-->

DAKTARI AFIKISHWA KIZIMBANI KWA KOSA LA KUMBAKA MGONJWA


DAKTARI Dhamana wa kituo cha afya Kombeni wilaya ya Magharibi Unguja, anadaiwa kumbaka msichana wa miaka 18, ambae alikwenda kupata matibabu.

Daktari huyo alifikishwa katika kizimba cha mahakama ya Mkoa Vuga kujibu shitaka hilo, ambalo alilikana kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Mshitakiwa huyo alietajwa kwa jina la Suleiman Said Omar (39), alidaiwa kutenda kosa hilo huko Kombeni kwa kumuingilia kwa nguvu msichana huyo (jina linahifadhiwa) na kumsababishia maumivu makali.

Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Abdalla Mgongo alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya mkoa, Essaya Kayange, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa kutumia nafasi yake kama Daktari Dhamana.

Alidai kitendo hicho alikifanya kituo cha afya Kombeni wilaya ya magharibi Unguja.

Kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar namba 6 ya mwaka 2004, kitendo hicho ni kosa chini ya vifungu vya sheria namba 125 (1) (3) (c) na 126 (1).

Mashitakiwa alikana shitaka hilo na kuiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo halikupingwa na upande wa mashtaka.

Pamoja na kukana, wakili wa serikali alidai yupo tayari kuthibitisha shitaka hilo baada ya ushahidi kukamilika.

Hivyo umeiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa, pamoja na kutolewa hati za wito kwa mashahidi.

Mshitakiwa yuko nje baada ya kudhaminiwa na watu watatu wenye vitambulisho na mmoja akiwa ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sambamba na kuwasilisha fedha taslimu shilingi 500,000.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 18 mwaka huu kwa kusikilizwa na upande wa mashitaka umetakiwa kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
SOURCE:ZANZI NEWS
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment