Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Ikungi na ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza kuu la uongozi Taifa,Bwana Athumani Henku akizungumza na mwandishi wa habari hizi(Picha Na Jumbe Ismailly).
Na Jumbe Ismailly,Ikungi      
CHAMA Cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida kimesema kitaandika barua kwenda CUF Makao makuu kuomba kuvunja masharti  kwenye wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida yaliyofikiwa katika kikao cha pamoja cha vyama vilivyopo kwenye umoja wa Ukawa kuhusu kuachiana majimbo ya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ubabe wanaofanyiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA).
Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ikungi,Athumani Henku alisema CUF wilaya ya Ikungi haipingani kabisa na masharti yaliyofikiwa kwenye kikao hicho cha pamoja na inaunga mkono kwa asilimia mia moja masharti hayo yatekelezwe kwenye wilaya zote za Tanzania,isipokuwa wilayani Ikungi peke yake.
Mwenyekiti huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akielezea masikitiko yake juu ya ubabe,dharau na manyanyaso wanayofanyiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida kwa ujumla pamoja na kutokuwa tayari kutekeleza makubaliano hayo kwenye jimbo hilo.
Alisema Henku ambaye pia ni mjumbe wa Baraza kuu la uongozi taifa la chama hicho,kuwa CHADEMA wilaya na hata Mkoa wa Singida haipo tayari kutekeleza makubaliano hayo licha ya kuwepo baadhi ya maeneo ambacho chama hicho hakikubaliki zaidi ya CUF.
Hata hivyo mjumbe huyo aliyefuatana na katibu wa chama hicho alifafanua kwamba sababu zinazochangia chama hicho kutokuwa tayari kushirikiana na Chadema wilayani Ikungi ni pamoja na Chadema kukiuka masharti ya makubaliano yaliyofikiwa na vyama vilivyopo kwenye umoja wa Ukawa.
Kwa mujibu wa Henku sababu nyingine ni kwamba mbunge wa jimbo hilo,Tundu Lissu kwa mamlaka aliyopewa aligawa mfuko wa jimbo hilo bila kufuata utaratibu wa sheria inayoongoza matumizi ya mfuko huo,kijiji cha Ikungi kuwa na mpango wa kuanzisha michango ambayo ni kinyume cha imani ya ajenda ya ukombozi na hata katiba ya nchi.
“Tumegundua kuwa mwenyekiti wa Kijiji cha Ikungi na serikali yake wana mpango wa kuanzisha chanzo kipya cha mapato ambacho kitamtaka mkazi yeyote yule ambaye siyo mzawa wa Ikungi anapohamia katika Kijiji hicho kulipa shilingi 20,000/= kwa kila mwezi jambo ambalo ni kinyume na katiba ya nchi”alisisitiza mwenyekiti huyo
Aidha tuhuma zingine ni viongozi wa Chadema kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo pamoja na tabia ya baadhi ya wafuasi wa Tundu Lissu kuwabeza kwa kusema kwamba CUF Ikungi hawana uwezo wa kuongoza au kugombea kwenye nafasi yeyote ile na kushinda.
Henku hata hivyo alifafanua kwamba kwa sasa yeye kama mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ikungi ana kazi ya kukijenga chama hicho katika wilaya yake,na atakuwa na ziara ya miezi miwili kabla ya kuanza harakati za kutangaza kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo lolote lililopo katika wilaya hiyo.
Akizungumzia tuhuma zilizoelekezwa kwa CHADEMA na mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ikungi,Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Singida,Shabani Limu alikiri kwamba CUF haina mtaji wa kuachiwa kugombea nafasi yeyote ile katika jimbo la Singida mashariki na magharibi.
Hata hivyo Limu alisema cha kushangaza ni kwamba Henku pamoja na kuwa ni mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ikungi,amekuwa akitumia nafasi ya ujumbe wa baraza kuu la uongozi taifa kushinikiza lazima aachiwe nafasi ya kugombea ubunge wakati muda wote hakuwepo na wala hafahamike kwenye majimbo yote mawili.
Kuhusu ziara anayofanya katika maeneo mbali mbali ya wilaya ya Ikungi,mwenyekiti huyo alionyesha kushangazwa na mwenyekiti huyo wa CUF kwa kile alichodai kwamba hata huko anakofanya mikutano amekuwa akiwatumia viongozi wa Chadema kuwaandalia mikutano ya hadhara