CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimetoa mwezi mmoja kwa
serikali kulipa malimbikizo yao ya madeni ya walimu yanayofikia bilioni
33.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, rais wa
chama hicho, Greisoni Mukoba, alisema wamechoka kupewa ahadi hewa na serikali ndio maana wamefikia hatua hiyo.
‘Tumetoa mwezi huu wa tisa uwe wa mwisho kuililia
serikali, baada ya hapo tutaamua hatua gani tufanye, maana tumekutana na
makatibu wakuu wa wizara zinazowahudumia walimu lakini bado tunaishia
kupewa ahadi hewa,” alisema Mukoba.
Mukoba aliongeza kuwa Agosti 14, mwaka huu, walikutana na
makatibu wakuu wanaowahudumia walimu pamoja na Katibu Mkuu ofisi ya
Rais Menejimenti ya Umma, wakatakiwa kuwasilisha madai yao yote.
“Tulikutana na makatibu, katika kikao hicho,
tuliwafahamisha kuwa walimu wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 33 na
mwisho wa kikao hicho
tulikubaliana CWT iwakilishe madai hayo ndani ya wiki mbili,” aliongeza
Mukoba.
Mukoba alisema wiki mbili zilipofika, walienda kuonana
tena na Katibu Mkuu, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
kuwasilisha vitabu vyenye madai mbalimbali ya walimu.
“Madai hayo tuliyaambatanisha kwenye barua Na
CWT/004/UTMS/VOL.11/94 na madai hayo sasa yamefikia sh bilioni sita,”
alisema Mukoba.
Mukoba aliishangaa serikali kuanzisha Mpango wa Matokeo Makubwa sasa
“Big Result Now”, huko walimu ambao ndio watekelezaji wakubwa wa mpango
huo, wana maisha magumu kutokana na mishahara kuwa midogo na kuzidi kwa
malikimbizo ya madeni yao.
“Walimu ambao ndiyo watelekezaji wakuu wa mpango huu japo hawaelewi au
hawajapewa semina elekezi, lakini ndio watekelezaji wakubwa.
Naishangaa serikali kuwadharau walimu na nakuhakikishia mpango huo hautafanikiwa kama walimu hawapati haki zao,” alisema Mukoba.
Mukoba aliionya serikali ikamilishe madai ya walimu ili wafanye kazi kwa moyo tofauti na sasa ambapo wengi wamekata tamaa.
‘‘Walimu wa nchi hii wamekata tamaa. Mioyo yao imekufa ganzi kwa sababu serikali imekataa kuwalipa malimbizo yao.
Kwa nini serikali imeamua kuwatendea jeuri walimu kiasi hiki?” alihoji Mukoba.
0 comments :
Post a Comment