Dar
es Salaam. Mambo yamekuwa mazito. Ndivyo inavyoonekana baada ya vyama
vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa
kutangaza mgombea urais jana badala yake ukatoa ahadi mpya kwamba sasa
atatangazwa muda wowote ndani ya siku saba.
Kauli
hiyo inayoibua maswali mengi imekuja baada ya viongozi wa umoja huo
waliofanya vikao hadi usiku jana bila ya viongozi wakuu wa CUF ambao
wameahidi kutoa msimamo wao leo saa 5.00 asubuhi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kilichodumu kwa saa
11.30, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema wamekamilisha
mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye watamtangaza kwenye
mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel
Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo alisema hakuna mpasuko kama
inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Mwenyekiti
Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu
wake wa Bara, Magdalena Sakaya hawakuhudhuria kikao hicho
kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum
jijini Dar es Salaam.
Badala
yake, Sakaya aliiambia Mwananchi jana jioni kuwa CUF haikuweza kushiriki
kikao hicho kwa kuwa kulikuwa na mambo ambayo hawajakubaliana ndani ya
chama na kwamba kama wangemaliza mapema, wangekwenda kwenye kikao hicho.
Baadaye
usiku, CUF ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa
itazungumza na waandishi wa habari leo saa 5.00 asubuhi kwenye ofisi za
chama hicho Dar es Salaam kutoa taarifa kuhusu Ukawa.
Kutokuwapo
kwa viongozi wa CUF jana na habari kwamba chama hicho kitatoa taarifa
peke yake leo, kunaweka giza nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa;
Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ambavyo vilikubaliana kusimamisha
mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Kutokuwapo
kwa viongozi wa CUF kulisababisha Ukawa kushindwa kumtaja mgombea wake
na habari ambazo zilipatikana awali, zilisema huenda vyama hivyo
vikatangaza jina la chama kitakachotoa mgombea urais badala ya jina la
mgombea.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zilisema hoja kubwa ilikuwa katika suala la
mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye
ameshachukua fomu za CUF na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
ambaye anaungwa mkono na vyama vyote vinne.
Tayari
Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila ya mafanikio, wakati Dk
Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa
CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Sakaya
alisema jana kuwa CUF haikushiriki kikao cha jana kutokana na
kutoafikiana baadhi ya mambo ndani ya chama chake, ikiwa ni pamoja na
suala hilo la kusimamisha mgombea mmoja wa urais kupitia
Ukawa.“Nilimpigia simu (naibu katibu mkuu wa Chadema, John) Mnyika
kumwambia kwamba tunaweza tukachelewa kwa sababu tulikuwa katika kikao
cha CUF cha majadiliano, lakini mpaka sasa (saa 1:48 usiku) bado
hatujapata mwafaka,” alisema Sakaya na kuongeza:
“Tukishakamilisha
majadiliano yetu kama chama, tutakwenda kuzungumza chini ya mwamvuli wa
Ukawa kwa sababu tunahitaji kujiridhisha kwanza kabla ya kuzungumza au
kufanya maamuzi yoyote.” alisema.
Sakaya
alipoulizwa ni mambo gani ambayo hawajakubaliana na wenzao wa Ukawa,
alisema hawezi kuyazungumza hadi pale watakapoyamaliza na kuwaita
wanahabari kwa pamoja na kutoa ufafanuzi.
Alisema
hawakutuma mwakilishi katika kikao hicho na kwamba kama kulikuwa na
mwakilishi aliyekwenda kwa ajili yake binafsi na si kukiwakilisha chama.
Viongozi
wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD vinavyounda umoja huo,
walianza kuingia kwenye ukumbi wa hoteli hiyo saa 3.00 asubuhi, huku Dk
Slaa akiwaeleza waandishi wa habari kwamba hoja kubwa ya kikao hicho
ilikuwa ni mgawanyo wa majimbo, yakiwamo 26 mapya pamoja na kumtaja
mgombea urais.
“Tutawaeleza
kinachoendelea ngoja tuingie katika kikao kwanza. Ila hoja kuu ndiyo
hizo mbili na tukishakubaliana tutawaeleza wala haina shida,” alisema Dk
Slaa.
Takriban
wiki moja iliyopita, Profesa Lipumba akiwa na viongozi wakuu wa Ukawa
waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa mgombea urais
wa Ukawa angetangazwa Julai 14 (jana), kwa maelezo kuwa majadiliano
yalikuwa yakiendelea.
Lakini
jana, Profesa Lipumba pamoja na viongozi wenzake wa CUF, hawakuonekana,
jambo ambalo liliibua maswali mengi kwa wanahabari.
