisha mustakbali wa kisiasa wa wanasiasa hawa katika uongozi wa nchi hii.
Hakuna haja ya kukaza mishipi ya shingo kupinga ukweli huo kwa sababu Lowassa asingekuwa wa kwanza kufanya hivyo. Ukichunguza utagundua kuwa hata Nyerere, Mwinyi, Kikwete – wote waliwanyima fursa baadhi ya watu. Watawala wote wanafanya hivyo na si vibaya kufanya hivyo, kisiasa.
Akijua kuwa angekamilisha mawili hayo, kusafisha jina na kulipa kisasi, Lowassa aliutaka sana urais. Kuutaka sana si tatizo. lakini kuonyesha kuwa anautaka sana ilikuwa ni tatizo. Ilikuwa ni suala la ‘iwe isiwe’, ‘vyovyote iwavyo’ na ‘kwa gharama yoyote’. Ilitutisha baadhi ya watu. Na hilo lilikuwa kosa la kwanza alilolifanya.
Katika kuutaka sana urais, Lowassa kiaina alitoa ‘ultimatum’ (tishio) kwa chama chake. alinukuriwa akisema haoni uwezekano wa kushindwa na haoni mtu wa kumkata jina lake.
Hilo lilikuwa ni kosa jingine. Alikiuka msingi muhimu wa CCM ambao wenyewe wamekuwa wakiukariri mara kwa mara, ‘chama kwanza, mtu baadaye’.
Ni wazi kuwa kama angekuwa Rais, ingekuwa ngumu kwa CCM kumdhibiti. Angekuwa na nguvu kuliko chama. Haipaswi kuwa hivyo, hususan, sasa wakati ambao Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana anamikakati ya kukipa chama nguvu zaidi za kusimamia Serikali.
Lowassa akaendelea kufanya kosa jingine la kukaribisha marafiki na wapambe wenye tuhuma na tabia za kutia shaka katika kampeni yake. Miongoni mwa hao walikuwapo mawaziri wa zamani na wafanyabiashara waliotoka serikalini kwa kashfa mbalimbali.
Haikuwa hatua nzuri kwa Lowassa ambaye tayari ana doa la Richmond kujizungushia atu wenye madoa kama yeye.
Hata watu waliojitokeza hadharani kuhoji uamuzi wa Kamati Kuu, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake Sophia Simba, Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Vijana wa CCM, Emmanuel Nchimbi na mbunge wa Afrika ya Mashariki, Adam Kimbisa, kwa maoni yangu waliongozwa na maslahi yao kuliko ya watu. Hakuna kati yao mwenye rekodi safi ya kuonyesha anasimamia maslahi ya umma. Kwangu hawa wote ni ‘opportunists’.
Kampeni ya Lowassa pia ilikuwa ya kitajiri. Pesa zilikuwa nje nje hadi ikawa ni ngumu kujua nani anamfuata Lowassa kwa sababu ya pesa na nani anaamini kwa dhati katika ubora wa urais wa Lowassa kwa ajili ya maendeleo!
Baadhi ya waandishi wa habari walineemeka mno katika kipindi hiki na ulikuwa muda mzuri kwa wenyeviti wa mikoa wa CCM kuchuma hadi wakajitoa ‘akili’ na kuonyesha wazi mapenzi yao. Hata Mwenyekiti wa Geita, anakotoka Magufuli, alikuwa kambi ya Lowassa!
Katika kuonyesha nguvu ya pesa tulishuhudia masheikh na wachungaji wenye njaa na mabodaboda waliokata tamaa wakienda kumshawishi agombee – usanii mtupu! Maandalio ya nguo na vifaa vingine vya Timu Lowassa yalikuwa makubwa mno – hata kabla hajajua kama atapita katika mchujo!
CCM kumteua Lowassa ingeweza hata kukiletea chama hicho hatari kwa sababu wapo wanaodhani mgombea huyo alikiuka si tu kanuni za maadili za chama, bali pia sheria za uchaguzi. Ikumbukwe msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alishaonya kuhusu kuzingatia sheria ya gharama za uchaguzi inayothibiti matumizi mabaya ya fedha katika mchakato huo.
Lowassa, akijua hatari anayokabiliana nayo kutoka kwa wahafidhina ndani ya chama waliohoji maadili yake, akaamua kuja na mkakati wa kuunda ‘kundi la msukumo kutoka nje ya chama’ ili wahafidhina wafanye uamuzi kwa shinikizo. Haukuwa pia mkakati mzuri sana na kinyume na matarajio uliimarisha azma ya wahafidhina ya ‘kumkata’.
