IKIWA
imebaki siku tatu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake
Wajumbe wa Mkutano Mkuu zaidi ya 3,000 tayari wamewasili mjini Dodoma na
kusababisha ulinzi mkali kuimarishwa kila kona ya mji huo. Polisi
waliovaa sare na wale wasiovaa sare wameonekana kila eneo la mji wa
Dodoma wakiwemo wale wa Kikosi cha Farasi ikiwa katika kuhakikisha kuwa
hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo kutokana na Serikali nzima
kuhamia mji huo kwa ajili ya mchujo wa kumpata mgombea urais
atakayepeperusha bendera ya CCM.
Kila kona ya mji wa Dodoma
wananchi na baadhi ya wageni wamekuwa wakizungumzia mchakato huo ambao
ni mgumu ndani ya CCM wa kuhakikisha kuwa wanampata mgombea ambaye
anakubalika na kuuzika kwa wananchi. Baadhi
ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo ambao ndio watakaopitisha jina la
mgombea urais wamesema ikiwa Kamati Kuu ya CCM itawapa jina la mgombea
ambaye haendani na maisha ya Watanzania wamesema hawatapiga kura na
kisha watatoka nje.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini
Dodoma jana wajumbe hao wamesema kwa sasa hata wao wamechoka kutokana na
vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wagombea ambapo baadhi yao
walichukua takwimu za wanachama waliofariki na kudai kuwa wamepata
wadhamini wengi.
Walisema ni bora Azimio la Arusha lirudi kwa
muda lakini wanaitaka Kamati Kuu kufanya uamuzi sahihi katika kumpata
mgombea urais wa CCM vinginevyo ni bora wasipige kura na kama
itawezekana basi watalikataa jina la mgombea urais litakalopitishwa.
Wajumbe
hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema wanataka kiongozi wa
leo kwani kila mtu anaitwa mzee akiwemo January Makamba, Mark Mwandosya
na Makongoro Nyerere ambao wao kwa mtazamo wao wanaamini kuwa ndio
wanaweza kuwapitisha mmoja kati ya hao.
Wakizungumzia kuhusu
kupewa fedha na mmoja wa wagombea wa chama hicho ili wampitishe,
walisema wao hawawezi kuhongwa kwa kuwa wako zaidi ya 1,900 sasa huyo
ambaye anatajwa ana hela ya kuwahonga wajumbe wote atawezaje.
"Hatujui
nani kahongwa kama ambavyo habari zimeenea lakini ukweli ni kwamba huyo
anayetajwa kuwahonga sidhani kama anafedha ya kuwahonga wajumbe wote
lakini sisi tunavyodhani inawezekana huyo aliyesambaza habari hizo ndiye
anayehonga watu hao,"walisema wajumbe hao.
Kwa upande wake Kada
anayedaiwa kutumika na mgombea nafasi ya Urais kugawa fedha Cyprian
Musiba, alisema anashangazwa na tuhuma kuwa alikuwa akigawa fedha na
kisha kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
wakati jambo hilo sio na kweli.
Akizungumza na waandishi wa
habari mjini Dodoma jana Musiba alisema hizo ni siasa chafu za kutaka
kuwachafua watu ili waonekane kuwa ni watoa rushwa wakati wanaosambaza
habari hizo ndio hao wahusika.
"Kama mnavyoniona hapa na mimi
nimeita ili kuwaambia ukweli hivi kama ni kuwahonga unawahonga wajumbe
wa Mkutano Mkuu wangapi jamani hata ninyi waandishi hebu pimeni wenyewe
kweli kila mmoja apewe kiasi walichosema ni jambo la ajabu sana na
ukweli ni kwamba hizo habari si za kweli,"alisema Musiba.
Wakati
huo huo, Rais Jakaya Kikwete jana alitarajiwa kuongoza kikao cha Kamati
ya Usalama na Maadili ya Chama hicho ambacho kilishindwa kuanza katika
muda mwafaka kutokana na sababu ambazo hazikufahamika.
Kikao
hicho ni moja kati ya vikao vitatu muhimu katika kuelekea kumpata
mgombea wa chama hicho ambapo leo Rais Jakaya Kikwete atazindua ukumbi
mpya wa CCM ulioko nje kidogo ya mji wa Dodoma kabla ya kwenda kulivunja
Bunge na baadaye kuhudhuria Kikao cha Kamati Kuu ya CCM ambacho
kitakuwa na majina matano ya awamu ya kwanza ya wagombea.
0 comments :
Post a Comment