Katika
kuonyesha kuwa kikao hicho kilipangwa kuwa siri, viongozi wa Ukawa
hawakutaka kutaja eneo kinapofanyika na kuwaeleza wanahabari kuwa
wataitwa kupewa taarifa na kufafanua kuwa kulikuwa na vikao vya ndani
vilivyokuwa vikiendelea.
Hata baada ya wanahabari kubaini eneo ambalo kikao hicho kinafanyika, viongozi hao walikuwa wagumu kutoa taarifa.
Habari
kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo zinasema kuwa Profesa Lipumba
anashinikiza kupitishwa na Ukawa kugombea urais, jambo ambalo linapingwa
na viongozi wengine wa vyama vinavyounda umoja huo kwa maelezo kuwa
tayari CUF imesimamisha mgombea wa urais Zanzibar.
Idadi
kubwa ya viongozi wa vyama hivyo wanashinikiza Dk Slaa apewe nafasi hiyo
kutokana na kukubalika zaidi kuliko Profesa Lipumba. Pia anapigiwa
upatu kutokana na rekodi yake kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 wakati
alipomtikisa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.Taarifa zaidi zinaeleza
kuwa hoja ya ugawaji wa majimbo haikuwa na nguvu kama ya urais ambayo
imekitikisa kikao cha jana mpaka kufikia hatua ya viongozi kulumbana
waziwazi na kuonyana kwamba wasipokuwa makini umoja huo utatetereka.
“Leo
viongozi wa CUF hawapo, wapo wa vyama vingine,” alisema mmoja wa wajumbe
wa mkutano huo na alipotakiwa kufafanua sababu hiyo alisisitiza kusema
kwamba “hata kwa macho huoni kaka”.
Awali,
licha kutokuwapo kwa wawakilishi wa CUF, viongozi wengine wa umoja huo
walishindwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari saa 9.30 alasiri kama
walivyokuwa wameahidi badala yake walimtuma Ofisa Habari wa Chadema,
Tumaini Makene kuwaeleza wanahabari kuwa mjadala uliokuwa ukiendelea
ulikuwa wa majimbo mapya kwa kuwa ni suala jipya na lilikuwa limeibua
changamoto mpya.
“Kwa sasa
viongozi wanajadili kuhusu majimbo mapya ya uchaguzi ambayo Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeyatangaza juzi. Subirini tu wala msiwe na
haraka,” alisema Makene na kuahidi kuwa taarifa za kikao zingetolewa saa
12.30 jioni.
Hata
ulipofika muda huo, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa zaidi ya waandishi
wa habari kutakiwa kuvuta subira mpaka kikao kimalizike. Ilipofika saa
1.45 usiku, Makene aliwaeleza waandishi wa habari kwamba majadiliano
bado yalikuwa yakiendelea na muda wowote taarifa zingetolewa.
Viongozi wengine waliokuwapo katika kikao hicho ni Mnyika, Dk Slaa na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe.
Mtatiro aonya kuvunjika
Akiandika
katika ukurasa wake wa Facebook, naibu katibu mkuu wa zamani wa CUF,
Julius Mtatiro jana aliwaonya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa
wanaosema “bora Ukawa ivunjike”, akisema hali hiyo ikitokea vyama hivyo
havitabaki salama.
Mtatiro,
ambaye amekiri kuandika onyo hilo kwenye ukurasa wake, alisema: “Mimi
nataka kurudia kusema hapa, kwamba Ukawa ikivunjika kwa sababu yoyote
ile, ni kitendo cha vyama vya upinzani kuwasaliti wananchi. Hakuna lugha
nyingine.”
Alisema
wanaofurahia Ukawa kutetereka na wanaoombea ivunjike wanafanya maombi
yasiyo na tija kwa Taifa, kwa kuwa Ukawa ikishavunjika vyama vya
upinzani havitabaki salama hata kidogo.
“Athari ambazo chama kimoja kimoja kinazipata ndani ya Ukawa ni chache kuliko chama kimoja kikienda kivyake,” alisema.
“Ukawa
ilikuwa na malengo makubwa sana. Ukiachilia mbali uchaguzi, kuna ajenda
ya Katiba. Tuliondoka kwenye Bunge la Katiba na kuacha Sh. 30 milioni
kila mjumbe kwa sababu ya kujenga mshikamano wa upinzani. Kuvunja Ukawa
leo ni kusema pia tunakubali Katiba Inayopendekezwa.”CHANZO:MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment