-->

GAZETI LA MWANANCHI NA MTANZANIA YAFUNGIWA

Serikali imeyafungia  kutochapishwa Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia  27 Septemba,2013  kutokana na mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari  na makala  za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi  wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano  ulipo nchini.

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa  kutochapishwa kwa siku kumi na nne(14) kuanzia 27 Septemba,2013.Adhabu  hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali(Government Notice )Namba 333 la  tarehe 27 septemba,2013.

Gazeti la MWANANCHI limepewa  adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo  wa uchochezi na uvunjifu wa amani,mfano tarehe 17 Julai,2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI
2013”  kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya
habari waraka huo ulikuwa wa Siri  haukupaswa kuchapishwa Magazetini.


Aidha, katika toleo la Jumamosi,tarehe 17 Agosti,2013 lilichapisha habari
yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI”  habari  hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa  mkali mwenye hasira.Habari na picha  hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika
maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam.Jambo ambalo halikuwa la
 ukweli.
Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo  halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti.Serikali na jeshi la Polisi  linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi  lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.

Hivyo basi,kwa gazeti hili kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya
kiislam  mbwa ni najisi hapaswi kuingia  katika maeneo ya ibada.

Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini(90) kuanzia  tarehe 27 Septemba,2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.Gazeti  hili limeonywa mara nyingi  lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa   kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za  fani ya
Habari.
Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia  maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20  Machi,2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA  DAMU”,tarehe 12 Juni,2013,toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo  “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”.

Aidha, siku ya Jumatano,tarehe 18  Septemba,2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha  Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo  ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia  kompyuta  kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika  .Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la  Polisi linahusika  na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana kwa  kumwagiwa tindikali na  waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya.

Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.

Kwaujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya
  wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama  wavione kuwa
haviwasaidii.

Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali  imelifungia gazeti la Mtanzania  kutochapishwa kwa muda wa siku  tisini(90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332(Government Notice No.332)  la tarehe 27 septemba,2013,. Serikali inawataka wamiliki,wahariri  na wanahabari kwa ujumla kuwa makini,kuzingatia weledi,miiko na madili  yataaluma uandishi wa habari.

Serikali inawataka wamiliki na hasa  wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa  vinazingatia taaluma,kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na  uzalendo wa hali ya juu.

Serikali inavionya vyombo vya habari  vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia  hatua kali ikiwemo ya kuvifungia .Serikali haitakubali kuona vyombo vya  habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani  nchini.
Imetolewa na

MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI,VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA,2013
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment