RESEARCH AND EDUCATION FOR DEMOCRACY IN TANZANIA (REDET)
July 6, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baadhi ya vyombo vya habari katika taarifa zao zilizochapishwa katika matoleo yao ya Jumatatu tarehe 6 Julai, 2015 vimechapisha taarifa zinazohusu utafiti uliofanywa na REDET juu ya Maoni ya Wananchi Kuhusu Uchaguzi Mkuu Utakaofanyika Oktoba 2015. Taarifa hizi zimesababisha wadau wengi hapa nchini kutaka ufafanuzi kutoka REDET.
Kama ilivyo kawaida yake REDET imejijengea heshima na utamaduni wa kufanya kazi zake kwa misingi ya uwazi na ukweli. Kwa hali hii tunapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
i. REDET ilifanya utafiti juu ya maoni ya wananchi kuhusu hali ya siasa Tanzania na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015 kuanzia tarehe 23 hadi 26 Juni 2015. Utafiti ulikusudiwa kufanyika katika mikoa yote 30 Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa bahati mbaya kibali cha kufanya utafiti Zanzibar hakikutolewa kwa wakati. Hivyo taarifa za utafiti zilipatikana kutoka mikoa 25 ya Tanzania Bara tu. Badala ya kupokea taarifa za mahojiano 1,500, zilipokelewa 1,250 sawa na takribian asilimia 83. Rasimu ya taarifa ya awali iliandaliwa kutoka mikoa hiyo tu;
ii. Tarehe 2 Julai, 2015 REDET ilitoa mwaliko wa Mkutano wa Wanahabari ili kuwawezesha Watanzania kupitia vyombo vya habari kupokea matokeo ya utafiti Jumapili tarehe 5 Julai, 2015 saa 5.00 asubuhi;
iii. Baada ya kutafakari kwa kina na kwa kuzingatia ukweli kwamba rasimu ya taarifa ya utafiti haikuhusisha mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uongozi wa REDET uliazimia kufanya juhudi zaidi ili kuwezesha mamlaka husika katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuridhia utafiti huu uhusishe pia mikoa ya Zanzibar, ili ripoti itakayotolewa iwe kamilifu na yenye sura ya Kitaifa;
iv. Tarehe 4 Julai, 2015, REDET ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kuhairishwa kwa mkutano wa wanahabari uliokuwa ufanyike tarehe 5 Julai, 2015 kutokana na kutokamilika kwa taarifa kamili ya utafiti;
v. REDET imewasilisha maombi kwa uongozi wa juu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuomba uwasiliane na mamlaka husika Zanzibar ili ruhusa iweze kutolewa kufanya utafiti huu katika mikoa mitano ya Zanzibar;
vi. REDET itatoa taarifa kamili ya utafiti kuhusu Maoni ya Wananchi Kuhusu Uchaguzi Mkuu Utakaofanyika Oktoba 2015, mara tu taarifa yake itakapokamilika; na
vii. Mwisho, uongozi wa REDET unaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.
Imetolewa na:
Menejimenti,
Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET)
Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET)
0 comments :
Post a Comment