Hata hivyo, makosa ya kimkakati aliyoyafanya Lowassa yanaeleweka. Alikuwa na kazi mbili ya kuzuia na kushambulia na akatumia mkakati wa kutumia maguvu mengi kuliko akili. Hatimaye ikamgharimu.
Lakini Lowassa angefanyaje? Jibu rahisi ni kuwa angekuwa mnyenyekevu kitabia, angetengeneza timu ya watu wasafi, angefanya mambo kwa kiasi na chinichini. Wazungu wanasema, ‘ chochote kikizidi sana kinadhuru’.
Kilichomponza Membe…
Binafsi sikutarajia kwamba Membe angepita katika mchujo, wakati Lowassa amekatwa. Nilitarajia kuwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ingeona busara ya kukata jina lake (Membe) ili kuvunja makundi na kuleta umoja katika chama.
Nani asiyejua kuwa Membe ndiye aliyekuwa mpinzani wa moja kwa moja wa Lowassa? Hawa ni kama Simba na Yanga.
Kotowiva kwa kwa kambi ya Lowassa na Membe hakukuja hivi hivi. Timu ya Lowassa iliamini kuwa Membe ni mtu wa karibu wa Kikwete na ndiye chaguo la Ikulu. Kwa hiyo timu ya Lowassa iliamini juhudi za Ikulu kumkata mgombea wao zililenga kumsaidia Membe.
Kutokana na ukaribu unaozungumzwa wa Kikwete na Membe, ambao ni kama mashemeji ukizingatia Membe anatoka Lindi kama mama Salma, haikuwa ngumu kwangu kutabiri kuwa Membe angeanguka katika Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo ilijaa wapenzi wa Lowassa.
Kadhalika, haikuwa ngumu kung’amua kuwa kijana mwingine wa Kikwete, mwandishi wake hotuba wa zamani, Januari Makamba angeungana na Membe kutupwa nje ya kinyang’anyiro. Ukaribu wao na Kikwete uliwaponza wawili hawa.
Katika ‘saga’ la Lowassa, sitaacha kuhoji kuhusu misimamo ya Kingunge Ngombale Mwiru, mwanasiasa mkongwe, ambaye kabla ya matukio haya nilimweka katika kiwango cha uadilifu, umahiri na heshima cha Nyerere, Kawawa na waasisi wengine.
Kwa nini alikubali kujipaka matope na kuondoa heshima yake kwa sababu ya Lowassa? Aliahidiwa nini hadi akajitokeza hadharani kama muasi na kujaribu kuaminisha watu kuwa CCM itashinda tu kama Lowassa atakuwa mgombea? Yule si Kingunge niliyemfikiria alivyo.
Magufuli aokota dodo…
Mwisho wa siku mwanakemia John Magufuli, aliyeendesha kampeni ‘poa’ ya bila mbwembwe, akaokota embe dodo mchangani katika Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kuwadondosha wanawake wawili Amina Salim Ally na Asha Rose Migiro ambao aliingia nao fainali katika kinyang’anyoro hicho.
Sina hakika kama anastahili zaidi kuliko wagombea wote lakini bila shaka alikuwa chaguo bora kuliko akina mama wawili alioingea nao fainali, ukizingatia changamoto zinazolikabili taifa na changamoto ya vyama vya upinzani.
Magufuli anatoka Kanda ya Ziwa. Yeye ni mtendaji mzuri anayetaka kuona matokeo, ana uzoefu usiopungua miaka 20 serikalini. Pamoja na kuwa ni mwanasayansi, Magufuli ni mwanasiasa mahiri jambo lililothibitika kwa jinsi alivyokuwa akichangamana na watu katika Mkutano Mkuu ukumbini hapo akiomba kura.
Magufuli ana udhaifu wake pia. Hajui Kiswahili na anachanganya ‘r’ na ‘l’ katika matamshi yake. Wakati fulani anaweza kuwa dikteta. Pia Magufuli ana maamuzi ya haraka. Naamini hana uzoefu mkubwa kimataifa na labda atawahitaji wazoefu kama Amina Salim Ally, Asha Migiro na Dk. Augustine Mahiga, kumsaidia katika eneo hilo.
Hata hivyo, ukweli ni kuwa changamoto nyingi zinazokabili Taifa kwa sasa ni za ndani zaidi kuliko nje. Tunatarajia Magufuli akipitishwa kuwa rais ataimarisha mshikamano wa Taifa, atapambana na rushwa na ufisadi, ataanzisha vita dhidi ya madawa ya kulevya, ataleta nidhamu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi.
Chanzo raiamwema
Kutoka Mzalendo net
0 comments :
Post a Comment