Dodoma.Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali
haijafuta daraja sifuri katika matokeo ya mitihani taifa ya shule za
sekondari na kwamba ilichokifanya ni kuondoa mrundikano wa madaraja.
Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Magige
alitaka kufahamu kama kushusha madaraja ni suluhisho la kuwaokoa vijana
waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Mapema
katika swali lake la msingi, Magige, alitaka kufahamu kama Serikali ina
mkakati wa kuanzisha mpango maalumu hasa wa ufundi kwa wanafunzi
waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali.
“Tumeongeza
madaraja ili kuwatambua watoto, kulikuwa na mrundikano katika daraja
moja. Serikali haijafuta division ziro na wala hakuna division V, ipo
division I, II,III, IV na ziro kama kawaida,” alisema.
Alisema
uamuzi wa kushusha madaraja, hauna lengo la kuwaokoa wanafunzi
wanaofanya vibaya na badala yake, unalenga katika kuondoa mrundikano wa
alama katika daraja moja.
Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.
Alisema
kulikuwa hakuna ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi kama kanuni
inavyosema kuwa lazima kuwe na ufuatiliaji wa asilimia 50 kwa 50 .
Alisema
kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa alama 50 katika ufuatiliaji wa
maendeleo ya mwanafunzi na katika mtihani ya kumaliza shule asilimia 50.
Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.
Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.
Hata
hivyo, baada ya kumaliza kujibu swali hilo, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka bungeni kauli ya waziri kuhusiana
na suala hilo.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema
Kuhusu
wanafunzi waliofanya vibaya mwaka jana katika mitihani yao, Mulugo
alisema Serikali haitaanzisha mpango maalumu wa ufundi kwa vijana hao.
Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.
Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho.
0 comments :
Post a Comment