Msekwa amesema kanuni zote za Bunge zipo vile vile tangu yeye
alipokuwa madarakani na kwamba kilichobadilika kwa sasa ni aina ya
wabunge waliopo.
Hata hivyo, hakufafanua kuhusiana na aina ya wabunge, lakini kwa
sasa Bunge hilo lina idadi kubwa ya wabunge vijana pamoja na wabunge
wengi kutoka upinzani.
Aliyasema hayo juzi usiku katika kipindi cha dakika 45
kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV na kituo cha redio cha
Redio One.
Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, alisema kinacholeta mzozo ni namna kiti
kinavyoongoza Bunge kwa maana ya staili inayotumika.
Aliongeza kuwa Bunge hilo lina mchanganyiko wa wabunge wa upinzani
na CCM ambao pia wamo vijana wa kutosha na kwamba kiti hakiwezi
kuendelea kutumia staili ile ile ya siku zote.
Msekwa ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee la CCM,
alikiri kwamba siku za nyuma kiti cha Spika kilikuwa kinaheshimika
tofauti na ilivyo sasa.
Mwanasiasa huyo alisema ni aibu na fedheha kwa wabunge kusimama na
kuzomea huku Spika naye akiwa amesimama na kwamba jambo hilo halikuwapo
wakati wa uongozi wake.
Alifafanua kuwa haya yanayotokea kwa sasa yanatokana na wakati huu
kuwa ni wa kizazi kipya na kwamba ili kuongoza mhimili huo, ni lazima
staili ibadilike.
Hata hivyo, Msekwa hakusema ni staili ya namna gani itakayoweza
kulibadilisha Bunge na kuondoa mizozo ambayo imekuwa ikijitokeza mara
kwa mara ikiwamo wabunge kutoka nje na kususia vikao.
Ingawa Msekwa hakuweka wazi kauli yake, lakini inaonyesha kuwa
anatoa angalizo kwamba kwa wakati huu Bunge haliwezi kuendeshwa kwa
misingi ya uhafidhina.
Wiki iliyopita wabunge wa upinzani walisimama bungeni kupinga
serikali kuwasilisha miswada mitatu ya gesi, mafuta na petroli, lakini
Spika alipinga hatua hiyo na kuagiza wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Baada ya agizo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Haki na
Mamlaka ya Bunge, Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, pamoja na
wajumbe wake walikutana na kuazimia kuwatimua wabunge wa upinzani 11.
Wabunge hao walitimuliwa na kuzuiwa kuhuduria vikao vyote vya Bunge
vilivyosalia kuanzia wiki iliyopita hadi chombo hicho kitakapovunjwa
kesho na Rais Jakaya Kikwete.
Kuhusu namna ya kumpata mgombea bora wa urais ndani ya CCM, Msekwa
alisema vikao vyote vitaangalia sifa 13 zilizowekwa na chama hicho.
Alisema vigezo hivyo ambavyo vipo wazi na kila mgombea anavijua
ndivyo vitakavyotumika ili kila mgombea apate haki yake anayostahili.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments :
Post a Comment