Kamera hizi ni ghali zikiwa zimegharimu kiasi cha kuanzia dola 180,000 hadi dola 200,000 kwa kila moja
POPOTE utakapotulia na kutazama pambano lolote litakaloonyeshwa
moja kwa moja au kwa marudio, kupitia kituo cha Televisheni cha Azam
(Azam TV), usiwe na shaka, utaliona pambano maridadi.
Weka soda yako sebuleni kando kisha watazame Jerry
Santo na Amri Kiemba wakichuana katikati ya uwanja wowote ule wa soka
nchini huku kamera nane za Azam TV zinazorekodi pambano lao zikiwachukua
kwa umaridadi.
Kamera nane zamrekodi mchezaji
Katika pambano lolote litakaloonyeshwa na Azam TV
kutakuwa na kamera nane uwanjani. Huu ni wastani wa juu wa idadi ya
kamera zinazopaswa kuonyesha kwa ufasaha pambano lolote la soka ingawa
katika mechi za ligi nyingine au michuano mingine kunakuwa na kamera
zaidi za kuonyesha mbwembwe mbalimbali.
Kamera hizi ni ghali zikiwa zimegharimu kiasi cha
kuanzia dola 180,000 hadi dola 200,000 kwa kila moja. Ndani ya kila
kamera kuna mchanganyiko wa mashine ya Sony huku lensi ya kuvutia
matukio kwa ufasaha ikiwa ni ya kampuni ya Cannon. Kamera mbili zitakuwa
zinakaa katika kila nyuma ya lango la uwanja. Kamera hizi mbili zina
kishikilio kirefu na kuifanya ining’inie katika eneo lote la nyuma ya
lango kama tunavyoona katika mechi za Ligi Kuu England na michuano
mbalimbali.
Katika pande mbili za uwanja, karibu na benchi la
kila timu kutakuwa na kamera mbili ambazo watu wanaorekodi mpira
wataweza kukimbia nazo huku na kule kwa ajili ya kutokana matukio
yanayoendelea katika upande wa kulia na kushoto kuanzia pale anapokaa
mwamuzi wa akiba.
Kamera ya nne ni ile iliyosimama katikati ya
uwanja, karibu na mwamuzi wa akiba. Kamera hiyo huwa inasimama ilipo na
haisogei. Dhumuni kubwa ni kuzivuta kwa karibu sura za wachezaji au
mwamuzi inapohitajika.
Jukwaani kuna kamera kubwa zaidi, pengine kuliko
zote. Mtambo huu unarekodi mechi yote kwa juu na ni nzuri kwa mwelekeo
mzima wa ‘muvu’ kwa timu zote mbili. Lakini pia kando ya kamera hii kuna
kamera nyingine kubwa ambayo nayo inadaka kwa haraka matukio ya ndani
ya uwanja.
Pia bado kuna kamera ya saba ya mtu ambaye
anazunguka katika kando ya uwanja kwa ajili ya kuchukua mahojiano kabla
ya mechi, wakati wa mapumziko na mechi ikiisha. Kamera zote hizi saba
zina uwezo wa kurekodi na kuvuta kwa karibu tukio lililo umbali wa mita
400 kutoka zilipo. Hii ni sawa na muunganiko wa viwanja vinne vya
mpira!
OB Van ya kisasa zaidi barani Ulaya
Kamera hazina kazi yoyote kama huna OB (Outside
Broadcasting)Van ya kisasa. OB Van ni gari linalokamata matangazo
uwanjani na kwingineko nje ya studio kutokea katika kamera na kurusha
katika setalaiti iliyo hewani. OB Van ya Azam TV ni ya kisasa zaidi
ambayo ni zaidi ya OB Van zinazotumiwa na kampuni nyingine za Afrika.
Ikiwa imegharimu kiasi cha Euro 4 milioni, OB Van
hiyo ililetwa nchini na Kampuni ya Broadcast Solutions ya Ujerumani
chini ya mhandisi wake maarufu, Armando Santos ambaye ameondoka nchini
jana Ijumaa baada ya kuendesha mafunzo maalumu ya jinsi ya kuitumia OB
Van hiyo.
SOURCE:MWANASPOT
SOURCE:MWANASPOT
0 comments :
Post a Comment