Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua
hatua za haraka za kukomesha machafuko yanayoendelea Jamhuri ya Afrika
ya Kati. Akizungumza mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, Ban Ki moon amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa
kuchukua hatua za haraka za kuzuia wimbi la jinai mpya na maangamizi
makubwa ya kidini na kikabila nchini humo. Ban Ki moon amesisitiza na
hapa tunamnukuu: 'wingu zito jeusi la jinai kubwa na maangamizi ya
kidini na kikabila limetanda katika anga ya Afrika ya Kati', mwisho wa
kunukuu. Ban Ki moon ameongeza kuwa, iwapo mgogoro wa hivi sasa
unaoendelea kutokota Jamhuri ya Afrika ya Kati hautakomeshwa, bila shaka
kuna wasiwasi nchi hiyo itaendelea kushuhudia mapigano hadi miongo
kadhaa ijayo. Hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la
Amnesty International lilikosoa kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana
na mauaji yanayojiri nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taarifa ya
shirika hilo la kimataifa ilieleza kuwa, lina ushahidi wa kutosha
unaoonyesha ukatili na mauaji yanayofanywa na kundi la Kikristo la Anti
Balaka dhidi ya maelfu ya Waislamu nchini humo.
CHANZO:DW
CHANZO:DW
0 comments :
Post a Comment